JESHI la Polisi mkoani Singida limewaua kwa kuwapiga risasi
majambazi wawili waliokuwa wakijiandaa kufanya uhalifu katika Kijiji cha
Manga nje kidogo ya mji wa Singida.
Kamanda wa Polisi mkoani Singida, Godfrey Kamwela alisema tukio hilo
limetokea juzi, saa 12:00 jioni baada ya polisi kupata taarifa za siri
kutoka kwa raia wema.
Kamwela alisema majambazi hayo yalikuwa na bunduki moja aina ya SMG
yenye namba 34555 ikiwa na risasi saba kwenye magazine, huku wakitumia
pikipiki T 634 BTW Sanlg.
Aidha, Kamanda Kamwela alisema askari polisi walifika katika eneo
hilo, na watu hao walistuka kwa kuwa wanafuatiliwa na askari na hivyo
kuanza kukimbia kuelekea Kijiji cha Uhamaka kwa kutumia pikipiki hiyo.
Hata hivyo, alisema walipoona polisi wanawakaribia waliitelekeza
pikipiki hiyo na kuanza kukimbia porini kwa miguu, lakini hali
ilipokuwa ngumu zaidi walianza kuwarushia polisi risasi, hivyo polisi
nao walilazimika kujibu.
“Majibizano hayo ya risasi yalipelekea majambazi wawili kujeruhiwa
huku mmoja akifanikiwa kukimbia. Majeruhi hao walifariki dunia wakati
wakikimbizwa hospitali ya mkoa kwa matibabu. Maiti zimehifadhiwa
hospitalini hapo kwa ajili ya kutambuliwa na ndugu zao,” alisema
Kamwela.
Alisema kwenye eneo la tukio ilipatikana bunduki moja aina ya SMG
ikiwa na risasi saba na pikipiki iliyokuwa wakiitumia kukimbia. Polisi
wanaendelea na uchunguzi ili kubaini kama kuna mtandao wa majambazi
pamoja na kumsaka mtuhumiwa aliyekimbia.
Wakati huohuo, polisi mkoani hapa inawashikilia watu wanne akiwemo
mhudumu wa nyumba ya kulala wageni ya Lake Hill Singida Motel kuhusiana
na tukio la ujambazi lililotokea kwenye hoteli hiyo.
Kamanda Kamwela alisema wizi huo ulitokea juzi, saa 9:30 usiku,
ambapo watu ambao idadi bado haijajulikana wakiwa na bunduki walivamia
hoteli hiyo na kuwapora wapangaji vitu mbalimbali.
Alisema watu hao walipofika katika hoteli hiyo walifyatua risasi
hewani kwa lengo la kuwatisha wapangaji na walinzi na kufanikiwa
kuwafunga kamba walinzi wote watatu na kuingia katika vyumba viwili na
kuwanyang’anya wapangaji mali pamoja na fedha.
Aliwataja wanaoshikiliwa kwa tuhuma hizo ni walinzi hao wa kampuni
binafsi ya ulinzi ya Mass Security ya mjini Singida ambao ni Juma
Mwangwi (35), Zakaria Pastory (23) na Donald Samson (19) na Mhudumu wa
hoteli hiyo, Alistides Salvatory (24).
Kamanda Kamwela alitaja vitu vilivyoporwa kuwa ni kompyuta mpakato
moja, simu tatu za mkononi zenye thamani ya sh milioni moja, saa mbili
za mkononi moja yenye thamani ya dola 500 za Marekani pamoja na fedha
taslimu sh 800,000 na dola 500
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment