Home » » Singida watakiwa kuchangamkia Soko la Hisa

Singida watakiwa kuchangamkia Soko la Hisa

 WAJASIRIAMALI na wafanyabiashara mkoani Singida wametakiwa kuchangamkia fursa zilizopo Soko la Hisa la Dar es Salaam ili kuboresha na kuendeleza biashara zao.
Mwito huo ulitolewa juzi na Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk Parseko Kone wakati akifungua semina ya siku mbili juu ya Soko la kukuza ujasiriamali iliyofanyika ukumbi wa Aqua Vitae mjini hapa.
Dk Kone alisema kuwa Soko la Hisa la Dar es Salaam kupitia kitengo chake kipya kijulikanacho kama “Soko la Kukuza Ujasiriamali”, ni suluhisho la upatikanaji wa mitaji kwa wajasiriamali kote nchini.
Alisema kuwa soko hilo litatoa suluhisho kwa changamoto zinazowakabili wajasiriamali katika upatikanaji wa uhakika wa mitaji ya muda mrefu kwa ajili ya kuendeleza biashara zao, jambo ambalo limekuwa likiwasumbua wajasiriamali na wafanyabiashara.
“Kwa hiyo basi, soko la kukuza ujasiriamali litasaidia kuleta msukumo wa utekelezaji sera mbalimbali za serikali zinazolenga kuondoa changamoto hizo na kuleta urahisi wa upatikanaji wa mitaji kwa ajili ya kukuza biashara zao,” Dk Kone alisema.
Aidha, alieleza kuwa soko hilo linatarajiwa kulichangamsha soko kwa ujumla kupitia ongezeko la utoaji na uorodheshaji wa hisa, kupanua wigo na fursa za kuwekeza mitaji na kuongeza ari ya wananchi kujiwekea akiba.
Kwa mujibu wa mkuu wa mkoa huo, baadhi ya faida ziletwazo na soko hilo ni kupunguziwa kodi katika gawio, kusamehewa kodi kwenye ongezeko la thamani ya mtaji na ushuru wa stempu na punguzo kodi ya makampuni.
Chanzo;Habari Leo

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2011. Singida Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogz za Mikoa