Home » » Wavamia nyumba, wazichoma moto

Wavamia nyumba, wazichoma moto

MWENYEKITI wa Kijiji cha Makunda, Kata ya Kyengege, wilayani Iramba kwa kushirikiana na watu wengine zaidi ya 50 wamevamia na kuchoma moto nyumba mbili za wakulima wakipinga kuwa si wazaliwa wa eneo hilo na kujipatia ardhi zaidi ya ekari 285.
Habari za uhakika kutoka katika eneo la tukio hilo zinaeleza tukio hilo limetokea juzi, saa 8:00 mchana katika mashamba ya kilimo Kijiji cha Makunda.
Kwa mujibu wa habari hizo, siku ya tukio watuhumiwa wakiwa na silaha za jadi walivamia makazi ya mkulima mwezao, Esau Talanzia (47) na kuchoma moto nyumba yake.
Pia walichoma magunia sita ya mahindi, magunia mawili ya alizeti godoro moja, fedha taslimu sh 450,000 na vitu vingine vilivyokuwemo, vyote vikiwa na thamani ya sh milioni 1.8.
Pia katika tukio hilo nyumba moja ya Matayo Kizaberga, mkulima na mkazi wa Makunda-Mbugani ilichomwa moto na vitu vyote vilivyokuwemo kuteketea.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Singida, Geofrey Kamwela, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba watu 25 akiwamo mwenyekiti wa kijiji wanashikiliwa na polisi kuhusiana na tukio hilo.
Kamanda Kamwela alisema chanzo cha tukio hilo ni mgogoro wa mashamba ambapo wanakijiji cha Makunda wanapinga waathirika hao kumiliki ekari 284 wakati si wazawa wa eneo hilo.
Alisema watuhumiwa wanatarajiwa kufikishwa mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika.
Chanzo;Tanzania Daima

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2011. Singida Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogz za Mikoa