Home » » GHARAMA ZA MRADI WA UMEME ZAFIKIA MIL. 101/-

GHARAMA ZA MRADI WA UMEME ZAFIKIA MIL. 101/-



na Jumbe Ismaily, Singida
SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Singida, limesema gharama za mradi wa umeme kutoka Mtinko hadi Ikhanoda zimepanda kutoka sh milioni 23 mwaka 2004 hadi kufikia sh milioni 101 mwaka huu.
Meneja wa TANESCO Mkoa wa Singida, Maclean Mbonile, alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mwishoni mwa wiki iliyopita.
Alisema mradi huo ulioanza mwaka 2003 ulitarajiwa kukamilika mwaka 2004, lakini haukuweza kukamilika kutokana na sababu mbalimbali za kiufundi.
Alizitaja sababu zilizokwamisha mradi huo kuwa ni vifaa vyote vya mradi kupelekwa kwenye miradi mingine, licha ya taarifa zake kuonyesha kuwa vimepelekwa kwenye mradi huo.
Aidha, alisisitiza kutokana na mradi huo kukaa muda mrefu bila kukamilika, watendaji wa shirika hilo wamekuwa wakiingiwa ugumu kuuombea fedha na hivyo wananchi kuendelea kukosa huduma hiyo.
Alifafanua baada ya mashauriano ya muda mrefu uongozi wa TANESCO Mkoa wa Singida walilazimika kutoa ufafanuzi juu ya hilo na kufanikiwa kutengewa sh milioni 101 kwa ajili ya kuukamilisha mradi huo unaofadhiliwa na shirika hilo.
“Kwa kweli mradi huu umetusumbua sana namna ya kuukamilisha, kwani kila unapoomba fedha hatukufanikiwa kupata kutokana na taarifa zilizoandikwa kuwa mradi umekamilika na wananchi wameanza kupata huduma,” alisisitiza Mbonile.
Akizungumzia kupatikana kwa fedha za mradi huo, Diwani wa Ikhanoda, Hinga Mnyawi, alisema hali hiyo inaleta faraja kwa wananchi wa kata hiyo, kwani wamekuwa na hamu ya kupata huduma hiyo kwa muda mrefu.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2011. Singida Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogz za Mikoa