Na Nathaniel Limu, Singida
WAKALA wa Barabara (TANROAD) mkoani Singida,
umetumia zaidi ya Sh bilioni 4.4, kugharamia matengenezo ya barabara kwa
kiwango cha udongo na chagarawe.
Hayo yalisemwa juzi na Meneja wa TANROADS mkoani hapa, Mhandisi Yustaki Kagole,
wakati akitoa taarifa yake kwa Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk. Paseko Kone.
Kagole alisema, matengenezo hayo yalifanyika katika kipindi cha mwaka
2011/2012, ambapo matengenezo ya kawaida ya kilomita 637, yamegharimu zaidi ya
Sh milioni 897.
"Matengenezo ya vipindi maalumu ya kiliomita 102, yamegharimu zaidi ya Sh
bilioni 1.8 na matengenezo ya sehemu korofi yenye urefu wa kilomita 48.2, nayo
yamegharimu zaidi ya Sh milioni 640.6,” alisema.
Alisema mategenezo madogo kwa ajili ya kulinda na kutunza madaraja tisa,
yamegharimu Sh milioni 23.1, wakati matengenezo makubwa ya madaraja na ujenzi
wa makalavati manne, yamegharimu zaidi ya Sh milioni 351.3.
“Miradi midogo ya maendeleo ya barabara za mkoa zenye urefu wa kilomita 51,
umegharimu zaidi ya Sh milioni 714.3,” alisema.
Alisema lengo lao ni kuhakikisha kuwa, barabara zote zinapitika kwa urahisi
wakati wote wa mwaka kwa ajili ya kutia chachu maendeleo ya wananchi.
TANROADS mkoa wa Singida, unahudumia zaidi jumla ya kilomita 1,689.5, ambapo
kati ya hizo, barabara kuu (truck roads) ni kilomita 674.2 na barabara za mkoa
ni kilomita 1,015.3.
Hadi mei mwaka huu, mkoa ulikuwa na barabara za kiwango cha lami zenye urefu wa
kilomita 340 kwa barabara kuu.
Chanzo: Mtanzania
0 comments:
Post a Comment