Home » » ‘POLISI OMBENI VIBALI TANROADS’

‘POLISI OMBENI VIBALI TANROADS’



na Halima Jamal, Manyoni
KUTEUA kwa jeshi a polisi vituo vya vizuizi bila kupata kibali cha Wakala wa Barabarani (TANROADS), kumesababisha uharibifu wa barabara za lami zinazojengwa kwa gharama kubwa.
Hayo yamesemwa jana na Meneja wa TANROADS mkoani Singida, Yustaki Kangole, wakati akitoa taarifa yake kwa mkuu wa mkoa wa Singida, Dk. Parseko Kone, ambaye ameanza ziara ya siku mbili kukagua hali ya barabara.
Alisema Jeshi la Polisi kitengo cha usalama barabarani, limekuwa na tabia ya kuchagua maeneo yasiyofaa kwa ajili ya kuegesha magari makubwa kwa ukaguzi wao.
Aidha Kangole alisema ni vema jeshi hilo likaishirikisha TANROADS katika kuchagua maeneo ya ukaguzi wa magari ili uharibifu wa barabara hizo zinazojengwa kwa gharama kubwa usiendelee kutokea tena.
Meneja huyo aliyataja maeneo ambayo jeshi la polisi linayatumia bila ya ridhaa ya TANROADS kuwa ni Mzani wa Njuki, eneo la Ikungi, Manyoni na Misuna.
“Tunashauri uongozi wa mkoa, utoe maelekezo kwa polisi kuomba vibali TANROADS ili upewe maeneo ya vizuizi kwa kushauriana na TANROADS. Yapo maeneo maalumu katika barabara za lami ambayo magari mazito yanaruhusiwa kusimama bila kuleta madhara,” alisema Kangole.
Aidha Kangole alisema kuna tatizo jingine sugu la watumiaji barabara hasa madereva wa malori makubwa kutengenezea magari yao juu ya tabaka la lami na hivyo kuharibu barabara kwa jeki, mawe na mafuta ya magari.
“Pamoja na TANROADS kuanzisha kitengo cha elimu kwa umma, bado tatizo hili limeshamiri sana katika maeneo ya Mlima Saranda, Ikungi, Iguguno, Ulemo, Misigiri na Shelui. Tunadhani nguvu ya dola inahitajika katika hili,” alisema.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2011. Singida Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogz za Mikoa