Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
SERIKALI ya China imeiunga mkono serikali katika mkakati wake wa
kutoa elimu bure, ikisisitiza kuwa chini ya uongozi wa Rais John
Magufuli, Tanzania inasifika duniani.
Katika kuunga mkono elimu bure, ubalozi wa nchi hiyo nchini umetoa
msaada wa madawati 400 yenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 28 kwa shule
mbalimbali za msingi katika wilaya ya Iramba mkoani Singida.
Balozi wa China hapa nchini, Dk Lu Youq’ng alisema msaada huo ni moja
ya juhudi za nchi yake kuiunga mkono Serikali ya Tanzania katika kutoa
elimu bure. “Wakati mimi nimechangia madawati 300, Kampuni inayochimba
madini hapa ya Sun Shine Group imechangia madawati 100 ili kuniunga
mkono,” alifafanua.
Akikabidhi madawati hayo katika mikutano mitatu tofauti kwenye mji wa
Kiomboi, Shelui na Misigiri, Balozi Youq’ng alisisitiza umuhimu wa
Tanzania kuwekeza kwenye elimu kuwaletea wananchi wake maendeleo ya
kweli.
“Hata kama nchi ni maskini kiasi gani, lazima elimu itiliwe mkazo;
tena iwe ni elimu bora na elimu bora haiwezi kuja kwa wanafunzi kukaa
chini. “Madawati ni moja ya mambo ambayo yanamjengea mwanafunzi
mazingira mazuri ya kujifunzia,” alisema.
Aliongeza, “kutokana na umuhimu huo, ndio maana mbunge wenu
aliponijia na kuniomba msaada wa madawati, sikusita hata kidogo. Nilijua
anafanya hivyo ili kuisaidia jamii yake kuboresha elimu”. Aliyeomba
msaada huo ni Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba.
Aidha, balozi huyo amewapongeza wakazi wa mkoa wa Singida kwa
kumchagua Dk Magufuli kuwa Rais na kuongeza kusema kuwa chini ya uongozi
wake sasa Tanzania inasifika duniani kote. “Nitahakikisha nchi yangu
inaendelea kusaidia maendeleo ya nchi hii kwa kuwa urafiki wetu ni wa
enzi na enzi,” alisema.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mathew Mtigumwe alisema kuwa mkoa
unathamini msaada huo kwa kuwa umepunguza kwa kiasi kikubwa upungufu wa
madawati 4,016 ambayo wilaya hiyo ilikuwa nao.
Chanzo Gazeti La Habari Leo