Home » » Mkuu wa mkoa wa Singida aagiza waalimu wakuu wakajifunze matumizi ya fedha kwa mwalimu mkuu mwenzao

Mkuu wa mkoa wa Singida aagiza waalimu wakuu wakajifunze matumizi ya fedha kwa mwalimu mkuu mwenzao





Mkuu wa mkoa wa Singida Dk.Parseko Kone akizungumza na baadhi ya walimu wa shule ya sekondari Mwanzi Manyoni mjini.Dk.Kone hakufurahishwa na hali duni ya ofisi ya mkuu wa shule hiyo wakati shule ikiwa na akiba ya zaidi ya shilingi milioni sita.(Picha na Nathaniel Limu).
Mwalimu mkuu wa shule ya msingi mchanganyiko Ikungi wilaya ya Ikungi mkoani Singida, Olivary Kamili akiwa ofisini kwake akitekeleza majukumu yake. Mkuu wa mkoa wa Singida Dk.Parseko Kone ameagiza walimu wakuu wa shule za msingi na wakuu wa sekondari wafike shule ya msingi mchanganyiko Ikungi, ili wakajifunze juu ya matumizi bora ya fedha za Umma.(Picha na Nathaniel Limu).
Na Nathaniel Limu.
Mkuu wa  mkoa wa Singida Dkt. Parseko Kone amemwagiza mkurugenzi mtenadaji wa halmashauri ya wilaya ya Manyoni, achague walimu wakuu wanne wa shule za msingi na wakuu wa shule za sekondari wanne, awapeleke shule ya msingi mchanganyiko Ikungi, ili wakajifunze juu ya matumizi bora ya fedha za umma.
Akizungumza na walimu wa shule ya sekondari ya Mwanzi iliyopo mjini Manyoni pamoja na viongozi wa wilaya ya Manyoni Dkt. Kone amesema shule ya msingi mchanganyiko Ikungi wilaya ya Ikungi,ni shule ya mfano mkoani Singida kwa matumizi mazuri ya fedha za uuma.
Amesema Ofisi ya mkuu wa shule hiyo ni nzuri mno, pengine si rahisi kuifananisha na ofisi nyingi za wakuu wa wilaya. Ina samani za kisasa, tv, kompyuta, internet, jokofu na makochi ya hali ya juu na kuwa Ofisi kama ile inavutia na inachangia mhusika kubaki ofisini kipindi chote cha kazi.
Akifafanua zaidi, amesema majengo ya shule ya msingi mchanganyiko Ikungi pamoja na ujenzi wa uzio wa ukuta, yamekarabatiwa/kujengwa yana ubora unaofanana na thamani ya fedha zilizotumika.
Dkt. Kone amesema walimu wakuu wa shule za msingi na wakuu wa shule za sekondari, hawana budi kufika kwenye shule hiyo ili kujifunza mwenzao Olivary Kamilly (mwalimu mkuu wa shule ya msingi mchanganyiko Ikungi) anavyutumia fedha za umma vizuri.
Mkuu huyo wa mkoa, ametoa agizo hilo, baada ya kutokuridhishwa na hali duni ya ofisi ya mkuu wa shule ya sekondari Mwanzi mjini Manyoni, wakati shule hiyo benki ina zaidi ya shilingi milioni sita ambazo zimekaa kwa muda mrefu bila kutumiwa.
Katika hatua nyingine, Dkt. Kone amewaagiza watendaji wa halmashauri za wilaya na Manispaa, kujenga utamaduni wa kutembelea miradi mara kwa mara, ili miradi yote ya maendeleo iweze kutekelezwa kwa ubora unaofanana na fedha zilizotumika.
Amesema katika ziara yake wilayani Manyoni, amebaini baadhi ya miradi imetekelezwa chini ya kiwango na kitendo hicho kimechangiwa na viongozi kutokwenda vijijini  kutembelea miradi.
“Acheni tabia ya kukaa maofisini, jengeni utamaduni wa kusimamia kikamilifu miradi ya maendeleo, ili iwe na ubora unakusudiwa uweze kufikiwa”alisema Dk.Kone.
Aidha, amewataka kutunza vizuri miradi iliyomalizika na ile inayohitaji ukarabati, ifanyiwe ukarabati unaofanana na thamani ya fedha zitakazotumika.
Chanzo Mo Blog

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2011. Singida Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogz za Mikoa