MAHAKAMA ya Wilaya Manyoni mkoani Singida imemhukumu mkazi wa kijiji cha Matangalala wilayani humo, Maduhu Dotto (31) kwenda jela miaka 30 baada ya kumkuta na hatia ya kunajisi mtoto.
Aidha, Maduhu na mshitakiwa wa pili katika kesi hiyo, Juliana Malungo (28), wametakiwa kulipa faini ya Sh 200,000 kila mmoja.
Malungo ambaye ni mkazi wa mtaa wa Chang'ombe mjini Manyoni, alipatikana na hatia ya kula njama na Maduhu na kwamba ndiye aliyefanikisha kitendo cha kunajisi msichana mwenye miaka 14, kwa ahadi ya kumzawadia vitenge binti huyo.
Mwendesha Mashitaka, Mrakibu Msaidizi wa Polisi Hamis Fussi alidai mbele ya Kaimu Hakimu wa Wilaya ya Manyoni, Terrysophia Tesha kuwa Aprili 28 mwaka jana saa 6:45 mchana washitakiwa kwa pamoja walikula njama za kumnajisi binti huyo na kumsababishia maumivu makali sehemu zake za siri.
Fussi alidai kuwa siku ya tukio Juliana alikwenda nyumbani kwa mlalamikaji ( ambaye ndiye binti alinajisiwa) na kumshawishi binti huyo amsindikize mnadani.
Hata hivyo, hawakwenda mnadani, badala yake mshitakiwa alimpeleka binti huyo nyumbani kwake, ambako alikuwepo Maduhu na Juliana alimfungia ndani binti huyo wakiwa na Maduhu, naye akaondoka.
Alidai kuwa kutokana na kufungiwa huko, Maduhu aliamua kumwingilia kimwili binti huyo bila ridhaa yake na hivyo kumsababishia maumivu makali sehemu zake za siri.
Fussi aliiomba Mahakama itoe adhabu kali kwa washitakiwa, akidai kuwa vitendo vya kunajisi vinachangia mimba zisizotarajiwa na maambukizi ya magonjwa, ikiwemo wa Ukimwi.
Akitoa hukumu, Hakimu Tesha alisema kuwa ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka, umethibitisha bila kuacha shaka yoyote kuwa washitakiwa walitenda makosa hayo.
Chanzo Habari Leo
Chanzo Habari Leo
0 comments:
Post a Comment