Picha juu na chini ni Mbunge wa jimbo
la Singida mjini, Mh. Mohammed Gullam Dewji akihutubia wananchi kwenye
mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kituo cha mabasi cha zamani mjini
Singida.
Baadhi ya wananchi waliohudhuria
mkutano wa hadhara ulioitishwa kwa ajili ya mbunge wa jimbo la Singida
mjini Mh. Mohammed Gullam Dewji kuzungumza na wananchi wa jimbo lake.
Mbunge wa jimbo la Singida mjini, Mh.
Mohammed Gullam Dewji, akiwa anasalimiana na Wana CCM na wananchi wa
Singida mjini kwenye kituo cha mabasi cha zamani mjini Singida.
Na Nathaniel Limu.
Mbunge wa Singida mjini (CCM) Mh.
Mohammed Gullam Dewji amemwaga misaada mbalimbali ikiwemo kuwaongezea
mitaji wauza kahawa chungu, ambayo haijawahi kutolewa jimboni humo na
mbunge au mfadhili yeyote kwa wakati mmoja, kabla na baada ya Tanzania
kupata uhuru.
Misaada hiyo yenye thamani ya zaidi
ya shilingi milioni 87.9, ni pamoja na mabati 100 na mifuko ya saruji
100, kwa kila shule 17 za sekondari jimboni humo.
Misaada mingine ni vyereheni viwili kwa kila kata 19 na cherehani moja kwa kila tawi la CCM jimboni humo.
Pia vikundi 16 vya wajasiriamali
vikiwemo vya kung’arisha viatu, mafundi baiskeli, wapiga debe wa vituo
vya mabasi, wasukuma matoroli, wakereketwa wa mashina ya CCM,
watengeneza viatu vya kienyeji na baba, mama lishe, kila kimoja
kimeongezewa mtaji wa shilingi 500,000 taslimu.
Vifaa hivyo na mitaji ya biashara,
vimetolewa kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kituo cha
zamani cha mabasi mjini Singida.
Akizungumza kwenye mkutano huo wa
hadhara uliohudhuriwa na maelfu ya wana-CCM na wananchi kwa ujumla, Mh.
Dewji amesema msaada huo ni mwendelezo wa misaada yake anayoitoa kwa
ajili ya kuiunga mkono serikali katika kuwatumikia wananchi.
Amesema pia kuwa misaada hiyo ni
sehemu yake ya utekelezaji wa ilani ya CCM katika kuwatumikia wananchi
wa jimbo la Singida mjini.
Amesema “Tunatakiwa tujitume usiku na
mchana, ili tuhakikishe kila tuliyoyaahidi kwenye ilani yetu, yote
tumeyakamilisha, vinginevyo wananchi hawatatuelewa. Wananchi wanahitaji
utimilifu wa ahadi na sio uhodari wa kujieleza kwenye majukwaa”.
Katika hatua nyingine, Mh. Dewji
ametumia fursa hiyo kuwaomba viongozi na watendaji kuendelea na moyo
safi wa kuwatumikia wananchi bila kuchoka.
Amesema pia wawe waaminifu na
waadilifu kwa wananchi na waongozwe kwa dhamira iliyo njema, yenye
uzalendo wa kuipenda nchi yetu na watu wake.
Mbunge Dewji amesema “Tuendelee
kuhubiri amani na utulivu kwenye majukwaa, wakati wote tuwaelekeze
wananchi kwenye kujiletea maendeleo endelevu ya wakati huu na wakati
ujao”.
0 comments:
Post a Comment