DSC01222

Diwani wa CHADEMA kata ya Mungaa jimbo la Singida Mashariki, Matheo Alex (wa pili kushoto aliyenyanyua mkono juu) akiwa katika chumba cha mahakama ya hakimu mkazi mjini Singida akisubiri kusomewa shitaka lake la kukata kata ng’ombe sita mali ya Mary John mkazi wa kijiji cha Minyinga kata ya Mungaa.Wa pili kulia ni mtoto wa diwani Alex, Faraja na wa pili kushoto Bahati Sumbe (mwenye jacketi la njano) wameunganishwa kwenye kesi moja na diwani Alex.
Na Nathaniel Limu.
Kesi ya kukata kata ng’ombe sita inayomkabili diwani wa kata ya Mungaa kupitia tiketi ya CHADEMA, jimbo la Singida Mashariki Matheo Alex na washitakiwa wenzake wawili, inatarajiwa kuunguruma kesho asubuhi kwenye mahakama ya hakimu mkazi mjini Singida.
Washitakiwa wengine ni mtoto wa diwani huyo Faraja Matheo na mwingine ni mjomba wa diwani huyo Bahati Sumbe.
Ng’ombe hao waliokatwa katwa ni mali ya Mary John mkazi wa kijiji cha Minyinga kata ya Mungaa jimbo la Singida mashariki na wana thamani ya zaidi ya shilingi milioni 3.5 milioni.
Mei 17 mwaka huu wakati washitakiwa hao walipofikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza, mwendesha mashitaka Mussa Chemu amedai kuwa mnamo Mei 13 mwaka huu saa 5.00 asubuhi huko katika kijiji cha Minyinga, kwa makusudi washitakiwa wote kwa pamoja walishirikiana kukata kata ng’ombe sita mali ya Mary John.
Washitakiwa wamekana shitaka hilo na wako nje kwa dhamana ya kila mmoja amedhaminiwa na watu wawili ambao kila mmoja ametoa ahadi ya dhamana ya shilingi milioni tano.
Washitakiwa hao wanatetewa na wakili maarufu Tundu Lissu ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Singida Mashariki.
 Chanzo Mo Blog