SERIKALI imetakiwa
kuangalia uwezekano wa kutenga zaidi ya asilimia 40 ya fedha zinazokusanywa
katika uchangiaji huduma za matibabu, kwa ajili ya kutumika kwenye
kitengo cha maabara.
Hatua hiyo
itasaidia katika kuboresha kitengo hicho ambacho kinatajwa kuwa
huchangia zaidi ya asilimia 70 ya maamuzi ya Daktari katika kutibu iwapo
kitatoa matokeo na takwimu sahihi za uchunguzi wa magonjwa.
Wito huo
umetolewa leo na Rais wa Chama cha wanasanyansi wa maabara
za uchunguzi wa afya ya binadamu nchini bw Sabasi
Mrina, wakati akizungumza kwenye ufunguzi wa wiki ya maadhimisho ya
wana-taaluma wa maabara ambayo mwaka huu kitaifa inafanyika mjini Singida.
Bw Mrina amesema
ingawa inaaminika kuwa kitengo cha maabara ndicho kinachokusanya fedha
nyingi zaidi za uchangiaji huduma za matibabu, lakini chenyewe
kimebaki kuwa omba-omba kutokana kutopewa fedha kwa ajili ya
kukiboresha ili kiweze kutoa huduma nzuri zaidi kwa wagonjwa.
Mgeni rasmi katika
maadhimisho hayo Kaimu Mkuu wa mkoa wa Singida Bibi Queen Mlozi amesema kuna
haja ya kuboreshwa kwa huduma za uchunguzi wa magonjwa kutokana na
umuhimu wake katika tiba.
Wiki ya wataalamu wa maabara za afya
ilianza kuadhimishwa rasmi nchini mwaka 2011, ikiwa na lengo la kutoa elimu kwa
jamii juu ya umuhimu wa kuchunguza afya, kufanya tathimini ya
utendaji kazi, changamoto zinazojitokeza na kuweka mikakati mbalimbali kwa
ajili ya kuboresha kitengo hicho.
0 comments:
Post a Comment