WILAYA ya Iramba mkoani Singida
inatarajia kuanzisha machinjio ya kuku wa asili ifikapo Julai mwakani.
Mkuu wa wilaya hiyo bwana Yahaya Nawanda
amebainisha hayo Mjini Kiomboi wakati akifungua mafunzo ya siku
mbili juu ya ufugaji kuku kisasa na kuanzisha SACCOS ya wafugaji kuku
Amesema lengo la machinjio hayo ya kisasa
yaliyopangwa kujengwa katika mji wa Misigiri ni kuhakikisha kuwa kuku
wanaozalishwa wanaongezwa thamani kwa kuchinjwa na kusindikwa ili kukidhi
mahitaji ya soko badala ya kusafirishwa hai kwa adha kubwa na wengine kufa
njiani.
Amesema uamuzi wa kujenga machinjio
hayo umefikiwa baada ya kubaini kuwa licha ya ufugaji wa kuku wa asili
kuwa moja ya shughuli kuu za kiuchumi mkoani Singida, kumekuwepo na
changamoto mbalimbali.
Amesema miongoni mwa changamoto hizo ni
pamoja na ukosefu wa soko la uhakika na bei nzuri, uhaba wa madawa na
vifo vinavyotokana na magonjwa na mazingira magumu ya usafirishaji.
Amesema kujengwa kwa machinjio hayo na kunzishwa
kwa soko la kuku pamoja na kituo cha kutoa elimu juu ya ufugaji wa kuku
kisasa, vitasaidia kuwaingiza wananchi kufuga kuku kibiashara ili
kujikomboa kiuchumi.
Inakadiriwa kuwa zaidi ya kuku
milioni mbili wa asali wanafugwa mkoani Singida.
0 comments:
Post a Comment