Home » » Mkandarasi atishia kujitoa ujenzi wa barabara

Mkandarasi atishia kujitoa ujenzi wa barabara

KAMPUNI ya China ya Sinohydro imetishia kusimamisha ujenzi wa barabara ya lami ya Manyoni- Itigi mkoani Singida hadi Chaya mpakani mwa Tabora kutokana na kuidai Serikali zaidi ya Sh bilioni 14.7. Madai hayo ni sehemu ya gharama za ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 89.3 kwa kazi ambayo imekwishafanyika.

Hali hiyo inatajwa kuwa moja ya sababu za utekelezaji wa mradi huo kuwa nyuma kwa zaidi ya miezi sita sasa kutokana na mkandarasi kukabiliwa na uhaba wa fedha.

Mkandarasi mshauri wa mradi huo Nicholas Geyer kutoka Ireland, alisema kutokana na madai ya fedha kwa muda mrefu bila mafanikio, shughuli hiyo inaweza kusimamishwa wakati wowote.

Alisema hatua hiyo itakachelewesha zaidi ujenzi na kuigharimu Serikali kwa kulazimika kulipa fidia kwa mujibu wa sheria za mikataba.

Hata hivyo, Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Singida, Yustaki Kangole alisema anaamini Serikali italipa fedha hizo kumuwezesha mkandarasi kuendelea na ujenzi.

Alisema huo ni sehemu tu ya miradi mingi nchini inayodaiwa zaidi ya Sh bilioni 300.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk. Parseko Kone, aliyetembelea ujenzi wa barabara hiyo alisema na kuchelewa suala kubwa ni kuzingatia ubora.

Ujenzi wa barabara ya lami ya Manyoni-Itigi-Mkoani Singida hadi Chaya mpakani mwa Tabora unaogharimu zaidi ya Sh bilioni 100 ulitarajiwa kukamilika Desemba mwaka huu kwa mujibu wa mkataba.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2011. Singida Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogz za Mikoa