Home » » Wanafunzi wabuni kifaa cha kumwagilia

Wanafunzi wabuni kifaa cha kumwagilia


Wanafunzi wawili Fideli Samwel na Jafari Ndagula kutoka shule ya sekondari Ilongero, iliyopo mkoani Singida, wameibuka washindi katika mashindano ya sayansi kwa vitendo iliyoshirikisha mikoa 18 nchini.

Mashindano hayo yalishirikisha wanafunzi 120 kutoka  shule za sekondari 60 pamoja na walimu wao wa sayansi, kwa ajili ya kuonyesha ubunifu na vipaji vya kisayansi ili kuzalisha wataalamu wengi nchini.

Ndagula alizungumza na NIPASHE jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki baada ya kutangazwa kuwa mshindi, alisema kubuni kifaa cha umwagiliaji, hawakuwa na uhakika wa kushinda kwenye maonyesho hayo na kwamba wanamshukuru Mungu kuwafanikisha.

Kifaa hicho kinatumika kama pampu ya kusukuma maji ambayo ina mipira maalumu inayoweza kumwagilia shamba au bustani.

“Unajua mashindano yalikuwa magumu, karibu washiriki wote wamejiandaa vizuri walibuni vifaa ambavyo vinahitajika ndani ya jamii, hivyo tusikate tamaa bali kila mmoja asonge mbele,” alisema. 

Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba alisema katika kuhakikisha vipaji hivyo vinaendelezwa Serikali imetenga Sh. bilioni 26 kwa ajili ya ukarabati wa maabara zake na kujenga zingine kwenye shule zote nchini.

Alisema mpango huo utasaidia kuongeza kasi kwa wanafunzi kujifunza masomo ya sayansi kwa kuwa na maabara za kutosha na za kisasa, pia serikali inajenga mtandao wa ufundishaji (ICT) utakaounganishwa kwenye Mkongo wa Taifa na mwalimu kufundisha kimtandao.

Naye Balozi wa Ireland nchini, Flonnual Gilsenan, alisema Serikali yake itaendelea kulidhamini Jukwaa la vijana wanasayansi Tanzania (YST) ili kuhakikisha linatimiza malengo ya kuzalisha wataalamu.

“Nitaendelea kushirikiana na Serikali yangu kuendeleza ubunifu wa vijana wa Kitanzania kupitia YST, pia naishukuru serikali ya Tanzania kwa ushirikiano wao,”alisema.

Naye Mkurugenzi wa YST, Gozbert Kamugisha, alisema maonyesha hayo yanadhihirisha ubunifu wa hali ya juu kwa Taifa kupata wataalamu wa kutosha, ikiwa fursa hiyo itatumika kuboresha kazi zao.

Alisema YST inasaidia kuwatangaza wasayansi miongoni mwa vijana na kuwapa moyo wa kutafuta ufumbuzi wa matatizo yanayowakabili katika maisha ya kila siku.

Katika mashindano hayo mshindi wa kwanza alipata Sh. milioni moja, medali, kikombe na tiketi ya kwenda kushiriki mashindano ya wanasanyansi vijana nchini Ireland.
 
CHANZO: NIPASHE




0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2011. Singida Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogz za Mikoa