Home » » DOLA ZA MAREKANI MILIONI 132 KUTUMIKA MRADI MKUBWA WA UMEME WA UPEPO WA MEGAWATI 50 SINGIDA. KUTOA AJIRA 2,200

DOLA ZA MAREKANI MILIONI 132 KUTUMIKA MRADI MKUBWA WA UMEME WA UPEPO WA MEGAWATI 50 SINGIDA. KUTOA AJIRA 2,200



 

Mwenyekiti wa Kamati  ya Kudumu ya Bunge ya  Nishati na Madini, Richard Ndassa akitoa maagizo kwa Wakandarasi, Wataalamu kutoka Shirika la Umeme Nchini (Tanesco), Wizara ya Nishati na Madini na viongozi mbalimbali kwenye majumuisho  ya ziara ya kamati hiyo, baada ya kufanya ukaguzi wa miradi ya umeme mkoani Singida pamoja na kuzungumza na wananchi.
Mwenyekiti wa Kamati  ya Kudumu ya Bunge ya  Nishati na Madini, Richard Ndassa (katikati) akisisitiza  jambo  katika eneo la mradi wa kuzalisha umeme kwa njia ya  upepo lililopo Kisesile wilayani Singida Mjini  mara kamati hiyo  ilipotembelea mradi huo ili kujionea maendeleo yake pamoja na kuzungumza na watendaji wa eneo hilo.



Na Greyson Mwase, Singida.

Mkuu wa Kitengo cha Miundombinu  na  Nishati  kutoka Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC)  Pascal Malesa  amesema kuwa serikali inatarajia kutumia   Dola za Marekani  Milioni 132 kwa ajili ya kukamilisha mradi wa kuzalisha umeme wa upepo wenye uwezo  wa Megawati 50 ifikapo  mapema mwaka 2016.

Malesa aliyasema hayo mbele ya Kamati ya  Kudumu ya Bunge  ya Nishati na Madini  iliyofanya ziara ya kutembelea mradi wa kuzalisha  umeme kwa njia ya upepo unaojengwa  katika eneo la  Kisesile  nje kidogo ya  Singida  Mjini. Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini  ipo mkoani  Singida kwa ajili ya kukagua miradi ya umeme ili kujionea maendeleo yake pamoja na kuzungumza na wananchi.

Alisema mradi huo  unatekelezwa kwa ubia kati ya  Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) lenye asilimia 60, Shirika la Umeme Nchini (Tanesco) lenye  asilimia 20 na kampuni ya  Power Pool  East  Africa Limited yenye asilimia 20 chini ya kampuni ya ubia iitwayo  Geo  Wind Power  Tanzania  Limited  (Geo Wind)  iliyoundwa mwaka 2011.

Malesa alieleza kuwa gharama hizo zinahusisha utekelezaji wa mradi huo  awamu ya kwanza kwa ajili ya kuzalisha megawati 50 ambayo itahusisha ujenzi  wa msongo wa umeme  wa kilovolti 220 umbali wa kilomita 12 na kuunganisha kwenye gridi ya  taifa.

Alisema  fedha hizo ni  mkopo kutoka  Benki ya  Exim  ya  China na  kuongeza  kuwa kwa  sasa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) linafuatilia mkopo  huu chini  ya udhamini wa Serikali  kupitia  Wizara ya  Fedha  baada ya kukamilisha  vigezo vyote  vya mradi vilivyotolewa na benki hiyo kwa ajili ya kupata mkopo  wa masharti nafuu na kuviwasilisha benki ya Exim ya  Serikali ya watu wa  China.


Alieleza kuwa baada ya  Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya   Fedha kuwasilisha maombi  ya mkopo kwenye Benki ya Exim  ya China mwaka 2013, ujumbe wa kwanza kutoka  benki hiyo  uliwasili Tanzania mapema Machi 2014 na kufanya uhakiki wa awali wa mradi.

Alisema pamoja na uhakiki wa mradi huo, ujumbe  huo ulifanya mazungumzo  na Wizara ya  Fedha na wanahisa wa mradi na kuongeza kuwa ujumbe wa pili  kutoka Benki ya Exim  ulifika Tanzania mapema Mei, 2014 na kufanya  uhakiki wa kina wa mradi ikiwa ni pamoja na kutembelea eneo la mradi mkoani Singida  na kufanya mazungumzo na uongozi wa mkoa wa Singida.

Akielezea hatua iliyofikiwa kuhusu mkopo, Malesa aliieleza kamati kuwa baada ya Serikali kupitia NDC kutimiza masharti  yote  ya mkopo  na  Benki ya  Exim  kutoka China  kufanya uhakiki wa mradi,  benki hiyo iliridhia  kutolewa kwa mkopo wenye masharti nafuu tangu mwezi  Septemba mwaka jana  kwa ajili ya ujenzi wa mradi huu.

Aliongeza kuwa hivi sasa Serikali kupitia  Wizara ya  Fedha iko katika majadiliano ya masharti ya mkopo na kusisitiza kuwa NDC inafuatilia majadiliano hayo  ili kuhakikisha kuwa yanasainiwa mapema ili kuanza ujenzi mara moja  ili kuendana na  Mpango wa Matokeo Makubwa  Sasa (BRN) ambao umeeleza wazi  kuhusu lengo la  serikali  kutekeleza na kukamilika kwa mradi huu mwaka 2016.

Akielezea matarajio ya mradi huo Malesa alisema mara baada ya kukamilika kwa mradi huo, mradi utaimarisha  uwezo wa Gridi ya Taifa hasa wakati  wa kiangazi kwa kuzalisha  umeme wa  uhakika na hivyo kusaidia uhifadhi  bora wa maji katika bwawa la Mtera na hivyo kupunguza makali ya mgawo  wa umeme nchini.

“ Mradi utalipunguzia Taifa mzigo wa kutumia  fedha za kigeni  kuagiza mafuta  ya dizeli yanayotumika kwenye mitambo ya kufua umeme wa dharura”, alisema Malesa
Malesa aliongeza kuwa vilevile  mradi utajenga uwezo wa kitaalam  kwa watanzania  kupitia progamu za kubadilishana uzoefu pamoja na ujuzi na kuongeza uhifadhi wa mazingira.

Alisema mradi utaingiza Dola za Marekani  milioni 23.2 kwa mwaka kutokana  na mauzo ya umeme na kutoa ajira zipatazo 2,200 na kusisitiza kuwa mradi utalipa kodi mbalimbali serikalini  ikiwa ni pamoja na  Kodi ya Ongezeko la Pato (VAT) na nyinginezo.

Akielezea changamoto za mradi  Malesa alisema ni pamoja na kuchelewa kwa upatikanaji wa mkopo kwa masharti nafuu  kutoka Benki ya Exim ili kugharamia ujenzi wa mradi na kuongeza kuwa  hali hiyo inatokana na Benki ya Exim kubadilisha  sera za riba nafuu kutoka asilimia  moja hadi mbili na muda wa mkopo kupungua kutoka miaka 25 hadi 20 huku  Wizara ya  Fedha  ikipendelea riba kuwa asilimia moja kama ilivyokuwa awali.

Akielezea mikakati ya kukabiliana na changamoto hiyo Malesa alisema kuwa NDC ikishirikiana na wanahisa wenzake, inafuatilia kwa karibu  sana upatikanaji wa mkopo  kutoka Benki ya  Exim mapema iwezekanavyo hasa ikizingatiwa kuwa mradi huu unatekelezeka kwa faida kwa kuzingatia masharti mapya  ya Benki ya Exim.

Akielezea suala la  fidia kwa wananchi waliopisha mradi huo  Malesa alisema kuwa jumla ya shilingi milioni 418 zililipwa kama  fidia kwa wakazi waliopisha mradi huo katika awamu  mbili tofauti.

Akielezea chagamoto wakati wa ulipaji wa fidia, Mkuu wa wilaya  ya  Singida Mjini anayehamishiwa katika wilaya ya Urambo Queen Mlozi, alisema  wapo wakazi sita wasiokuwa waaminifu walilipwa zaidi ya mara moja huku baadhi yao wakilipwa bila kuwa na  maeneo.

Mlozi alisema suala la watuhumiwa hao ofisi yake imeshalikabidhi katika Ofisi ya Taasisi  ya Kuzuia  na Kupambana na  Rushwa (Takukuru) kwa hatua zaidi. Wakati huohuo  akizungumza kwa niaba ya Kamati ya  Kudumu ya  Bunge ya Nishati na Madini, Mwenyekiti wa kamati hiyo  Richard Ndassa aliitaka serikali kuharakisha mchakato wa mkopo kutoka  Benki ya  Exim ili mradi huo  uanze mara moja na mkoa wa Singida uanze kunufaika na mradi huo.

Ndasa alisema  kuwa mbali na uwezo wa kuzalisha megawati 50, mradi huo una uwezo wa kuongeza hadi megati 300 kiasi ambacho ni kikubwa kwenye  Gridi ya Taifa.

Alisema mbali na  kupunguza tatizo la mgawo wa umeme,  mradi huo pia utapelekea punguzo la bei ya umeme kutoka  shilingi za kitanzania senti 30 ya awali hadi senti 13 na hivyo kuchangia kwenye  ukuaji wa uchumi wa nchi.
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2011. Singida Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogz za Mikoa