Mkuu wa
Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi amelishukuru Shirika la Nyumba
Taifa (NHC) kwa msaada wa mifuko ya saruji 10, kofia za bati 20, mabati
90 ya geji 28 vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya shilingi 2.6 milioni
ukiwa ni msaada kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa bweni la sekondari
Mwanzi iliyoko Wilayani Manyoni Mkoani Singida.
Dkt.
Nchimbi ametoa shukrani hizo juzi wakati akipokea masaada huo kutoka
kwa Meneja wa NHC Mkoa wa Singida Ladislaus Bamanyisa na kutoa wito kwa
mashirika, watu binafsi na taasisi zikiwemo mabenki, kuiga mfano mzuri
wa NHC kusaidia serikali katika kuboresha sekta mbalimbali ikiwemo ya
elimu.
“Mimi
nitumie nafasi hii kuwaita au kuwaalika mabenki na taasisi zingine kuja
mkoani Singida kutuunga mkono katika kutekeleza miradi mbalimbali ya
maendeleo ya wananchi, pamoja na uboreshaji wa miundo mbinu ya shule za
msingi na sekondari”,amesema.
Ameongeza
kuwa benki, shirika au watu binafsi watakaojitokeza kuunga mkono
kuuendeleza Mkoa wa Singida kwa kujenga jengo lo lote pamoja na majengo
ya shule, huduma za afya na mengine yanayolenga kuwanufaisha wananchi,
wataruhusiwa kupaka rangi na kuweka nembo zao ili kutangaza shughuli au
huduma wanazotoa.
Amesema
kwa njia hiyo benki, taasisi au watu binafsi watakuwa wamejitangaza na
tangazo hilo litadumu kwa muda mrefu ikilinganishwa na matangazo
mengine.
“Kwa
upande wa wadau binafsi na wao wataruhusiwa kuweka picha za familia zao
kwenye majengo au miradi husika. Kama ni mfugaji na ameuza sehemu ya
mifugo yake kugharamia miradi wa umma, ataruhusiwa kuweka picha ya
familia na ng’ombe zao”, amesema Dkt. Nchimbi.
Naye
Meneja wa NHC Mkoa wa Singida Ladislaus Bamanyisa, amesema wataendelea
kuiunga mkono serikali katika kuboresha sekta mbalimbali na huo mchango
ni sehemu ndogo ambapo shirika bado linaendele ana jitihada za kukusanya
michango mingine.
Wakati
huo huo Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Nchimbi amezungumza na watumishi
wa halmashauri ya Wilaya ya Manyoni na kuwaeleza kuwa halmashauri za
wilaya na manispaa zimekuwa ni chanzo au viwanda vya kuzalisha mabango
na kelele nyingi kwa wananchi kutokana na huduma zisizokidhi mahitaji na
ubadhirifu wa fedha za umma.
Dkt.
Nchimbi ameongeza kuwa ataelekeza nguvu zake kuanzisha na kufufua
kilimo cha umwangiliaji na ufugaji wa samaki ili Mkoa uweze kunufaika
kiuchumi na ujio wa makao makuu kuhamia mkoa jirani wa Dodoma.
“Sisi
wakazi wa mkoa wa Singida sote ni lazima tujiandae kikamilifu kulisha
makao makuu ya nchi yatakapokuwa Dodoma. Tuitumie fursa hiyo kumtokomeza
adui umaskini”, amesisitiza.
Naye
Mkuu wa Wilaya ya Manyoni Geofrey Mwambe amesema wakati wanaendelea na
ujenzi wa bweni halmashauri ya Manyoni imejipanga pia kujenga uzio
katika shule hiyo ya sekondari ya Mwanzi ili kuboresha ulinzi katika
shule hiyo.
Mwambe
amesema kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wanamalizia ujenzi wa
bweni moja na kuanza ujenzi wa bweni lingine huku akiwashukuru
wafanyabiashara wa Wilaya ya Manyoni kwa kujitoa katika kusaidia
maendeleo ya Wilaya hiyo.
0 comments:
Post a Comment