Home » » Jamii yaombwa kusaidia makundi maalumu yasiyojiweza.

Jamii yaombwa kusaidia makundi maalumu yasiyojiweza.


Mkuu wilaya Iramba-Singida, Yahaya Nawanda akikabidhi msaada wa madaftari kwa mwanafunzi Hilda Samwel (12) uliotole na vikundi vitatu vya jumuiya ya kuweka na kukopeshana (SELC).
Na Nathaniel Limu
Mkuu wa wilaya Iramba mkoani Singida, Yahaya Nawanda ameitaka jamii kusaidia makundi yasiyojiweza, wakiwemo watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi, ili kujenga moyo wa upendo baina yao.
Nawanda alisema hayo wakati akikabidhi vifaa mbalimbali vya shule msingi, kwa ajili ya wanafunzi wa shule sita  za watoto wanaoishi kwenye mazingira hatarishi, wilayani humo.
Msaada huo ulitolewa na vikundi vitatu vya jumuiya ya kuweka na kukopeshana(SELC), ambavyo kila mwanachama huchangia Shilingi mia tatu, kwa ajili ya kusaidia makundi mbalimbali yasiyojiweza, wilayani Iramba.
Alibainisha kuwa, msaada siyo lazima iwe kitu chenye thamani kubwa, bali waweza kuwa hata wenye thamani ndogo, lakini utakuwa umewaondoa wahitaji kutoka hatua moja hadi nyingine, kulingana mahitaji yao.
Msaada huo uliojumuisha sare za shule, madaftari, rula na kalamu, ulitolewa kwa wanafunzi 74 wa shule sita za msingi katika kata ya Kiomboi, ikiwemo Kiomboi hospitali, Salala, Lulumba shule ya msingi na Sekondari, Igumo, Kiomboi Bomani na Kizega.
Vikundi hivyo vitatu vinavyounda jumuiya hiyo ambavyo kila kimoja kina wanachama 30 ni Msweki, Loelya na Umoja, ambavyo kwa pamoja vimeshirikiana kutoa msaada huo wenye thamani ya Sh. 395,000.
Mapema akisoma risala ya vikundi hivyo kwa mgeni rasmi, katibu wa Msweki, Johari Manguli alisema wamelazimika kutoa msaada huo kutokana na wanafunzi hao kufiwa na wazazi wao wote wawilina wengine mzazi mmoja.
Aidha Johari aliomba wadau, wafadhili na mashirika yenye uwezo kujikita zaidi kusaidia makundi mbalimbali yenye matatizo, wakiwemo watoto waliofiwa na wazazi wao na wale wanaoishi kwenye mazingira hatarishi.
Hata hivyo baadhi ya wazazi na walezi katika hafla hiyo waliofiwa na waume wao,pia wanafunzi waliopoteza wazazi wao, walieleza kwa masikitiko tabu na shida wanazopata katika kukabaliana na maisha ya kila siku.
DC Iramba Yahaya Nawanda akimkabidhi mwanafunzi Jacob David (11) wa shule msingi Kiomboi hospitali msaada wa madaftari uliotole na vikundi vitatu vya jumuiya ya kuweka na kukopeshana (SELC).

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2011. Singida Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogz za Mikoa