Home » » WATUMISHI WA UMMA WACHANGISHWA UJENZI WA MAABARA

WATUMISHI WA UMMA WACHANGISHWA UJENZI WA MAABARA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Gratian Mukoba
Serikali imebuni utaratibu wa kuchangisha fedha za ujenzi wa maabara kwa kuwachangisha walimu na watumishi wengine wa umma.
Zoezi hilo linatekelezwa na wakurugenzi watendaji wa halmashauri nchini, ambao baadhi wameandika barua kwa waratibu elimu wa kata kutekeleza uchangishaji huo na kuwasilisha fedha hizo kwenye halmashauri.

Kwa mujibu wa barua ya Septemba 15, mwaka huu, kutoka moja ya halmashauri nchini (jina limehifadhiwa) kwenda kwa waratibu wa elimu wa kata, ikiwa na kichwa cha habari cha `Michango ya maendeleo kuchangia ujenzi wa maabara', imewataka waratibu hao kukusanya fedha hizo kutoka kwa walimu.

Aidha, barua hiyoambayo NIPASHE imeiona nakala yake, imeeleza kuwa kulingana na agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania juu ya ukamilishwaji wa maabara katika shule zote za sekondari nchini, uongozi wa halmashauri umeridhia uchangiaji huo.

“Kwa barua hii, naagiza uchangiaji wa ujenzi wa maabara kutokana na maamuzi ya wilaya,” ilieleza sehemu ya barua hiyo.

Barua hiyo ilitaja viwango vya uchangiaji kuwa ni Sh. 60,000 (waratibu elimu kata), Sh. 60,000 (walimu ngazi ya mshahara TGTS F-G), Sh. 30,000 (ngazi ya mshahara TGTS D-E) na Sh. 20,000 ( TGTS B-C).

Aidha, barua hiyo ilieleza kuwa michango hiyo itatolewa kwa awamu mbili Septemba na Oktoba, mwaka huu.

Barua hiyo pia imeagiza walimu wakuu kusimamia michango hiyo kwa shule zao na kufikisha fedha hizo halmashauri.

Katika Wilaya ya Same, baadhi ya wakuu wa shule walisema wamepata maelekezo ya wazazi wenye watoto wa kidato cha kwanza kuchangia Sh. 30,000 na kidato cha pili hadi sita kuchangia Sh. 20,000, ambazo zinapaswa kuwasilishwa kwa wakuu wa shule, ambao watazipeleka halmashauri.

Baadhi ya wauguzi waliozungumza na NIPASHE kwa njia ya simu kutoka mkoani Manyara, walithibitisha kupewa barua zinazowataka kuchanga fedha hizo kwa ajili ya ujenzi wa maabara nchi nzima.

“Tumeuliza juu ya utaratibu huu, wamesema ndiyo utekelezaji wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN)…mchango huu unafanywa kama wa lazima kwa kuwa msimamiaji ni bosi wa walimu,” alisema mmoja wa wauguzi.

Aidha, baadhi ya walimu wamelalamikia utaratibu huo na kueleza kuwa kwa kuwatumia walimu umeonekana kuwa wa lazima, huku walimu wakiwa na mishahara duni, madai serikalini na kudhulumiwa stahili zao mbalimbali.

Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Gratian Mukoba, akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu, alithibitisha kupokea malalamiko ya walimu kwenye wilaya tofauti nchini.

“Nilipokea malalamiko yakielezea barua hiyo inayowataka kuchangia. Tumewaagiza viongozi wa CWT kushughulikia ili iwe kwa hiari na siyo kukatwa kwenye mishahara,” alisema Mukoba.

Alisema iwapo fedha hizo zitakatwa moja kwa moja kwenye mishahara ya walimu haitakuwa sahihi.Mukoba alisema makato ya kisheria yamewekwa wazi, ambayo ni mfuko wa hifadhi ya jamii na kodi.

Hivyo, akasema inapojitokeza michango mingine, maamuzi yanapaswa kufanywa na walimu wenyewe na siyo kutoa maelekezo kutoka juu kwenda chini.“Mwalimu ndiye atoe idhini ya mshahara wake kukatwa.

Siyo vibaya maabara kujengwa. Lakini tatizo mchangishaji ni nani? Kuwatumia barua kutoka ngazi ya juu, ni kama kuwalazimisha bila kuongea nao,” alisema Mukoba.

Alisema ni vyema maamuzi yakaanzia chini kwa walimu wenyewe kuliko inavyofanyika sasa, kuanzia juu, ikiwa ni pamoja na kuwa na utaratibu wa wazi ambao haugubikwi na kiini macho.

“Lazima ijulikane mkusanyaji ni nani, atakusanya kiasi gani na atapeleka kiasi gani kwenye ujenzi huo. Tunahofia matumizi mabaya ya fedha,” alisema Mukoba.

NIPASHE ilimtafuta Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, alisema hana taarifa kuhusiana na suala hilo na kuelekeza aulizwe Katibu Mkuu.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2011. Singida Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogz za Mikoa