Home » » MAAMBUKIZI YA VVU YAPUNGUA

MAAMBUKIZI YA VVU YAPUNGUA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

TANZANIA imefanikiwa kupunguza viwango vya maambukizi mapya ya Virusi vya Ukimwi (VVU) kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto kutoka asilimia 26 mwaka 2009 hadi kufikia asilimia 15 mwaka 2012.
Hayo yalibainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk. Parseko Kone, wakati wa uzinduzi wa mpango wa ushirikiano ili kupunguza VVU na vifo vya wajawazito na watoto, iliyofanyika mjini Singida juzi.
Dk.Kone alifafanua kwamba pamoja na mafanikio hayo, serikali hivi sasa inalenga kutokomeza kabisa maambukizi hayo.
Mkuu wa Mkoa huyo pia alipokea msaada wa vifaa mbali mbali vilivyotolewa na Watu wa Marekani kupitia Shirika ka misaada la USAID kama sehemu ya Mpango wa dharura wa Rais wa Marekani wa kupambana na Ukimwi (PEFER).
“Ni katika utekelezaji wa mkakati huo wa kitaifa, leo nitazindua mkakati wa tokomeza maambukizi mapya ya VVU toka kwa mama kwenda kwa mtoto kwa mkoa wa Singida,”alisema.
Kwa mujibu wa Dk.Kone, takwimu zinaonesha kwamba hapa nchini kati ya wajawazito 100,000 wanaojifungua, 454 hufariki kutokana na matatizo wakati wa mimba au uzazi na watoto 26 hufariki dunia kati ya watoto 1,000 wanaozaliwa kila mwaka.
Awali, Mkurugenzi wa Tunawajali, Dk.Gottlieb Mpangile akitoa maelezo ya mradi huo, pamoja na kukabidhi msaada wa vifaa vyenye thamani ya sh. milioni 155, alivitaja vituo vitakavyonufaika na msaada huo kuwa ni hospitali za Mtakatifu Gasper, Caroluos, Misheni ya Kilimatinde na Kiomboi, Manyoni, Makiungu, Iambi, vitoa vya afya Ndago, Ikungi na Sokoine.
Alisema kuwa nia ya Tanzania ni kupunguza vifo vya akina mama wakati wa uzazi, jambo alilosema linawezekana.

Chanzo:Tanzania daima

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2011. Singida Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogz za Mikoa