Mkuu
wa wilaya ya Ikungi mkoani Singida, Gishuli Charles (kulia) akitoa
maelekezo juu ya mikakati ya kuboresha kilimo cha pamba mbele ya wajumbe
wa kikao cha kazi cha kutathimini zao la pamba msimu huu
kilichohudhuriwa na wajumbe kutoka bodi ya pamba na wadau wa zao hilo.
Dc Charles alikuwa mwenyekiti wa kikao hicho kilichofanyika kwenye
ukumbi wa mikutano wa ofisi ya mkuu wa mkoa mjini hapa. Kushoto ni kaimu
katibu tawala mkoa wa Singida,Mumba.
Baadhi
ya wajumbe wa kikao cha kazi cha kutathimini kilimo cha pamba cha msimu
huu kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa ofisi ya mkuu wa mkoa
mjini Singida.(Picha na Nathaniel Limu).
Na Nathaniel Limu, Singida
MVUA
zilizonyesha kwa mtawanyiko usioridhisha msimu huu na kusababisha ukame
mkali,zimeathiri zaidi ya hekta 2,000 za zao la pamba na mavuno
yanatarajiwa kuwa hafifu;imeelezwa.
Hayo
yamesemwa na mkuu wa mkoa wa Singida,Dk.Parseko Kone,wakati akifungua
kikao cha kazi cha wadau wa zao la pamba mkoani hapa, kilichofanyika
kwenye ukumbi wa mikutano wa ofisi ya mkuu wa mkoa mjini hapa.
Alisema
kwa kuzingatia hilo,mkoa wa Singida kwa kushirikiana na bodi ya pamba
umeona umuhimu wa kukutanisha wadau wa zao la pamba ili kujadili
maendeleo ya kilimo cha pamba cha mkataba ambacho kina tija zaidi.
Aidha,
Dk.Kone alisema kukutana huko pia zitatolewa taarifa za mafanikio na
changamoto mbalimbali zilizojitokeza msimu wa 2014/2015,na kuweka
mikakati ya kufanikisha masuala ya soko la pamba katika msimu huu.
“Napenda
tuelewe kuwa mkutano huu ni fursa nzuri ya kuwakutanisha viongozi na
wataalam wa ngazi ya wizara,mkoa,halmashauri na wakulima,ili kujadiliana
mafanikio yaliyopatikana,changamoto zilizopo na kuweka mikakati ya
kuhakikisha juhudi za kuongeza tija na faida katika uzalishaji wa zao la
pamba, zinaendelezwa”,alifafanua.
Katika
hatua nyingine,Dk.Kone alisema katika msimu huu jumla ya wakulima 821
wa zao la pamba,wamepewa mafunzo ya kilimo bora cha pamba.
Aidha,
alisema katika msimu huu jumla ya hekta 6,757 za pamba zimelimwa,chupa
11,346 za viuatilifu na mabomba 35 ya kunyunyizia pamba,yalisambazwa na
kampuni pekee inayoshughulkia zao la pamba mkoani hapa ya Biosustain ya
jijini Dar-es-salaam.
“Nitumie
fursa hii kuipongeza kampuni ya Biosustain kwa kazi nzuri
inayojishughulisha na kilimo cha mkataba mkoani mwetu.Kampuni hii
imeweza kufufua zao la pamba kwa kuanzisha kiwanda cha kuchambua
pamba.Mfumo wa kilimo cha mkataba umeweza kunufaisha wakulima
2,500”,alisema Dk.Kone.
Zao
la pamba ni miongoni mwa mazao makuu manne ya biashara yanayozalishwa
hapa nchini na linachukua nafasi ya nne kwa kuchangia uchumi wa
taifa.Wastani wa faifa wa uzalishaji, ni kilo 300 kwa ekari
ikilinganishwa na lengo lililowekwa la kufikia uzalishaji wa kilo 1,500
kwa ekari ifikapo mwaka huu wa 2015.
Kwa
mkoa wa Singida,hali ya uzalishaji wa pamba imekuwa ikibadilika kwa
kiasi kikubwa ikilinganishwa na mazao mengine ya biashara, kutokana na
kuyumba kwa bei ya zao hilo mwaka hadi mwaka.
Baadhi
ya mikakati ya kuimarisha kilimo cha pamba mkoani hapa ambayo imewekwa
na kikao hicho,ni pamoja na kuhamasisha kila kaya inalima si chini ya
ekari mbili kila msimu.
Mikakati
mingine ni halmashauri kushirikiana na wataalamu wa vipimo kuhakikisha
matumizi sahihi ya vipimo yanatumika wakati wa kuuza pamba,kuhimiza
kilimo cha mkataba na kila mdau wa kilimo cha pamba,atimize wajibu wake.
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.