Home » » Mvua zaathiri hekta 2,000 za zao la Pamba Mkoani Singida

Mvua zaathiri hekta 2,000 za zao la Pamba Mkoani Singida


DSC05358
Mkuu wa wilaya ya Ikungi mkoani Singida, Gishuli Charles (kulia) akitoa maelekezo juu ya mikakati ya kuboresha kilimo cha pamba mbele ya wajumbe wa kikao cha kazi cha kutathimini zao la pamba msimu huu kilichohudhuriwa na wajumbe kutoka bodi ya pamba na wadau wa zao hilo. Dc Charles alikuwa mwenyekiti wa kikao hicho kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa ofisi ya mkuu wa mkoa mjini hapa. Kushoto ni kaimu katibu tawala mkoa wa Singida,Mumba.
DSC05355
Baadhi ya wajumbe wa kikao cha kazi cha kutathimini kilimo cha pamba cha msimu huu kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa ofisi ya mkuu wa mkoa mjini Singida.(Picha na Nathaniel Limu).
Na Nathaniel Limu, Singida
MVUA zilizonyesha kwa mtawanyiko usioridhisha msimu huu na kusababisha ukame mkali,zimeathiri zaidi ya hekta 2,000 za zao la pamba na mavuno yanatarajiwa kuwa hafifu;imeelezwa.
Hayo yamesemwa na mkuu wa mkoa wa Singida,Dk.Parseko Kone,wakati akifungua kikao cha kazi cha wadau wa zao la pamba mkoani hapa, kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa ofisi ya mkuu wa mkoa mjini hapa.
Alisema kwa kuzingatia hilo,mkoa wa Singida kwa kushirikiana na bodi ya pamba umeona umuhimu wa kukutanisha wadau wa zao la pamba ili kujadili maendeleo ya kilimo cha pamba cha mkataba ambacho kina tija zaidi.
Aidha, Dk.Kone alisema kukutana huko pia zitatolewa taarifa  za mafanikio na changamoto mbalimbali zilizojitokeza msimu wa 2014/2015,na kuweka mikakati ya kufanikisha masuala ya soko la pamba katika msimu huu.
“Napenda tuelewe kuwa mkutano huu ni fursa nzuri ya kuwakutanisha viongozi na wataalam wa ngazi ya wizara,mkoa,halmashauri na wakulima,ili kujadiliana mafanikio yaliyopatikana,changamoto zilizopo na kuweka mikakati ya kuhakikisha juhudi za kuongeza tija na faida katika uzalishaji wa zao la pamba, zinaendelezwa”,alifafanua.
Katika hatua nyingine,Dk.Kone alisema katika msimu huu jumla ya wakulima 821 wa zao la pamba,wamepewa mafunzo ya kilimo bora cha pamba.
Aidha, alisema katika msimu huu jumla ya hekta 6,757 za pamba zimelimwa,chupa 11,346 za viuatilifu na mabomba 35 ya kunyunyizia pamba,yalisambazwa na kampuni pekee inayoshughulkia zao la pamba mkoani hapa ya Biosustain ya jijini Dar-es-salaam.
“Nitumie fursa hii kuipongeza kampuni ya Biosustain kwa kazi nzuri inayojishughulisha na kilimo cha mkataba mkoani mwetu.Kampuni hii imeweza kufufua zao la pamba kwa kuanzisha kiwanda cha kuchambua pamba.Mfumo wa kilimo cha mkataba umeweza kunufaisha wakulima 2,500”,alisema Dk.Kone.
Zao la pamba ni miongoni mwa mazao makuu manne ya biashara yanayozalishwa hapa nchini na linachukua nafasi ya nne kwa kuchangia uchumi wa taifa.Wastani wa faifa wa uzalishaji, ni kilo 300 kwa ekari ikilinganishwa na lengo lililowekwa la kufikia uzalishaji wa kilo 1,500 kwa ekari ifikapo mwaka huu wa 2015.
Kwa mkoa wa Singida,hali ya uzalishaji wa pamba imekuwa ikibadilika kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na mazao mengine ya biashara, kutokana na kuyumba kwa bei ya zao hilo mwaka hadi mwaka.
Baadhi ya mikakati ya kuimarisha kilimo cha pamba mkoani hapa ambayo imewekwa na kikao hicho,ni pamoja na kuhamasisha kila kaya inalima si chini ya ekari mbili kila msimu.
Mikakati mingine ni halmashauri kushirikiana na wataalamu wa vipimo kuhakikisha matumizi sahihi ya vipimo yanatumika wakati wa kuuza pamba,kuhimiza kilimo cha mkataba na kila mdau wa kilimo cha pamba,atimize wajibu wake.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2011. Singida Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogz za Mikoa