Home » » WAAHIDI KUCHAGUA VIONGOZI WATAKAOCHOCHEA KILIMO

WAAHIDI KUCHAGUA VIONGOZI WATAKAOCHOCHEA KILIMO

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.


WAKULIMA na wafanyabiashara wa mkoani Iringa wameahidi kuchagua viongozi watakaokuja na sera itakayoleta ufumbuzi wa haraka utakaoshawishi uzalishaji wa kilimo chenye tija kitakachotoa pia fursa kwa vijana wanaomaliza vyuo vikuu kujiajiri katika sekta hiyo. 

Wakishiriki mjadala wa kilimo na mnyororo wa thamani uliofanyika juzi katika Ukumbi wa Chuo Kikuu Huria mjini Iringa, wadau hao walisema wanashindwa kuamini kama mazingira ya sasa ya kilimo na biashara yake yanategemewa na asilimia 80 ya Watanzania.
 
Mjadala huo uliohusisha pia wawakilishi wa baadhi ya vyombo vya habari wa mjini Iringa, vyama vya wataalamu na wawekezaji wa kilimo, mifugo na wafanyabiashara uliandaliwa na East Africa Business and Media Training Institute kupitia mradi wake wa Best Dialogue Radio Project.

Mwenyekiti wa mradi huo, Rosemary Mwakitwange alisema mijadala hiyo inafanywa katika Mikoa ya Mbeya, Ruvuma, Iringa, Njombe, Rukwa na Morogoro inayotekeleza Mradi wa Ukanda wa Kilimo wa Kusini mwa Tanzania (SAGGOT).
 
“Lengo ni kuamsha mjadala utakaokifanya kilimo kiwe ni kazi ya faida na ya kudumu kwa wananchi kama sera ya kilimo inayoelekeza kuwa sekta ya kilimo inatakiwa kutoa mchango mkubwa katika kutengeneza ajira kwa vijana, na hivyo kutoa matumaini mapya kwa vijana waliomaliza shule,” alisema.

Mwenyekiti wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA) mkoani Iringa, Lucas Mwakabungu alisema wakulima wanajitahidi sana kuongeza tija lakini serikali imeshindwa kuboresha miundombinu itakayowahakikishia soko pamoja bei elekezi.
 

Mwakabungu alitoa mfano wa jinsi serikali inavyoshindwa kuwashirikisha wadau wake kukabiliana na tatizo la vipimo batili vya uuzaji mazao ya kilimo (lumbesa) vinavyoathiri na kunyong’onyeza nguvu kazi ya mkulima.
 
Urasimu, rushwa,gharama kubwa za pembejeo, ukosefu wa mikopo na usimamizi na ushiriki mdogo wa wataalamu wa sekta ya kilimo ni baadhi ya mambo yanayofanya biashara ya kilimo iwe ngumu na kufuta matumaini ya Watanzania wakiwemo vijana kuiona kama moja kati ya sekta muhimu zinazoweza kutoa ajira kwo,” alisema. 

Mfanyabiashara wa bidhaa za kilimo, Enock Ndondole alikosoa utaratibu wa serikali wa kuanzisha mambo mengi ya kuikuza sekta ya kilimo; mambo yanayoendelea kushindwa kumuinua mkulima wa kawaida.
 
Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Iringa (IUCo), Jackson Michael alisema shughuli ya kilimo haiwavutii vijana walio wengi kwa sababu ya changamoto zake na akawasihi vijana wenzake kushiriki Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu kwa kuwachagua viongozi watakonesha dhamira ya dhati ya kuikomboa sekta hiyo ili itoe ajira kubwa kwa Watanzania.
 
“Tunaambiwa asilimia 80 ya Watanzania wanategemea kilimo, kuna maswali ya kujiuliza kama kweli Watanzania hao wanalima au wanataka kulima na kama wanalima wanafanya hivyo ili iwe nini?...Maana tunashuhudia baadhi yao wanapewa pembejeo bure na badala ya kuzitumia mashambani mwao wanauza,” alisema.
Chanzo:Majira

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2011. Singida Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogz za Mikoa