KAIMU Mkuu wa Wilaya ya Iramba, mkoani Singida, Christopher
Ngubiagai, ameagiza kusimamishwa kazi na kuwafikisha kwenye vyombo vya
sheria watumishi watatu wa halmashauri hiyo kwa tuhuma mbalimbali,
ikiwamo matumizi mabaya ya madaraka.
Ngubiagai ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, mkoani humo
alitaja tuhuma nyingine kuwa ni kushindwa kutoa ushauri makini na
kusababisha upotevu wa fedha na nguvu za wananchi katika ujenzi wa bweni
la wasichana la shule ya sekondari Kinyangiri wilayani Mkalama.
Aliwataja watumishi hao kuwa ni David Malegi, Mhandisi Msaidizi
Ujenzi, Hashim Ndwata (Fundi Sanifu) na aliyekuwa Mratibu wa Mradi huo,
Jeremiah Lubeleje ambaye kwa sasa amehamishiwa wilaya ya Masasi mkoani
Mtwara.
Alieleza kuwa mradi huo wa ujenzi wa bweni la wasichana ulianza
Septemba 6, mwaka 2011 wakati wilaya ya Mkalama ikiwa haijagawanywa
kutoka wilaya mama ya Iramba.
Ngubiagai alisema wafadhili wa mradi huo, Ubalozi wa Japan walitoa
hundi ya Sh milioni 133.7 kwa ajili ya ujenzi wa bweni hilo ambapo
halmashauri ilipewa jukumu la kusimamia, kutoa ushauri wa kitaalamu,
kununua na kuweka vitanda na magodoro ujenzi utakapokamilika.
“Ujenzi wa hosteli hiyo ulikuwa ukamilike Aprili 18, mwaka 2012
lakini hadi hivi leo ( zaidi ya miaka minne) haujakamilika na jengo
limekaa bila kutumika, huku wasichana waliopaswa kulitumia wakitembea
kilometa 14 kwenda na kurudi hali inayowaathiri kitaaluma,” alisema
Ngubiagai.
Mkuu huyo wa Wilaya alisema kuwa licha ya ujenzi huo kutokamilika
kama ambavyo mkataba ulielekeza, uongozi wa halmashauri ya Iramba pia
umeshindwa kukabidhi bweni hilo kwa halmashauri ya wilaya ya Mkalama.
Kutokana na hali hiyo, alisema njia pekee ni kuwasimamisha kazi
wahusika wa mradi huo ili uchunguzi wa kina ufanyike na ikithibitika
wamehusika na tuhuma hizo hatua za ukiukwaji maadili ya utumishi wa umma
zichukue mkondo wake.
Kusimamishwa kwa watumishi hao watatu kunafanya idadi ya
waliosimamishwa katika halmashauri hiyo hadi sasa kufikia tisa. Februari
mwaka huu watumishi sita wa Idara ya Afya nao walisimamishwa kwa tuhuma
ya upotevu wa zaidi ya Sh milioni 145.2 za Mfuko wa Afya ya Jamii
(CHF).
CHANZO: HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment