Kutovaa helmeti kwagharimu maisha ya wapanda bodaboda Baadhi wapata 
ulemavu wa kupoteza kumbukumbu Polisi watangaza kiama kwa wasiovaa 
helmeti Na Shadrack Sagati BRUNO Sigala (24) amelazwa katika Taasisi ya 
Mifupa ya Muhimbili (MOI) kwa miezi mitatu tangu alipoanguka na bodaboda
 mkoani Singida.
Katika ajali hiyo alivunjika mikono yote, mguu moja na alitikisika 
ubongo na sasa hana kumbukumbu. Ingawaje huu ni mwaka 2016. Lakini 
Sigala kwa kukosa kumbukumbu, anasema ni mwaka 2018.
Hali kadhalika, wakati amelazwa wodini hapo kwa takribani miezi 
mitatu hadi sasa, yeye anadai kwamba ana miaka mitano tangu afikishwe 
katika wodi hiyo ya wagonjwa wa mivunjiko! Wauguzi wanaomhudumia 
wanaeleza kuwa Sigala anasubiri kufanyiwa upasuaji wa mikono na mguu 
baada ya kuhamishwa kutoka katika wodi inayoshughulika na majeraha ya 
kichwa.
"Alipoanguka na bodaboda aliumia vibaya kichwani, migugu pamoja na 
mikono. Alipofikishwa hapa madaktari waliangalia kipaumbele kwanza ni 
ubongo, baada ya kupata ahueni katika majeraha yake ya kichwa ndipo 
alipohamishiwa katika wodi hii ili aendelee na matibabu ya miguu na 
mikono," anasema Ofisa Uhusiano wa MOI, Patrick Mvungi.
Bruno Sigala ni kielelezo cha waendesha pikipiki maarufu kama 
bodaboda ambao wanaanguka na kuumia vibaya kichwani kutokana na kutovaa 
kofia ngumu ya kinga yaani helmeti kwa kimombo.
Kijana huyo alikuwa anafanya biashara ya kubeba abiria kwa pikipiki 
na aligongwa na gari katika ajali iliyomfikisha Muhimbili. Katika ajali 
hiyo, Sigala aliumia kichwani, akajing’ata ulimi na kuvunjika mikono 
yote na mguu mmoja. Akijieleza kwa kubabaisha anakiri kuwa hakuwa amevaa
 kofia wakati anaendesha pikipiki.
"Sikuwa najua umuhimu wa kofia hiyo, kwani mafunzo yenyewe ya 
kuendesha nilijifunzia tu mitaani, nikaanza biashara ya kubeba abiria."
Kofia ngumu zimetengenezwa kwa lengo la kumlinda mwendesha bodaboda 
asiumie kichwa pale apatapo ajali. Baadhi ya kofia hizi zinatengenezwa 
zikiwa na sehemu ya kupitishia hewa, kufunika uso usiathirike kwa kioo 
maalumu ambacho hata kikivunjika hakileti madhara kwa mvaaji pamoja na 
kulinda masikio.
Mwendesha pikipiki yuko hatarini kupoteza maisha pale apatapo ajali 
kama hakuvaa kofia ngumu. Tafiti zinaonesha kuwa kofia ngumu hupunguza 
hatari ya mwendesha pikipiki kuumia kichwa pale apatapo ajali kwa 
asilimia 69 na inapunguza kifo kwa asilimia 42.
Takwimu zilizopo katika Taasisi ya Mifupa (MOI) ya Hospitali ya Taifa
 ya Muhimbili ambazo zinahusisha miezi sita, Machi 15 hadi Septemba 15, 
2011, zinaonesha kwamba wapanda bodaboda wengi wanaojeruhiwa vibaya pale
 ajali za pikipiki zinapotokea, ni wale wasiovaa helmeti.
Wengi wao wanajeruhiwa vibaya kichwani. Daktari bingwa wa Magonjwa ya
 Mifupa katika Taasisi ya MOI, Dk Bryson Mcharo, anasema katika utafiti 
wake wa miezi 6 ukihusisha majeruhi wapatao 722, amebaini kuwa nusu ya 
majeruhi hao walipanda pikipiki bila kuvaa helmeti.
"Katika utafiti huo nilibaini kuwa madereva pikipiki ambao wanaona 
umuhimu wa helmeti ni wale ambao angalau wamepitia mafunzo ya udereva na
 wana leseni, lakini wengi wa majeruhi ambao hawakuvaa kofia hawana 
leseni na pia hawana mafunzo ya kuendesha pikipiki,” anaeleza Dk Mcharo.
"Karibia nusu ya majeruhi hao, asilimia 46, waliumia kichwani jambo 
linaloonesha kwamba madereva wengi na abiria wao hawazingatii uvaaji wa 
helmeti," anasema Dk Mcharo.
anasema kati ya majeruhi hao madereva wa pikipiki ndio wengi na zaidi ya nusu, asilimia 51.8, hawakuvaa helmeti.
Kwa mujibu wa Dk Mcharo, nusu ya majeruhi hao, walipata ajali baada 
ya kugongana au kugongwa na magari na asilimia 7 waligongana kati ya 
pikipiki na pikipiki huku asilimia 27 ni majeruhi waligongwa na 
pikipiki.
Mkuu wa Kitengo cha Dharura katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk 
Juma Mfinanga, anasema mwaka 2015 walipokea majeruhi 8,400 waliotokana 
na ajali za barabarani kiwango ambacho ni asilimia 61 ya majeruhi wote 
wa ajali waliofikishwa katika kitengo hicho.
Dk Juma anafafanua kuwa kati ya majeruhi hao asilimia 71 walikuwa ni 
madereva, asilimia 46 walikuwa ni abiria wakati asilimia 39 walikuwa ni 
waenda kwa miguu. Anasema kwa mwaka huu kuanzia Januari hadi Julai 
pekee, majeruhi wa pikipiki waliofikishwa kwenye kitengo hicho ni 4,900 
kiwango ambacho ni sawa na asilimia 64 ya majeruhi wote wa ajali za 
barabarani.
Anasema nusu ya ajali hizo (asilimia 51) ni majeruhi waliotokana na 
ajali za pikipiki, huku idadi ya wanaume ni mara tatu ya wanawake ya 
majeruhi wote waliofikishwa hospitalini hapo.
Dk Juma anasema majeruhi walioumia kichwani walikuwa ni asilimia 42 
na kati ya hao asilimia 8 hadi 10 ni wagonjwa waliojeruhiwa vibaya na 
kupona kwao ni kwa kudra za Mwenyezi Mungu, huku asilimia 85 hadi 88 ni 
wale ambao wameumia kwa kiwango cha kati na asilimia 61 ya majeruhi hao 
walivunjika mifupa mirefu ambayo ni mikono na miguu.
Majeruhi waliohamishiwa katika taasisi ya mifupa ni asilimia 89.1 ya 
majeruhi wa pikipiki waliopokelewa kituoni hapo mwaka 2015. Kuhusu 
gharama, Dk Juma anasema gharama zinatofautiana kulingana na hali ya 
mgonjwa, lakini akasema kwa wastani hospitali inatumia zaidi ya Sh 
650,000 kwa mgonjwa mmoja anayefikishwa katika kitengo cha tiba ya 
dharura kwa ajili ya kumtibia wakati wa dharura.
Uvaaji wa helmeti kwa dereva na abiria wa pikipiki ni moja ya 
masharti yaliyowekwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na 
Majini (SUMATRA) wakati wa kutoa leseni kwa dereva wa pikipiki.
"Lazima awe na helmeti na abiria wake pia atatakiwa kuvaa kofia ya 
kujikinga wakati wote na kwamba kofia hiyo inatakiwa kuwa na alama ya 
eneo la utoaji huduma ya usafiri," inasema kanuni ya usafirishaji ya 
pikipiki za magurudumu mawili na matatu ya mwaka 2010.
Kanuni hiyo inatoa masharti kwamba dereva wa pikipiki ya magurudumu 
matatu kwamba haruhusiwi kubeba idadi ya abiria zaidi ya mmoja, dereva 
wa pikipiki anatakiwa kuvaa kofia ngumu ya kujikinga wakati wote yeye na
 abiria wake.
Lakini jambo hilo halifanyiki. Pikipiki nyingi zinazobeba abiria 
zinatisha, unaweza kukuta dereva na abiria wake hawajavaa helmeti, au 
dereva anayo lakini abiria hana. Wakati mwingine unaweza kukuta dereva 
kavaa na abiria kaishikilia mkononi au kuipakata.
Hili limechangia dereva na abiria kupoteza maisha pindi inapotokea ajali.
Hili ndilo limemfanya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, 
kutahadharisha kwamba kupanda pikipiki bila kuvaa kofia ngumu ni dhamira
 ya kujiua, kwa sababu dereva na abiria wakipata ajali ni rahisi 
kupoteza maisha kwa kupigiza kichwa chini.
Makonda anawataka madereva wa bodaboda na abiria wao kuvaa helmeti. 
“Nimeshawasiliana na kamati yangu ya usalama barabarani mkoa. Hili 
nitalisimamia kikamilifu lazima wote wawe na helmeti,” anasema Makonda.
Mkurugenzi wa Udhibiti wa Usafiri wa Barabara wa Sumatra, Johansen 
Kahatano, anasema sheria ya Sumatra ya pikipiki inamtaka dereva wake 
avae helmeti wakati wote, kushindwa kufanya hivyo ni kuvunja sheria kwa 
makusudi. Kuhusu madai ya abiria kutopenda kuvaa hizo kofia, Kahatano 
anasema kwamba amekuwa anawashauri waendesha pikipiki wasipakie abiria 
ambao hawataki kuvaaa kofia ngumu.
"Usimamizi ni mgumu. Lakini tunaendelea kutoa elimu kwamba abiria 
akipanda pikipiki aone umuhimu wa kuvaa helmeti na kuthamini maisha 
yake. Hilo ni jambo la lazima. Sisi kama mamlaka tuna kazi ya kuendelea 
kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kuvaa kofia ," anasema Kahatano.
Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohamed Mpinga, hataki 
kumung’unya. Uvaaji wa kofia ngumu helmeti kwa waendesha pikipiki na 
abiria wao ni lazima. Yule ambaye atakaidi agizo hilo atakamatwa na 
kuchukuliwa hatua za kisheria. Itaendelea kesho. Inserts "Karibia nusu 
ya majeruhi hao, asilimia 46, waliumia kichwani jambo linaloonesha 
kwamba madereva wengi na abiria wao hawazingatii uvaaji wa helmeti" 
“Majeruhi walioumia kichwani walikuwa ni asilimia 42 na kati ya hao 
asilimia 8 hadi 10 ni wagonjwa waliojeruhiwa vibaya na kupona kwao ni 
kwa kudra za Mwenyezi Mungu.” “Kupanda pikipiki bila kuvaa kofia ngumu 
ni dhamira ya kujiua, kwa sababu dereva na abiria wakipata ajali ni 
rahisi kupoteza maisha kwa kupigiza kichwa chini.”
Chanzo Gazeti la Habari leo
Chanzo Gazeti la Habari leo
0 comments:
Post a Comment