Mkuu
wa Mkoa wa Singida Mhandisi Mathew J. Mtigumwe amezindua huduma tembezi
za madaktari bingwa humo na kuwasihi wananchi kujitokeza kwa wingi
kupata huduma hizo za kibingwa.
Huduma
zilizozinduliwa Wilayani Iramba katika hospitali ya Kiomboi zitahusisha
huduma za za upasuaji, meno, macho, upasuaji wa mifupa, huduma za
kibingwa za magonjwa ya watoto, wanawake na huduma za mionzi.
Mhandisi
Mtigumwe amesema matarajio ya mkoa huo ni kuwa huduma tembezi za
kibingwa zitasaidia kutambua na kutibu magonjwa mbalimbali kabla
hayajafikia hatua ya usugu na kupunguza gharama za rufaa za wagonjwa
kwenda nje ya mkoa.
“Huduma
tembezi za kibingwa zitawasaidia wananchi kutambua uwepo wa huduma za
kibingwa katika mkoa wa singida na kupata matibabu kwa gharama nafuu”
alisema Mhandisi Mtigumwe.
Naye
Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt. John Mwombeki akisoma taarifa ya hali ya afya
Mkoa wa Singida amesema wazo la kuanzisha huduma tembezi za kibingwa
limetokana na idadi kubwa ya operesheni zilizofanyika kwa mwaka
2015/2016 na pia mkutano wa wadau wa afya mkoani hapa kuafiki wazo la
kuanzisha huduma hiyo.
"Kwa
kipindi cha mwaka 2015/2016 jumla ya operesheni kubwa na ndogo 4,836
zimefanyika katika hospitali mbalimbali mkoani hapa, aidha Idara ya
macho katika hospitali ya Mkoa imefanya jumla ya operesheni kubwa na
ndogo 2,020" ameongeza Dkt. Mwombeki.
Dkt.
Mwombeki amesema uwepo wa madaktari bingwa 11 mkoani Singida pia
umekuwa chachu ya utekelezaji wa huduma hiyo huku Mkoa ukifanya jitihada
za kuazima madaktari wengine katika mikoa jirani ya Dodoma na Manyara.
Baadhi
ya wagonjwa waliohudhuria katika siku ya kwanza ya zoezi hilo huku
huduma hiyo ikitarajiwa kufanyika kwa muda wa siku tano wilayani hapo
wameeleza shauku na furaha yao ya kusogezewa huduma za kibingwa katika
halmashauri zao.
"Nilikuwa
naumwa jino ambalo limeota vibaya, niliambiwa nitaweza kufanyiwa
operesheni katika hospitali kubwa kama Muhimbili lakini hawa madaktari
wametusaidia , nimepata huduma haraka na kwa gharama nafuu, nawasihi
wenzangu waje kwa wingi" amesema Bi Neema Josseph Mkazi wa Kijiji cha
Kizaga Wilayani Iramba.
Naye
Mzazi wa mtoto Jonas Masaka amesema huduma za kibingwa zitamsaidia
mtoto wake mwenye matatizo ya macho na hiyo kumpunguzia gharama ya
kumpeleke katika hospitali kubwa kutibu tatizo la macho linalomsababisha
mtoto huyo kushindwa kusoma vizuri.
Huduma
ya tembezi za kibingwa Mkoani Singida zitafanyika katika Wilaya zote
tano za Mkoa nwa Singida na hvyo kupunguza wagonjwa wa rufaa
watakaopelekwa hospitali za Bugando, KCMC na Muhimbili.
0 comments:
Post a Comment