Na Beatrice Lyimo-MAELEZO
Serikali imetoa kauli kuhusu hali ya chakula nchini na kusema
kuna chakula cha kutosha pamoja na ziada ya asilimia 123.
Ziada hiyo ya chakula inatokana na uzalishaji wa msimu wa
mazao mwaka 2015/2016 ambao unapelekea upatikanaji wa chakula kwa mwaka
2016/2017.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dkt.
Charles Tizeba leo mjini Dodoma alipokuwa akitoa kauli ya Serikali kuhusu hali
ya chakula nchini.
“Takwimu zinaonesha upatikanaji na mahitaji ya chakula nchini
ni wa kuridhisha kwa kiwango cha utoshelevu wa ziada kwa asilimia 123” Dkt.
Tizeba.
Katika kufafanua hali hiyo, Dkt. Tizeba amesema kuwa kulingana
na takwimu zilizopo hali ya upatikanaji na mahitaji ya chakula nchini inautoshelevu
wa ziada kwa asilimia 123 ambapo nafaka ni asilimia 113 na mazao yasio ya nafaka
ni asilimia 140 ambapo viwango vya ziada kwa mazao yote ya chakula ni tani 3,013,515.
Dkt. Tizeba ameongeza kuwa Wakala wa Hifadhi ya Chakula ya
Taifa (NFRA) inauwezo wa kuhifadhi jumla ya tani 246,000 ambapo kufikia
Septemba 6, ilikuwa na akiba ya tani 67,506.920 za chakula kinachojumuisha
mahindi, mpunga na mtama.
Pia amesema kuwa
Serikali inaendelea na mpango wake wa kuiongezea NFRA uwezo wa kuhifadhi chakula
katika kanda sita baada ya kupata mkopo wa dola za Kimarekani million 55 kutoka
Serikali ya Poland ambazo zitatumika kujenga vihenge vyenye uwezo wa kihifadhi
tani 190,00 na maghala yenye uwezo wa kuhifadhi tani 60,000.
Kuhusu muda wa Serikali wa kutoa vibali vya kuuza chakula nje
ya nchi, Dkt Tizeba amesema kuwa lengo ni kutoa nafasi kwa Serikali kukamilisha
taarifa ya tathimini ya awali ya uzalishaji wa mazao ya chakula kwa mwaka
2015/2016 na hali ya upatikanaji wa chakula kwa mwaka 2016/2017.
Mbali na hayo, Dkt Tizeba amesema kuwa katika kuboresha hali ya usalama wa
chakula nchini, Serikali kupitia Wizara
ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi inapitia upya mfumo wa utoaji wa vibali vya
kusafirisha chakula nje ya nchi ili kuwezesha ufuatiliaji wa karibu kuliko
ilivyo sasa.
Aidha, Dkt. Tizeba amesema kuwa utoaji wa vibali vya
kusafirisha mazao nje umejitokeza baada ya kuona chakula kinasafirishwa nje
bila kufuata utaratibu maalumu ambapo wafanyabiashara wa nchi jirani walijihusisha
kununua vyakula vikiwa bado mashambani kabla ya kuvunwa.
Aidha, ametoa wito kwa wananchi kuhifadhi chakula cha kutosha
kwa matumizi katika kaya ambapo ameitaka sekta binafsi kuendelea kushiriki
katika kutoa masoko ya kununua na kuuza mazao katika maeneo yenye uhaba.
Kuhusu hali ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi
inayoikabili dunia ikiwamo upungufu wa mvua , Dkt Tizeba amesema kuwa Serikali itaendelea
na juhudi za kuhimiza na kupanua kilimo cha umwagiliaji mashambani kwa
kuimarisha miundombinu iliyopo na uvunaji wa maji ya mvua ili kuongeza
uzalishaji wa mazao wenye tija.
Hata hivyo, Serikali inaendelea kuhamasisha na kuelimisha
wafanya biashara kuuza unga nje ya nchi badala ya mahindi au mchele badala ya
mpunga ili kuendana na Sera ya kuendeleza Viwanda nchini na kuongeza thamani ya
mazao ya kilimo.
0 comments:
Post a Comment