Na Daudi Manongi,
MAELEZO.
Serikali kupitia Wizara ya
Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo limefanya mchakato wa upatikanaji wa Sheria ya
Huduma za Habari ambao umekuwa ni kilio kikubwa kwa wanahabari kwa zaidi ya
miaka 20 na sasa uko mbele ya kamati ya kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii ukikaribisha
maoni kutoka kwa wadau mbalimbali wa sekta ya Habari ambapo mpaka sasa asilimia
90 ya maoni yamepokelewa.
Muswada huu wa Sheria za Huduma za Habari wa
2016 umelenga kuboresha taaluma ya uandishi wa Habari nchini na kuifanya kuwa
rasmi mbele ya Jamii
Muswada
huu unapendekeza kutunga Sheria ya Huduma za Habari kwa madhumuni ya kuweka
utaratibu wa kisheria katika tasnia ya habari, kuunda Bodi ya Ithibati ya
Wanahabari, kuunda Baraza Huru la Habari, kushughulikia masuala ya kashfa,
makosa yanayohusiana na utangazaji na masuala yanayohusiana na hayo.
Muswada
huu umegawanyika katika Sehemu Nane. Sehemu ya Kwanza inahusika na masharti ya
ambayo ni jina la Sheria, tarehe ya kuanza kutumika, matumizi na tafsiri ya
misamiati na maneno yaliyotumika.
Sehemu
ya Pili inahusika na Idara ya Habari kuwa Masemaji Mkuu wa Serikali, majukumu
ya Mkurugenzi wa Idara ya Habari, aina za umiliki wa vyombo vya habari, inatoa
wajibu kwa vyombo vya habari kutoa habari kwa Umma na Serikali na pia
inaainisha wajibu wa vyombo vya habari binafsi kutoa habari na kulinda maadili
ya kitaaluma ya vyombo vya habari, utoaji leseni kwa magazeti, ufutwaji wa leseni
na utaratibu wa kutoa malalamiko.
Sehemu
ya Tatu inamaanisha masharti yanayohusu uanzishwaji wa Bodi ya Ithibati ya
Wanahabari, muundo wa Bodi ya Ithibati, majukumu ya Bodi, mamlaka ya Bodi,
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi, majukumu ya Mkurugenzi Mkuu, watumishi wa Bodi,
uthibitishaji wa wanahabari, Kitambulisho cha Wanahabari, Mfuko wa Mafunzo ya
Wanahabari na vyanzo vya fedha za Mfuko.
Sehemu
ya Nne ina masharti yanayohusu uanzishwaji wa Baraza Huru la Habari, uanachama
wa Baraza, majukumu ya Baraza, mwenendo na mikutano ya Baraza, mamlaka ya
Baraza, majukumu ya Katibu wa Baraza na kuondolewa kwa Katibu wa Baraza. Vile
vile, Sehemu hii inaipa Baraza mamlaka ya kushughulikia malalamiko dhidi ya
machapisho. Mtu asiyeridhika na uamuzi wa Baraza anaweza kukata rufaa Mahakama
Kuu.
Sehemu
ya Tano inahusika na masuala ya kashfa Sehemu hii inatoa ufafanuzi endapo jambo
lolote litachapishwa na kutangazwa na mtu na kusababisha kuharibu sifa ya mtu
au kuchafua jina lake; mtu huyo atakuwa ametenda kosa kwa mujibu wa Sheria.
Aidha Sehemu hii imeanisha utangazaji wa mambo yenye kashfa ambayo yanaruhusiwa
ikiwa mambo hayo yatatangazwa na Rais Serikali au Bunge au jambo lolote
litakalotangazwa mahakamani wakati wa kusikilizwa shauri au kutangaza jambo
lolote kwa mujibu wa Sheria.
Sehemu
ya Sita inaainisha masharti yanayohusu masuala ya fedha za Bodi na vyanzo vya
mapato ya Bodi. Aidha, makadirio ya bajeti ya Bodi, utoaji wa taarifa za fedha,
vitabu vya fedha vya Bodi pamoja na ukaguzi wake vimewekewa masharti. Sheria ya
Huduma za Habari.
Sehemu
ya Saba inahusu makosa mbalimbali ambayo yanahusu vyombo vya habari. Sehemu hii
imeainisha makosa dhidi ya utangazaji wa habari ambao umepigwa marufuku, habari
za kuchochea uasi, makosa ya uchochezi, utangazaji wa habari za uongo au za
kutia hofu na woga kwa jamii. Aidha, makosa yanayotendwa na mashirika au kosa
litakalotendwa na mtumishi anayemwakilisha mwajiri yameainishwa na kuwekewa
adhabu.
Sehemu
ya Nane inahusika na masuala ya jumla ambapo inapiga marufuku uingizaji wa
machapisho ambayo hayana manufaa kwa umma. Aidha inampa mamlaka Mkurugenzi wa
Huduma za Habari, afisa polisi au afisa yeyote muidhiniwa kukamata chombo
chochote kinachoendeshwa kinyume na Sheria. Vile vile, Sehemu hii inaainisha
masharti yanayompa mamlaka Waziri kutengeneza kanuni kwa ajili ya uendeshaji
bora wa Sheria hii na uanzishwaji.
MWISHO.
0 comments:
Post a Comment