Fidelis Butahe, Manyoni
MKAZI wa Kata ya Kintinku, Wilaya ya Manyoni, Hadija Ismail (58) amependekeza
Katiba Mpya iwe na kifungu kinachosema misafara yote ya viongozi hususan
Rais iwe na magari yasiyozidi 10 ili kupunguza gharama za
uendeshaji.
Hadija alisema kuwa fedha zinazotumika kugharimia magari zaidi ya 30
yanayokuwa katika msafara mmoja wa Rais, zinaweza kujenga madarasa na kuwalipa
fedha ya ziada walimu wanaoishi vijijini.
Akizungumza wakati akitoa maoni juu ya Katiba Mpya juzi, Hadija alisema
Katiba Mpya inatakiwa kueleza wazi suala hilo, kwa kuwa fedha za walipa kodi
ndiyo zinazotumika kuendeshea magari hayo.
“Rais msafara wake unatakiwa kuwa na magari 10 tu, msafara wa Waziri Mkuu na
Makamu wa Rais unatakiwa kuwa na magari matano matano,” alisema Hadija.
Alisema kuwa ni ajabu kwa viongozi wa Serikali kutumia magari mengi katika
shughuli zao za kila siku wakati kuna baadhi ya vijiji, wananchi wanatumia
jembe la mkono katika shughuli za kilimo.
“Mfano msafara mmoja unakuwa na magari 30, ukipiga hesabu ya gharama ya mafuta
kwa magari 20, labda kutoka Dodoma mpaka Singida, zinatosha kabisa kununulia
trekta la kilimo” alisema Hadija.
Pia Hadija alisema kuwa viongozi wote wanaochaguliwa na wananchi wanatakiwa
kukaa madarakani kwa vipindi viwili tu na siyo kama ilivyo sasa ambapo wapo
wabunge wenye miaka zaidi ya 30 bungeni.
“Diwani na mbunge nao wanatakiwa kuwa na vipindi viwili tu vya kugombea kama
ilivyo kwa Rais” alisema.
Chanzo: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment