Kaimu  meneja wa mamlaka ya chakula na dawa kanda ya kati(TFDA), Aberl Deule  akizungumza na waandishi wa habari (hawapo kwenye picha) juu ya zoezi la  kukagua bidhaa katika maduka ya wilaya ya Manyoni.
Moto  ukiwa umewaka kuteketeza bidhaa zenye thamani ya zaidi ya shilingi  milioni tano ambazo ni sumu na zile ambazo muda wake wa kutumika  umekwisha.Bidhaa hizo zilikamatwa na TFDA katika baadhi ya maduka ya  wilaya ya Manyoni.
Bidhaa ambazo zina sumu na zilizokwisha muda wake zilizokamatwa na TFDA kabla hazijateketezwa kwa moto.
Kaimu  meneja wa TFDA kanda ya kati, Aberl Deule (wa kwanza kulia) akitoa  maelekezo kwa muuza duka wa Manyoni mjini.
                       (Picha na habari, Nathaniel  Limu).
Mamlaka  ya Chakula na Dawa Kanda ya Kati (TFDA) imeteketeza bidhaa mbali mbali  zenye thamnai ya zaidi ya shilingi milioni tano zikiwemo zile ambazo  muda wake wa kutumika umeisha.
Bidhaa  hizo ni pamoja na soda, juice, biskuti (muda wake wa kutumika  uliishapita) na maziwa ya unga ya watoto wadogo aina ya Lactogen (18 na  2) ambayo ni bandia.
Bidhaa  zingie zilizoteketezwa ni tani moja ya vipodozi hatari kwa matumizi ya  binadamu yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni tatu.
Vipodozi hivyo vyenye kemikali za hydroquinone na zebaki, hutumiwa kubadilisha rangi ya ngozi (kujichubua).
Akizungumza  muda mfupi baada ya kuteketeza bidhaa hizo, Kaimu Meneja TFDA Kanda ya  Kati Aberl Deule, amesema msako wa ukaguzi wa kuangalia ubora na usalama  wa chakula, dawa na vipodozi, ulianza Novemba 13 hadi 17 wilayani  Manyoni.
Amesema  msako huo ambao ni endelevu, ulifanyika katika maeneo 52 ya Manyoni  mjini na Itigi, ambayo ni pamoja na viwanda vya kutengeneza vyakula,  kuuzia vyakula, maduka ya vipodozi, maduka ya dawa za binadamu na yale  ya dawa za mifugo.
Katika  hatua nyingine, Kaimu Meneja huyo amewataka wananchi kuhakikisha  wanatumia bidhaa ambao hazijaisha muda wake na zile ambazo  hazina sumu.
Kwa  upande wa wafanyabiashara, Deule amewataka muda wote wahakikishe  wanampatia mteja bidhaa zenye ubora, zisizokuwa na sumu na zile ambazo  muda wake wa kutumika, haujaisha.
Amesema  “Wafanyabiashara mnaojishughulisha na biashara za chakula, dawa,  vipodozi na vifaa tiba, hakikisheni majengo yenu yanasajiliwa na TFDA. Hakikisheni pia  bidhaa, mnazozalisha au kuuza ni salama kwa afya ya  binadamu na bora”.
Deule  amewataka wajenge utamaduni wa  kukagua bidhaa zao ili kubaini kama  kuna bidhaa zilizopitwa muda wa matumizi na wajiepushe kuuza vipodozi  vyenye viambato vya sumu.
Imedaiwa  kuwa mfanyabiashara aliyefahamika kwa jina moja la Anord wa Manyoni  mjini,  amelazwa katika hospitali  ya wilaya, muda mfupi baada ya  shehena ya biadhaa zisizokuwa salama kwa matumizi ya binadamu, kukamatwa  dukani kwake.
0 comments:
Post a Comment