Makuli
kumi wakipakia juu ya lori gunia moja la viazi vitamu lenye zaidi ya
kilo 150 lenye thamani ya shilingi 35,000.Wakulima wa zao la viazi
vitamu tarafa ya Ihanja wilaya ya Ikungi mkoa wa Singida,wamelalamikia
ujazo huo pamoja na bei wanayopewa kwa madai kuwa ni ya kinyonyaji.
Magunia
ya zao la viazi vitamu katika kijiji cha Ighuka wilaya ya Ikungi,vikiwa
tayari kusafirishwa ndani na nje ya nchi kwa ajili ya kwenda kuuzwa.
Lori
ambalo dereva wake aliomba lisitajwe namba zake za usajili likiwa
linapakia magunia ya viazi vitamu katika kijiji cha Ighuka wilaya ya
Ikungi.(Picha na Nathaniel Limu).
Na Nathaniel Limu.
Wakulima
wa zao la viazi vitamu tarafa ya Ihanja wilaya ya Ikungi mkoani Singida
wamelalamikia tabia ya wafanyabiashara ya kuwalazimisha kuuza gunia
lenye uzito wa kilo zaidi ya 150 kwa bei ndogo ya shilingi 35,000.
Wamedai kwamba ujazo huo wa gunia la viazi vitamu unaojulikana kwa jina la ‘polo’, unachangia wakulima kunyonywa mapato yao.
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti na MO Blog, wakulima hao wamedai kuwa gharama
wanazotumia katika kulima na ile ya kusafirisha hadi barabarani zao la
viazi vitamu, haiwezi kurudi kwa bei wanayopewa na wafanyabiashara hao.
Mmoja
wa wakulima hao Doricus Hussein, amesema wafanyabiashara hao wanaotoka
katika mikoa ya Dodoma, Tanga, Dar-es-salaam, Zanzibar pamoja na visiwa
vya Comoro, wamekuwa hawako tayari kununua zao hilo kwa kutumia vipimo
kwa madai kuwa hakuna soko litakalonunua viazi vitamu kwa kutumia
mizani.
Alitumia
fursa hiyo kuiomba serikali ya kijiji kwa ushirikiano na halmashauri ya
wilaya ya Ikungi,kuangalia uwezekano wa kuwasaidia wakulima wasiendelee
kunyanyaswa na kudhulumiwa na wafanyabiashara hao.
Kwa
upande wake Kaimu Afisa Mtendaji wa kata ya Pum Miraji Ntungu, amesema
kuwa licha ya kupiga marufuku ujazo wa rumbesa unaolalamikiwa na
wakulima hao, lakini ni wakulima wenyewe ndio wanaopingana na agizo hilo
kwa madai kuwa serikali haijawasaidia kutafuta mbegu ya viazi vitamu.
Ntungu
amesema kwa siku moja magunia yasiyopungua 200 husafirishwa kutoka
kijiji cha Puma pekee kwenda kwenye masoko ya ndani na nje ya nchi,
ambapo kila gunia hulipiwa ushuru wa shilingi elfu moja.
Kwa
upande wao wafanyabiashara hao wanaolalamikiwa, wamedai kuwa hakuna
soko linaloweza kununua gunia la viazi vitamu lisilo kuwa na ujazo wa
rumbesa iliyopitiliza.
Mmoja
wa wafanyabiashara hao Bw. Shabani Hamisi Bilali, amesema pia
wanawataka wakulima hao kujaza gunia ujazo huo wa rumbesa ili pamoja na
mambo mengine, wao waweze kufidia gharama za upakiaji na usafirishaji
na hivyo kupata faida inayokidhi mahitaji.
Na Mo Blog