MWENYEKITI WA KIJIJI CHA PUMA WILAYA YA IKUNGI SINGIDA ANUSUSRIKA KUPIGWA,ASINDIKIZWA NA POLISI

 
 Wananchi wa kijiji cha Puma katika wilaya ya ikungi mkoani Singida wame mkataa mwenyekiti  wa kijiji hicho katika mkutano wake wa kwanza na kusababisha diwani wa kata hiyo  kwa kushirikiana na jeshi la polisi kuingilia kati na kufunga mkutano kabla ya wakati ili kumnusuru asipigwe na wananchi.
Wananchi hao waliokuwa na hasira wamesema hakuna sababu ya kuwa na mwenyekiti ambaye wananchi hawamkubali kwa sababu katika uchaguzi uliopita kulikuwa na udanganyifu katika upigaji kura,kutokana na hali hiyo wamesema ni bora kuachana na vyama vya siasa wachague mwenye kiti wa kimila ili kukisaidia kijiji cha puma kupata maendeleo.
Baada ya vurugu  kuongezeka diwani wa kata hiyo kwa tiketi ya CCM,Bwana ramadhani kulungu ilibidi kufunga kikao hicho ili kuweza kumnusuru mwenyekiti wa kijiji cha puma na kuwatuliza wananchi ilikusitokee uvunjifu wa amani.
Mwenyekiti wa kijiji cha puma  kwa tiketi ya CCM ,Bwana Sifa Joramu awali ambaye alishindwa kabisa kuendesha kikao chake ,baada ya jeshi la polisi kuingilia kati na kuamua kumsindikiza kwa ulinzi mkali huku wananchi waki mzomea na kusema hawamtaki,amesema hizo ni fujo za vyama vya upinzani lakini yeye  atahakikisha kazi anafanya kwa sababu yeye ndiye aliyeshinda na kuapishwa kwa kazi ya uwenyekiti wa kijiji cha puma. 
Kundi la watu waliamua kumfuata na kumbeba  juu kisha kumzungusha mitaani Bwana Hassan Chaimbo aliye gombea kwa tiketi ya CHADEMA na kushindwa kwa kupata kura mianne arobaini na nne dhidi ya  Bwana Sifa  Joramu alishinda uwenyekiti wa kijiji cha puma kwa tiketi ya CCM katika uchaguzi uliofanyika mwishoni  mwaka jana na kupata kura mianne hamsini na saba.
 Chanzo:ITV Tanzania
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
KUELEKEA UCHAGUZI 2015: JE UNAPENDA NANI AWE KIONGOZI WAKO? JAZA FOMU HII FUPI HAPA

TRA YAAGIZWA KUHARAKISHA UKAGUZI WA SUKARI NCHINI

 
Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe
 
Kamati ya kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), imeiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kuharakisha agizo la ukaguzi wa sekta ndogo ya sukari ili kupata ufumbuzi wa haraka.
 
Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe, akitoa maamuzi mara baada ya kuhojiana na TRA, alisema uingizwaji holela wa sukari una hatari kwa ukuaji wa viwanda vya ndani.
 
“Tunataka taarifa ili tuweze kuwa na mikakati endelevu ya kuzuia sukari ya magendo, unasababaisha sukari inayozalishwa na viwanda vyetu na miwa ya wakulima ina kosa soko,” alibainisha.
 
Hivi karibuni, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Janeth Mbene, alipotembelea kiwanda cha sukari cha TPC mkoani Kilimanjaro, alielezwa jinsi sukari ya nje iliyojaa sokoni na wao kukosa pa kuiuza.
 
Alisema watakutana na Wizara zinazohusika kujadili na kuanza operesheni maalum kwenye maduka mbalimbali na kukamatwa sukari ya nje na ya viwandani inayouzwa kwa wananchi kwa bei ndogo.
 
CHANZO: NIPASHE
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

TAMISEMI YAZUNGUMZIA VURUGU UCHAGUZI WA MITAA

Mkurugenzi wa Uchaguzi katika Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Khalist Luanda.
Imeelezwa kuwa uwazi katika uchaguzi wa Serikali za mitaa, ndiyo kiini cha vurugu zinazotokea wakati wa kuapisha viongozi waliochaguliwa kwenye maeneo mbalimbali nchini.

Kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa Uchaguzi katika Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Khalist Luanda, wakati akizungumza na NIPASHE kuhusu vurugu zilizojitokeza wakati wa uchaguzi wa serikali za mitaa Desemba, mwaka jana.

“Mfumo wa sasa katika chaguzi unawezesha mtu kujumlisha kura za kila kituo na kufahamu nani ameshinda, kwahiyo ni vigumu kufanya hujuma,”
alieleza Luanda.

Luanda aliagiza maofisa watendaji wote wanaobainika kuwa wazembe au wenye udhaifu wa aina yoyote, inayosababisha vurugu kiasi cha kuahirisha au kusimamisha shughuli za kuapisha viongozi hao, achukuliwe hatua kama mhalifu yeyote wa jinai, kama kanuni za uchaguzi zinavyoelekeza.

Alisema hali hiyo inatakiwa kuwa fundisho kwa wote watakaohusika kwenye zoezi la kupiga kura ya maoni, kuidhinisha au kubatilisha.

Katiba inayopendekezwa na kwenye uchaguzi mkuu wa viongozi, unaotarajiwa kufanyika Oktoba, mwaka huu.

Hata hivyo, Luanda alifananisha wanaofanya vurugu hizo na ‘Panya Road’ (mtandao wa wahuni), akisema Tanzania hakuna mfumo wa kisheria unaoelekeza mtu akidhulumiwa haki yake kufanya fujo.

Alihusisha wanaofanya vurugu hizo na waliokuwa wakifanya vurugu kwenye vituo vya uchaguzi, kwamba baada ya kushindwa wameweka mikakati ya kuvuruga shughuli za kuwaapisha waliowashinda.

Alipoulizwa matukio ambayo wananchi walibana maafisa watendaji wakidaiwa kuchakachua matokeo na kutangaza waliokuwa wagombea wa CCM kuwa washindi badala ya washindi halisi, alisema hakuna kitu kama hicho.

Luanda aliombwa kuzungumzia tukio la Kijiji cha Nduoni, Kirua Vunjo Magharibi,  Kilimanjaro ambako mgombea wa NCCR-Mageuzi alishinda lakini Afisa Mtendaji akatangaza kuwa mshindi ni mgombea wa CCM.

Baada ya wananchi kumbana, mtendaji huyo alibatilisha tangazo hilo na kurejesha ushindi kwa mgombea wa NCCR-Mageuzi baada ya wananchi
kumbana, akatangaza matokeo yaliyompa ushindi mgombea wa NCCR-Mageuzi.

Alisema hakuwa na taarifa ya tukio hilo na kama hivyo ndivyo, basi matatizo mengine yanatokana na udhaifu wa watendaji husika na kwamba hapo kinachohitajika ni wahusika kushughulikiwa kwa mujibu wa kanuni.

“Mtendaji anapokuwa na udhaifu binafsi, siyo sawa kuhusisha kasoro anazosababisha na serikali au chama chochote bali Msimamizi wa Uchaguzi, ambaye ni Mkurugenzi wa eneo husika anatakiwa kutumia kanuni za uchaguzi kumshughulikia,” alieleza Luanda.

Katika tukio la Vunjo, wananchi walijikusanya wakiwa na mabango yaliyoeleza masikitiko yao juu ya kuapishwa Joseph Msaki (CCM) aliyepata kura 158 kama Mwenyekiti wa kijiji ilhali Thomas Ngowi (NCCR-Mageuzi) aliyepata kura 163 akiachwa bila kuapishwa.

Wananchi hao walifikia uamuzi wa kufunga ofisi za Serikali ya Kijiji hicho, wakikataa kuongozwa na mwenyekiti asiye chaguo lao hali
iliyosababisha Afisa Mtendaji wa Kirua Vunjo Magharibi, Reginald Mlay,kumtangaza Thomas kuwa ndiye mwenyekiti halali.
CHANZO: NIPASHE
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

ANANITUKANA KISA NIMEMKATAA KIMAPENZI

 Shikamoo shangazi mkubwa. Mimi ni msichana mwenye miaka 26. Kuna kijana mmoja hapa mtaani kwetu alikuwa akinifuatilia kwa muda mrefu sana. Anataka niwe naye kimapenzi. Baada ya kuchekecha niliona siyo wa aina yangu hivyo nikamtosa. Kitendo cha kumkataa imekuwa shida sasa. Mana kila ninapokutana naye ananitukana. Nifanyeje?
Ramla,
Dar es Salaam.
Muonye kuhusiana na tabia yake hiyo. Kama bado anaendelea nenda katoe taarifa polisi maana ni makosa kisheria kumtukana mtu.
Nampenda lakini naogopa kumwambia
Pole na majukumu shangazi mkubwa. Nimetokea kumpenda msichana mmoja. Kila ninapomuona nahisi anafaa kuwa mama wa watoto wangu. Tatizo ni kwamba naogopa kumwambia kwani nahisi kuwa hatanikubali. Nifanyeje shangazi?
Juma,
Dar es Salaam.
Usihofu kukataliwa unapotaka kuomba kaka, maana yote ni majibu sahihi. La msingi ni kumwambia ili kujua msimamo wake.
Anataka tuzae kwanza ndipo anioe
Shangazi mimi ni msichana mwenye umri wa miaka 26. Nimemaliza chuo na nimebahatika kupata kazi kwenye kampuni moja hapa mjini. Tatizo ni kwamba, kuna mvulana nimempata ninahisi ananipenda sana. Lakini kila tunapoongea suala la ndoa anadai kuwa ni vyema nizae kwanza ndipo anioe. Ni sahihi shangazi?
Jane,
Mbeya.
Wala si sahihi Jane. Hiyo si mboga kusema hawezi kula hadi aonje kwanza. Kuwa na msimamo, wambie hakuna kuzaa hadi ipite ndoa kwanza.
Nyumba ndogo yangu inataka ndoa
Shangazi mimi ni mwanaume mwenye mke na watoto wawili. Tatizo langu ni kwamba nimekuwa na mwanamke nje ya ndoa yangu kwa miaka sita sasa. Mwanamke huyo amekuwa akinishawishi nimuoe. Lakini kimsingi dini yangu hairuhusu. Nifanyeje?
Japhet,
Dar es Salaam.
Wala sina ushauri juu ya hilo. Mana kwa kuwa unafahamu kama dini yako hairuhusu sasa unanitaka la rohoni au?
Mke wangu amenitelekeza na watoto
Pole na majukumu shangazi mkubwa. Mimi ni baba wa watoto watatu. Nimekuwa kwenye ndoa kwa muda wa miaka kumi sasa. Hivi karibuni mke wangu alinikimbia, mbaya zaidi amebeba hadi nguo zake na vitu vyake muhimu nifanyeje?
Baba George,
Dar es Salaam.
Kwanza katoe taarifa katika kituo cha polisi. Pili wafahamishe ndugu zake. Ukimaliza hakikisha watoto wako wanakuwa katika mikono salama. Hilo likiwa sawa endelea na maisha yako maana inaonekana alidhamiria na anajua anachokifanya. Kitendo cha kumfuatilia kitakupotezea muda.
Nasumbuliwa na wapenzi wangu wa zamani
Hujambo shangazi mkubwa? Mimi ni mwanaume mwenye umri wa miaka 30. Baada ya kuzunguka katika mambo yetu yale kwa muda mrefu, nimepata yule anayenifaa na nimeshafunga naye ndoa. Tatizo ni kwamba, wale wapenzi niliokuwa nao zamani wamekuwa wakinisumbua kwa meseji kwenye simu na wakati mwingine wanadiriki hata kumtukana mke wangu. Nifanyeje ili waachane na maisha yangu. Kimsingi naona wanaweza kuniharibia.
James,
Tanga.
Kwanza tafuta muda uongee na mkeo. Hakikisha humfichi kitu juu ya maisha yako yaliyopita. Akishakuelewa utakuwa ushaweka uzio. Hakuna atakayeweza kubomoa ndoa yenu. Ukimaliza waweke wazi kuwa hakuna kitakachoendelea baina yenu kwani tayari wewe ni mume wa mtu. Hapo heshima itachukua mkondo wake.
Rafiki yake anadai ni kahaba
Shangazi rafiki wa mpenzi wangu amenitumia ujumbe akidai kuwa mpenzi wangu huyo ni kahaba. Inawezekana kuna ukweli au hapendi tu mimi kuwa naye. Nishauri shangazi
Alphonce
Dar
Usikurupuke katika maamuzi. Jitahidi kulifanyia kazi, nina hakika jibu lake halipo mbali.
 Chanzo:Mwananchi
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

Chadema Singida wapanga kumburuza mahakamani msimamizi wa uchaguzi.


Mjumbe wa kamati ya utendaji CHADEMA manispaa ya Singida, Vicent Mughwai (katikati) akitoa taarifa kwa waandishi wa habari juu ya kusudio la chama hicho kumfungulia shitaka msimamizi wa uchaguzi wa serikali za mitaa manispaa ya Singida, kwa tuhuma ya kukiuka kanuni za uchaguzi huo. Vicent ndugu yake na mbunge wa jimbo la Singida mashariki na mnadhimu mkuu wa sheria CHADEMA, Tundu Lissu, ametangaza rasmi kumng’oa mbunge wa CCM jimbo la Singida mjini Mohammed Gullam Dewji, kwenye uchaguzi mkuu ujao. Kulia mjumbe wa kamati ya wilaya na katibu kata CHADEMA kata ya Unyambwa na kushoto ni mwenyekiti wa baraza la wazee wilaya CHADEMA Singida mjini.
Baadhi ya viongozi wa ngazi mbalimbali CHADEMA manispaa ya Singida, wakiwa kwenye mkutano wa chama hicho na waandishi wa habari ambapo CHADEMA walitoa taarifa kwa vyombo vya habari juu ya uchaguzi wa serikali za mitaa,vijiji na vitongozi uliomalizika Desemba 14 mwaka huu.
Baadhi ya waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali waliohudhuria kikao kilichoitishwa na CHADEMA manispaa ya Singida kutangaza nia ya kumfikisha mahakamani msimamizi wa uchaguzi huo manispaa ya Singida, kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo ya vitendo vya rushwa kwa ajili ya kukidhoofisha CHADEMA.
CHAMA  Cha Maendeleo na Demokrasia (CHEDEMA) halmashauri ya manispaa ya Singida, kinatarajia kumburuza mahakamani msimamizi wa uchaguzi wa serikali kutokana na tuhuma mbalimbali, ikiwemo ya uchakachuaji wa kura.
Hayo yamesemwa na mjumbe wa kamati ya utendaji CHEDEMA manispaa ya Singida,Vicent Mughwai,wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari iliyohusu uchaguzi wa serikali za mitaa uliomalizika Desemba 14 mwaka huu.
Alisema zoezi la uchaguzi wa serikali za mitaa manispaa ya Singida, kwa kiasi kikubwa haukufanyika kwa haki. Vitendo vya rushwa na ukiukwaji kuanzia uandikishwaji wa wapiga kura na ukiukwaji mkubwa wa kanuni za uchaguzi na wa kupata wagombea nafasi za uongozi na mchakato wa kupata viongozi na chaguzi mkuu.

Vicent alitaja baadhi ya vitendo vya ukiukwaji wa kanuni kuwa ni wasimamizi wa CHADEMA kuenguliwa kwenye nafasi ambazo walitaka kuja kuwatumikia wananchi kikamilifu, kwa lengo la  wagombea wa  CCM waweze kupita bila vikwazo vyovyote.
Mjumbe huyo alitaja vitendo vingine kuwa kada wa CCM kutumia gari kusomba watu na kuwapeleka kwenye vituo vya kupigia kura na wagombea wa CHADEMA kuzuiwa kuingia kwenye vyumba vya kuhesabia kura ili uchakachuaji uweze kufanyika kitendo ambacho ni kinyume na kanuni namba 22.
“Kutokana na ukiukwaji mkubwa wa kanuni za uchaguzi katika jimbo letu,tunaomba vyombo husika na serikali,vifanye uchunguzi wa kina na hatua kali zichukuliwe dhidi ya wote watakaobainika wana hatia”alisema.
Aidha, mjumbe huyo alisema CHADEMA inamwomba  Waziri wa TAMISEMI, amchukulie hatua kali msimamizi wa uchaguzi wa serikali za mitaa ambaye ni mkurugenzi wa manispaa ya Singida,kwa kushindwa kutekeleza majukumu yake kusimamia ipasavyo uchaguzi huo.

“Tunawasiliana na wanasheria wa chama chetu ili tuweze kuchukua hatua za kisheria kupinga matokeo yote  yaliyopatikana kutokana na ukiukwaji mkubwa wa kanuni.Lengo ni wapiga kura wetu waweze kutendewa haki”,alifafanua.
Kwa upande wa msimamizi wa uchaguzi serikali za mitaa manispaa ya Singida, Joseph Mchina, alisema CHADEMA  wanao haki ya kwenda mahakamani, ili waweze kupatiwa haki yao kama wanaamini kulikuwepo na ukiukwaji wa kanuni na vitendo vya rushwa katika uchaguzi huo.

“Mahali ambapo wagombea wa CHADEMA hawakuruhusiwa kuingia kwenye vyumba vya kuhesabia kura, nafasi ilikuwa finyu lakini mawakala wao waliruhusiwa.Viongozi wa CHADEMA ambao walikuwa sio wagombea wala wasimamizi, kanuni hazitoi nafasi kwao kuingia kwenye vyumba vya kuhesabia kura,l akini wao walilazimisha waingie kitendo ambacho hakikubaliki”,alisema Mchina.
 
Singida yetu Blog
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2011. Singida Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogz za Mikoa