Shikamoo shangazi mkubwa. Mimi ni msichana mwenye miaka 26. Kuna
 kijana mmoja hapa mtaani kwetu alikuwa akinifuatilia kwa muda mrefu 
sana. Anataka niwe naye kimapenzi. Baada ya kuchekecha niliona siyo wa 
aina yangu hivyo nikamtosa. Kitendo cha kumkataa imekuwa shida sasa. 
Mana kila ninapokutana naye ananitukana. Nifanyeje?
Ramla,
Dar es Salaam.
Muonye kuhusiana na tabia yake hiyo. Kama bado anaendelea nenda katoe taarifa polisi maana ni makosa kisheria kumtukana mtu.
Nampenda lakini naogopa kumwambia
Pole na majukumu shangazi mkubwa. Nimetokea 
kumpenda msichana mmoja. Kila ninapomuona nahisi anafaa kuwa mama wa 
watoto wangu. Tatizo ni kwamba naogopa kumwambia kwani nahisi kuwa 
hatanikubali. Nifanyeje shangazi?
Juma,
Dar es Salaam.
Usihofu kukataliwa unapotaka kuomba kaka, maana yote ni majibu sahihi. La msingi ni kumwambia ili kujua msimamo wake.
Anataka tuzae kwanza ndipo anioe
Shangazi mimi ni msichana mwenye umri wa miaka 26.
 Nimemaliza chuo na nimebahatika kupata kazi kwenye kampuni moja hapa 
mjini. Tatizo ni kwamba, kuna mvulana nimempata ninahisi ananipenda 
sana. Lakini kila tunapoongea suala la ndoa anadai kuwa ni vyema nizae 
kwanza ndipo anioe. Ni sahihi shangazi?
Jane,
Mbeya.
Wala si sahihi Jane. Hiyo si mboga kusema hawezi 
kula hadi aonje kwanza. Kuwa na msimamo, wambie hakuna kuzaa hadi ipite 
ndoa kwanza.
Nyumba ndogo yangu inataka ndoa
Shangazi mimi ni mwanaume mwenye mke na watoto 
wawili. Tatizo langu ni kwamba nimekuwa na mwanamke nje ya ndoa yangu 
kwa miaka sita sasa. Mwanamke huyo amekuwa akinishawishi nimuoe. Lakini 
kimsingi dini yangu hairuhusu. Nifanyeje?
Japhet,
Dar es Salaam.
Wala sina ushauri juu ya hilo. Mana kwa kuwa unafahamu kama dini yako hairuhusu sasa unanitaka la rohoni au?
Mke wangu amenitelekeza na watoto
Pole na majukumu shangazi mkubwa. Mimi ni baba wa 
watoto watatu. Nimekuwa kwenye ndoa kwa muda wa miaka kumi sasa. Hivi 
karibuni mke wangu alinikimbia, mbaya zaidi amebeba hadi nguo zake na 
vitu vyake muhimu nifanyeje?
Baba George,
Dar es Salaam.
Kwanza katoe taarifa katika kituo cha polisi. Pili
 wafahamishe ndugu zake. Ukimaliza hakikisha watoto wako wanakuwa katika
 mikono salama. Hilo likiwa sawa endelea na maisha yako maana inaonekana
 alidhamiria na anajua anachokifanya. Kitendo cha kumfuatilia 
kitakupotezea muda.
Nasumbuliwa na wapenzi wangu wa zamani
Hujambo shangazi mkubwa? Mimi ni mwanaume mwenye 
umri wa miaka 30. Baada ya kuzunguka katika mambo yetu yale kwa muda 
mrefu, nimepata yule anayenifaa na nimeshafunga naye ndoa. Tatizo ni 
kwamba, wale wapenzi niliokuwa nao zamani wamekuwa wakinisumbua kwa 
meseji kwenye simu na wakati mwingine wanadiriki hata kumtukana mke 
wangu. Nifanyeje ili waachane na maisha yangu. Kimsingi naona wanaweza 
kuniharibia.
James,
Tanga.
Kwanza tafuta muda uongee na mkeo. Hakikisha 
humfichi kitu juu ya maisha yako yaliyopita. Akishakuelewa utakuwa 
ushaweka uzio. Hakuna atakayeweza kubomoa ndoa yenu. Ukimaliza waweke 
wazi kuwa hakuna kitakachoendelea baina yenu kwani tayari wewe ni mume 
wa mtu. Hapo heshima itachukua mkondo wake.
Rafiki yake anadai ni kahaba
Shangazi rafiki wa mpenzi wangu amenitumia ujumbe 
akidai kuwa mpenzi wangu huyo ni kahaba. Inawezekana kuna ukweli au 
hapendi tu mimi kuwa naye. Nishauri shangazi
Alphonce
Dar
Usikurupuke katika maamuzi. Jitahidi kulifanyia kazi, nina hakika jibu lake halipo mbali.
 Chanzo:Mwananchi
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
0 comments:
Post a Comment