AFYA YA UZAZI: NAMNA YA KUCHUNGUZA HATUA ZA KUJIFUNGUA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 
Moja ya malengo ya milenia ni kupunguza kama si kuondoa kabisa vifo vya kinamama na watoto vitokanavyo na ujauzito, wakati wa kujifungua na wakati wa kulea.
Hili litawezekana tu iwapo kutakuwepo na huduma bora zitakazohakikisha uwepo wa uzazi salama.
Zipo sababu nyingi zinazochangia vifo vya uzazi lakini vingi vinasababishwa na uzingatiaji dhaifu wa muongozo wa uzazi salama.
Mwongozo uliotayarishwa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jami unaaminika kuwa ni bora kuliko ile iliyoandaliwa katika nchi nyingine za Afrika Mashariki na Kati.
Hii inamaana kwamba mwingozo huo  ukizimamiwa vizuri na wadau wote basi tatizo hili litakwisha.
Si kila wakati vifo hivi vinatokea kutokana na sababu za miundo mbinu kwani baadhi yake hutokea hata sehemu ambazo miundo mbinu si mibaya kiasi cha kusababisha ucheleweshaji wa kufanya uamuzi sahihi. 
Kadi ya kliniki ya wajawazito imetayarishwa maalumu kuelezea hatua kwa hatua namna ya kumhudumia mama mjamzito.
Huduma hizo ni tangu anapopata ujauzito, kutunza ujauzito, kujifungua na hata kwa kipindi fulani kilichopendekezwa baada ya kujifungua.
Kadi  hii kama itatumika vizuri ni rahisi kugundua viashiria vyote vya hatari na hatimaye kuchukua hatua kwa muda muafaka.
Kadi hii imegawanywa katika sehemu kuu tano na zote ni muhimu.
Sehemu yenye jedwali la hatua za uchungu ndio mahususi kwa dalili na hatua za kujifungua.
Baada ya njia kufunguka hatua inayofuata ni kutoka kwa mtoto kwa kanuni maalumu.
Lakini kufunguka kwa njia mpaka kiwango cha mwisho  si kila wakati inamaanisha mtoto atatoka.
Hii ni ishara hatarishi na kama hatua za jedwali zimesimamiwa vizuri litaonyesha hivyo ili hatua stahiki zichukuliwe.
Huu ni mfano mmoja tu. Uchambuzi wa kina kuhusu kadi ya kliniki ya wajawazito umefanywa katika makala zilizotangulia katika gazeti hili.
Iwapo mototo atatoka salama hatua inayofuata ni  kutoka kwa kondo la nyuma.
Ni wajibu wa mtoa huduma kuhakikisha kuwa kondo hilo limetoka katika muda muafaka na pia kulikagua kama limekamilika.
Chanzo;Mwananchi 

RC ASISITIZA WANANCHI KUSOMEWA MAPATO NA MATUMIZI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

SERIKALI za vijiji mkoani Singida zimetakiwa kuwasomea wananchi wake kwa mujibu wa taratibu taarifa za mapato na matumizi ya makusanyo mbalimbali wanayofanya ili kuondoa malalamiko yoyote yasiyo ya lazima.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk Parseko Kone alitoa agizo hilo katika Kata ya Kindai wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa vyumba vya maabara kwenye shule mbalimbali za sekondari zilizopo Manispaa hiyo.
Mkuu huyo wa Mkoa alilazimika kutahadharisha hilo baada ya baadhi ya wananchi kulalamika mbele ya yake kuwa uongozi wa kata hiyo hauna utamaduni wa kuwasomea taarifa za mapato na matumizi kwa mujibu wa taratibu na kuna ubadhirifu mkubwa.
Chanzo;Habari Leo

SIKIKA YAWAGAWA MADIWANI KONDOA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 
BAADHI ya madiwani katika Halmashauri ya Wilaya Kondoa, wamejitokeza kupinga uamuzi uliofikiwa na Baraza la Madiwani wa kulifukuza Shirika la Sikika wilayani humo.
Wakizungumza na gazeti hili hivi karibuni, madiwani hao walisema uamuzi huo hauna afya kwa maendeleo ya wilaya hiyo, kwani shirika hilo lilikuwa likisaidia kuonyesha udhaifu uliopo katika idara ya afya.
Kwa mujibu wa madiwani hao, uamuzi wa shirika hilo kufukuzwa ulianza kutengenezewa mazingira kwa madiwani wa CCM kufungwa na msimamo wa kichama juu ya shirika hilo.
Diwani wa Kata ya Kondoa Mjini, Hamza Mafita (CCM), alisema Sikika ni jicho la pili ambalo kama lingetumiwa vizuri lingeweza kuwasaidia madiwani kuona uchafu mahala ambapo wameshindwa kuufikia.
“Kuhusu Sikika mimi nilijua shirika hili litafukuzwa tu kwa sababu ya viongozi wetu kupenda kulinda ufisadi. Katika bajeti ya mwaka 2012/2013 miradi ya afya shughuli namba 12 ilitengewa bajeti ya sh milioni 17 kwa ajili ya kukarabati vizimba vya kuchomea takataka.
“Ilikuwa ni kwa ajili ya vituo vya afya vya Hamai na Mrijo. Kizimba cha Hamai kilijengwa chini ya kiwango thamani yake hata milioni mbili hakifiki, Mrijo kule hicho kizimba chenyewe hakipo,” alisema.
Diwani wa Viti Maalumu, Hija Suru (CCM), alisema uamuzi wa shirika hilo kufukuzwa ulikuwa na msukumo ndani yake wenye sura inayotiliwa shaka dhidi ya madiwani.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Suruke, Jafari Ganga (CUF) alisema uamuzi huo ulifanywa na madiwani wa CCM lakini madiwani wa upinzani walipiga kura ya kukataa shirika hilo kufukuzwa.
“Kikao cha Julai 26 kilihudhuriwa na madiwani 36 madiwani 26 wa CCM walishikizwa kupiga kura ya kuiondoa Sikika madiwani 10 wa upinzani tulikataa,” alisema.
Wakijibu madai hayo, Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Hisdory Mwalongo na Mwenyekiti wa halmashauri, Khamis Mwenda walitetea msimamo wao na kusema kuwa hatua zilizochuliwa dhidi ya shirika hilo ni sahihi.
Chanzo;Tanzania Daima 

MGIMWA AONYA MAAFISA MISITU

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Mahmood Mgimwa amewatahadharisha baadhi ya wafanyakazi waliopewa dhamana ya kusimamia rasilimali za misitu kutokuwa kichocheo cha uharibifu wa misitu kutokana na kutowajibika ipasavyo pamoja na kufanyakazi kinyume cha maadili.
Mgimwa alitoa tahadhari hiyo wakati wa ufunguzi wa mkutano mkuu wa mwaka wa siku tatu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), uliofanyika mjini Singida.
“Katika mikakati hii hatutegemei kuona wafanyakazi waliopewa dhamana ya kusimamia rasilimali hizi, wanakuwa kichocheo cha uharibifu wa misitu yaani kunakotokana na kutowajibika ipasavyo na kufanyakazi kinyume cha maadili,”alisisitiza.
Alifafanua kuwa ni jukumu la wataalamu wote kutekeleza mipango kazi inayoanishwa katika mikakati yao ya kuongoza na kuendeleza rasilimali za misitu na nyuki.
Kwa mujibu wa Naibu waziri huyo, TFS kwa niaba ya serikali ya Tanzania anatakiwa ajipambanue kwa kufanya kila linalowezekana katika kulinda rasilimali za misitu zilizopo na kuziendeleza kwa kuongeza maeneo zaidi ya misitu.
Naye Mtendaji Mkuu wa TFS, Juma Mugoo alisema katika kipindi cha kuanzia mwaka wa fedha wa 2010/2011 hadi 2013/2014, wameweza kutengeneza na kusambaza mizinga ya nyuki ipatayo 19,570 katika vituo vya wakala mizinga 5,729 na vijiji vilivyoko kando ya misitu ya Hifadhi mizinga 13,841.
Hata hivyo, Mugoo aliweka bayana kwamba vituo vya ufugaji nyuki vya Nyandakame Kondoa, Ukimbu Manyoni, Buha Kibondo na Mwambao wa Handeni vimewezeshwa kuwa vituo vya uzalishaji badala ya ilivyokuwa mwanzo kama vituo vya maonesho.
“Kiasi cha tani zaidi ya 7.6 za asali na kilo 458.5 za nta zilizalishwa na kuuzwa,vile vile wakala imeanzisha manzuki mpya 51 katika kanda za Kusini, Kaskazini, Mashariki, Kati na katika mashamba saba ya miti,”alisema.
Raisi wa Chama cha Wataalamu wa Misitu Tanzania (TAF), Prof. Reuben Mwamakimbullah alisema kwa kiasi kikubwa hali ya misitu nchini inasikitisha licha ya kuwepo wataalamu wanaolipwa kwa ajili ya kusimamia sekta hiyo. 
Chanzo;Tanzania Daima 

TUSIKUBALI KAMWE KUGEUZWA KARAI LA ZEGE 2015

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

 
Hakuna ubishi waandishi wa habari wana nafasi kubwa sana ya kuipatia jamii viongozi bora na sio bora viongozi, kama wataweka mbele uzalendo na kuacha kuchukua hongo kutoka kwa wagombea kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Nafahamu wapo waandishi wengi wenye uadilifu, lakini kwa sababu kwenye msafara wa mamba na kenge wamo, si ajabu kukuta ambao njaa yao ya muda mfupi inatupatia viongozi wabovu.
Kipindi cha uchaguzi ni wakati ambapo baadhi yetu tunajulikana thamani zetu. Wapo wa Sh20,000, wengine Sh50,000, pia wa Sh100,000 na wale wanaopewa hongo zaidi ya kiasi hicho.
Hongo hizi wanazopokea ili kumpamba mgombea kuliko uhalisia wake, zimekuwa na athari kubwa kiuchumi, kisiasa na kijamii ikiwamo kupata viongozi wasiofaa na wanaotanguliza masilahi yao binafsi mbele.
Sote tunafahamu Uchaguzi Mkuu wa 2005 na 2010 namna ambavyo tuliwapamba baadhi ya wagombea wakiwamo wa ubunge, tukawaaminisha wapigakura wakawachagua, lakini leo wanajuta. Natamani utaratibu ule wa zamani urejee, kwamba kama wananchi walikuwa na hitaji la kiongozi walimtafuta wenyewe na kumuomba ili agombee, leo mtu anagombea tena kwa kuhonga wapigakura.
Mwaka huu huenda tukawa na uchaguzi wa Serikali za mitaa, lakini mwakani tukawa na uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani watakaotuongoza kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Ni kipindi ambacho thamani ya waandishi wa habari hupanda kwa kipindi kifupi sana na kisha wanasiasa wakishaingia madarakani, huwatelekeza kama mafundi wanavyotumia karai la zege.
Nafahamu asilimia 75 ya wanahabari wote nchini ni wa kujitegemea ambao kimsingi wanalipwa kulingana na habari ama makala zitakazochapwa au kutangazwa na vyombo vya habari.
Ni ukweli malipo haya ni kidogo, lakini hiyo haiwezi kuhalalisha baadhi yetu kujiingiza katika vitendo vya kupokea hongo kutoka kwa wagombea ili tu wawaandike vizuri hata kama hawafai.
Maadili ya Uchaguzi Mkuu 2010 kwa wanahabari yaliweka sharti la lazima kwa wanahabari kuwahabarisha na kutoa elimu ya uraia kwa wapigakura ili wafanye uamuzi sahihi wakati wa kupiga kura.
Uamuzi sahihi ni kwa wapigakura kuchagua viongozi bora na siyo bora viongozi kwa sababu tu amepandishwa chati na wanahabari wakati dhamira yake ni kwenda kuchuma na si kusaidia jamii.
Wakati tunajiandaa na chaguzi nilizozisema, tayari wapo wagombea ambao wamekuwa ‘mzigo’ lakini wanajiandaa kufanya kila njia ili waweze kurudi tena bungeni kwa kipindi kingine.
Kuna taarifa zisizo rasmi baadhi yao wametenga hadi Sh200 milioni na sehemu ya fedha hizo imetengwa kwa ajili ya wanahabari wasioheshimu maadili ili wawasafishie njia hata kama hawafai.
Wanahabari tunapaswa kuanza kujitafakari sasa kama tumefanya nini kulisaidia taifa kupata viongozi bora, wazalendo na wenye dhamira ya dhati ya kuwaletea Watanzania maendeleo.
Haiwezekani leo hii tuna rasilimali kibao kuanzia madini ya kila aina, vivutio vya utalii, nishati ya gesi, wingi wa misitu na mazao ya baharini lakini Tanzania inakuwa miongoni mwa nchi maskini.
Hapa ni lazima tutafakari kauli ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere kuwa ili nchi iendelee inahitaji vitu vinne navyo ni ardhi, watu, siasa safi na uongozi bora. Ninasema tutafakari ni kipi tunachokikosa kati ya vitu hivyo vinne hadi Watanzania waendelee kuwa maskini licha ya kuwa moja ya nchi zinazoongoza barani Afrika kwa kuwa na rasilimali nyingi.
Hakuna ubishi tuna tatizo la uongozi ndio maana hatufiki kule tunakotaka kwenda na wanahabari wanalo jukumu zito la kuirudisha nchi hii kwenye mstari.
Chanzo;Mwananchi
 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2011. Singida Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogz za Mikoa