Mwenyekiti
wa bodi ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Anne Makinda
amezishauri hospitali, vituo vya afya na zahanati za serikali kuboresha
huduma za afya ili wananchi waliojiunga katika mifuko ya afya ya jamii
(CHF) na mfuko wa bima ya afya washawishike kutumia huduma katika
hospitali zao.
Makinda
ametoa rai hiyo alipotembelea hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida
kujionea huduma za Bima ya afya zinavyotolewa na changamoto zilizopo ili
kwa ushirikiano wa mfuko wa bima ya afya na wadau wake waweze
kuzitatua.
Amesema
hospitali na vituo binafsi au vya mashirika mbalimbali wamekuwa
wanufaikaji wakubwa wa kupata wateja wengi wa bima ya afya na mifuko ya
afya ya jamii kutokana na kusifiwa kuwa wanatoa huduma bora tofauti na
hospitali za serikali ambazo hupata wateja wachache na hivyo kupata
faida kidogo.
Makinda
amesema hamasa anayoitoa ya kuboresha huduma kwa vituo vya serikali
haimaanishi mfuko wa taifa wa bima ya afya hauthamini vituo na hospitali
binafsi bali inataka hospitali za serikali kuboresha huduma na kuingia
katika ushindani.
Ameongeza
kuwa changamoto ya ukosefu wa dawa na vifaa tiba inawakatisha tamaa
watumiaji wa bima ya afya pamoja na watu wengine kujiunga hata hivyo
mfuko wa bima ya afya na hospitali za serikali zimejipanga kuziondoa
changamoto hizo.
Aidha
Makinda ameupongeza Mkoa wa Singida kwa kufanya vizuri katika mfuko wa
afya jamii na bima ya afya huku akisisitiza kuendelea kuboresha ili Mkoa
wa Singida uwe mfano kwa mikoa mingine ya Tanzania.
Akitembelea
majengo mapya ya hospitali rufaa iliyopo eneo la Mandewa Makinda
amevutiwa sana na majengo hayo huku akiutaka uongozi wa Mkoa kwa
kushirikia na wadau wengine hasa mfuko wa bima ya afya kutafuta pesa za
ukamilishaji wa majengo muhimu ili huduma zianze kutolewa katika
hospitali hiyo kwakuwa itakuwa msaada hata kwa kanda nzima ya kati.
Naye
Mkuu wa Mkoa wa Singida Mheshimiwa Mhandisi Mathew J Mtigumwe
amemshukuru Anne Makinda kwa kuutembelea mkoa wa Singida ili kujionea
huduma za Bima ya afya zinavyotolewa.
Mheshimiwa
Mhandisi Mtigumwe amemuahidi Makinda kuwa Mkoa utaendeleza ushirikiano
mzuri na Mfuko huo na kuomba waendelee kutoa ushirikiano wa vifaa tiba
na ukarabati wa miundombinu ya hospitali na vituo vya afya vya serikali
ili kuboresha huduma za afya Mkoani Singida.
Ameongeza
kuwa Mkoa utaendelea kuhamasisha wananchi kujiunga na mfuko wa afya ya
jamii na bima ya afya ili wapate huduma bora hata wakati wakiwa na
upungufu wa fedha kwani bima huokoa maisha.
0 comments:
Post a Comment