Kiwango cha ufaulu wa 
mitihani ya kumaliza elimu ya msingi Mkoani Singida kimepanda kutoka 
wastani wa asilimia 58.41 mpaka asilimia 69.25 ikiwa ni ongezeko la 
asilimia 11 huku wanafunzi 14,759 wakichaguliwa kujiunga na masomo ya 
sekondari kwa kidato cha kwanza kwa mwaka 2017.
Buhacha Baltazar Kichinda 
akiongoza kikao cha uteuzi wa wanafunzi wa kidato cha kwanza kwa mwaka 
2017 kama Kaimu Katibu Tawala Mkoa na mwenyekiti wa kikao hicho amesema 
mkoa umefaulisha wavulana 6,852 na wasichana7,907 huku akiwapongeza 
waalimu wote kwa bidii ya ufundishaji iliyopelekea mkoa wa singida 
kushika nafasi ya 12 kati ya Mikao 26 ya tanzania bara.
Kichinda ameipongeza 
halmashauri ya Itigi kwa kushika nafasi ya kwanza kati ya halmasahuri 
saba za mkoa wa singida na ya 38 kitaifa kati ya halmashauri 186 za 
Tanzania bara huku ikifaulisha kwa asilimia 80.41. Aidha amewatia moyo 
halmasahuri ya Mkalama kwa ufaulu hafifu wa 57.51 na kuwa nafasi ya 155 
 kitaifa.
Kichinda ameongeza kuwa kwa
 sasa kila Mkurugenzi wa halmasahuri anapaswa kukaa na wadau wake wa 
elimu ili kupanga mikakati ya kuboresha zaidi elimu, amesema lengo kubwa
 kwa sasa ni kuhakikisha kila mwanafunzi aliyefaulu anajiunga na kidato 
cha kwanza na kumaliza elimu ya sekondari.
Amesema sekta ya elimu 
inachangamoto mbalimbali ikiwemo utoro wa walimu na wananfunzi, 
miundombinu ya vyumba vya madarasa kutotosheleza mahitaji halisi, 
upungufu wa waalimu, uhaba wa nyumba za walimu pamoja na waalimu wenyewe
 kuwa wachache tofauti na mahitaji halisi hivyo amewata wadau wa elimu 
kujipanga kutatua changamoto hizo na sio kusubiria serikali kuu kufanya 
kila kitu.
Aidha kichinda amesema 
kuwepo na utaratibu wa kuwapongeza waalimu hasa kwenye shule zilizofanya
 vizuri ili iwe motisha kwa kazi wanayoifanya huku akiitangaza shule ya 
msingi Utaho ya halmasahuri ya Ikungi kuwa ya kwanza kimkoa kwa shule 
zenye wananfunzi zaidi ya 40 na shule ya msingi Aghondi ya Itigi kuwa ya
 kwanza kimkoa kwa shule ambazo zina wanafunzi chini ya 40.
Naye Mkuu wa Wilaya ya 
Singida Elias Tarimo amesema ili kuboresha elimu mkoani Singida 
msisitizo uwepo wa kuhakikisha wananfunzi wote wanapata chakula shuleni 
ili waweze kusikiliza kwa umakini mzuri.
Tarimo ameongeza kuwa 
wazazi wanapaswa kutambua kuwa elimu bila malipo haiwaondolei wajibu wao
 kama wazazi wa kuhakikisha wanafunzi wanakula, wanalala na kuvaa hivyo 
hivyo watakaposhirikishwa katika kuchangia chakula, ujenzi wa mabweni au
 shuguli za elimu wajitoe kwani wamiliki wa shule ni wazazi.
Amesema utaratibu wa 
kufanya ukaguzi ili kuwatambua waalimu watoro au wazembe ufanyike katika
 halmashauri zote na kwa viongozi wote wanaotembelea vijijini bila ya 
kusubiri ziara maalumu ya ukaguzi na kuongeza kuwa hali hiyo 
itawaongezea umakini waalimu katika kutekeleza majukumu yao lakini pia 
watendaji watabaini changamoto za waalimu na shule na kuzitatua kwa 
uharaka. 
0 comments:
Post a Comment