Home » » ANANITUKANA KISA NIMEMKATAA KIMAPENZI

ANANITUKANA KISA NIMEMKATAA KIMAPENZI

 Shikamoo shangazi mkubwa. Mimi ni msichana mwenye miaka 26. Kuna kijana mmoja hapa mtaani kwetu alikuwa akinifuatilia kwa muda mrefu sana. Anataka niwe naye kimapenzi. Baada ya kuchekecha niliona siyo wa aina yangu hivyo nikamtosa. Kitendo cha kumkataa imekuwa shida sasa. Mana kila ninapokutana naye ananitukana. Nifanyeje?
Ramla,
Dar es Salaam.
Muonye kuhusiana na tabia yake hiyo. Kama bado anaendelea nenda katoe taarifa polisi maana ni makosa kisheria kumtukana mtu.
Nampenda lakini naogopa kumwambia
Pole na majukumu shangazi mkubwa. Nimetokea kumpenda msichana mmoja. Kila ninapomuona nahisi anafaa kuwa mama wa watoto wangu. Tatizo ni kwamba naogopa kumwambia kwani nahisi kuwa hatanikubali. Nifanyeje shangazi?
Juma,
Dar es Salaam.
Usihofu kukataliwa unapotaka kuomba kaka, maana yote ni majibu sahihi. La msingi ni kumwambia ili kujua msimamo wake.
Anataka tuzae kwanza ndipo anioe
Shangazi mimi ni msichana mwenye umri wa miaka 26. Nimemaliza chuo na nimebahatika kupata kazi kwenye kampuni moja hapa mjini. Tatizo ni kwamba, kuna mvulana nimempata ninahisi ananipenda sana. Lakini kila tunapoongea suala la ndoa anadai kuwa ni vyema nizae kwanza ndipo anioe. Ni sahihi shangazi?
Jane,
Mbeya.
Wala si sahihi Jane. Hiyo si mboga kusema hawezi kula hadi aonje kwanza. Kuwa na msimamo, wambie hakuna kuzaa hadi ipite ndoa kwanza.
Nyumba ndogo yangu inataka ndoa
Shangazi mimi ni mwanaume mwenye mke na watoto wawili. Tatizo langu ni kwamba nimekuwa na mwanamke nje ya ndoa yangu kwa miaka sita sasa. Mwanamke huyo amekuwa akinishawishi nimuoe. Lakini kimsingi dini yangu hairuhusu. Nifanyeje?
Japhet,
Dar es Salaam.
Wala sina ushauri juu ya hilo. Mana kwa kuwa unafahamu kama dini yako hairuhusu sasa unanitaka la rohoni au?
Mke wangu amenitelekeza na watoto
Pole na majukumu shangazi mkubwa. Mimi ni baba wa watoto watatu. Nimekuwa kwenye ndoa kwa muda wa miaka kumi sasa. Hivi karibuni mke wangu alinikimbia, mbaya zaidi amebeba hadi nguo zake na vitu vyake muhimu nifanyeje?
Baba George,
Dar es Salaam.
Kwanza katoe taarifa katika kituo cha polisi. Pili wafahamishe ndugu zake. Ukimaliza hakikisha watoto wako wanakuwa katika mikono salama. Hilo likiwa sawa endelea na maisha yako maana inaonekana alidhamiria na anajua anachokifanya. Kitendo cha kumfuatilia kitakupotezea muda.
Nasumbuliwa na wapenzi wangu wa zamani
Hujambo shangazi mkubwa? Mimi ni mwanaume mwenye umri wa miaka 30. Baada ya kuzunguka katika mambo yetu yale kwa muda mrefu, nimepata yule anayenifaa na nimeshafunga naye ndoa. Tatizo ni kwamba, wale wapenzi niliokuwa nao zamani wamekuwa wakinisumbua kwa meseji kwenye simu na wakati mwingine wanadiriki hata kumtukana mke wangu. Nifanyeje ili waachane na maisha yangu. Kimsingi naona wanaweza kuniharibia.
James,
Tanga.
Kwanza tafuta muda uongee na mkeo. Hakikisha humfichi kitu juu ya maisha yako yaliyopita. Akishakuelewa utakuwa ushaweka uzio. Hakuna atakayeweza kubomoa ndoa yenu. Ukimaliza waweke wazi kuwa hakuna kitakachoendelea baina yenu kwani tayari wewe ni mume wa mtu. Hapo heshima itachukua mkondo wake.
Rafiki yake anadai ni kahaba
Shangazi rafiki wa mpenzi wangu amenitumia ujumbe akidai kuwa mpenzi wangu huyo ni kahaba. Inawezekana kuna ukweli au hapendi tu mimi kuwa naye. Nishauri shangazi
Alphonce
Dar
Usikurupuke katika maamuzi. Jitahidi kulifanyia kazi, nina hakika jibu lake halipo mbali.
 Chanzo:Mwananchi
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2011. Singida Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogz za Mikoa