Home » » CCM Singida yabariki agizo la RC Kone

CCM Singida yabariki agizo la RC Kone



Na Nathaniel Limu
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Singida, kimebariki amri halali iliyotolewa na mkuu wa mkoa wa Singida, Dk. Parseko Kone, ya kupiga marufuku wafanyabiashara binafsi kununua alizeti moja kwa moja kutoka kwa mkulima.

Baraka hizo zimetolewa na chama hicho katika kikao chake cha halmashauri kuu kilichofanyika Julai 5, mwaka huu mjini hapa.

Kwa mujibu wa tamko la chama hicho lililotolewa na CCM mkoa wa Singida, limeeleza kuwa pamoja na mambo mengine, limebaini kuwa amri hiyo ni halali, haikueleweka vizuri kwa wananchi.

Mbali na hatua hiyo CCM, imeagiza elimu ya kutosha kuhusu amri hiyo, itolewe ili lengo la amri hiyo liweze kutekelezwa kwa makini.

Taarifa hiyo ya CCM imeeleza kuwa, amri iliyotolewa na Mkuu wa mkoa wa Singida Dk. Parseko Kone, haikukataza mtu au kikundi chochote kununua zao la alizeti, isipokuwa imeelekeza kwamba ni vyama vya msingi vya ushirika ndivyo vitakavyonunua moja kwa moja zao hilo kutoka kwa wakulima na kisha kuwauzia wafanyabiashara binafsi.

Awali agizo hilo la Mkuu wa mkoa liliagiza kwamba mbali na vyama vya ushirika kuwepo, yaanzishwe magulio katika maeneo mbalimbali ambayo wakulima wa alizeti watauza kwa watu mbalimbali, kwa kufuata bei elekezi kama njia ya kuwanufaisha moja kwa moja kuliko ilivyokuwa awali.

“Wenye viwanda vya kukamua mafuta, wanaruhusiwa kuanzisha ushirika wao wa kununua alizeti, ili mradi wafuate bei elekezi,” ilieleza taarifa hiyo ya CCM katika tamko lao

Akifafanua zaidi, Dk. Kone, alisema hivi sasa ameteua kamati ambayo itajikita katika kuhakiki uwepo na uwajibikaji wa vyama vya msingi vya ushirika.

“Pia tutachunguza uwajibikaji wa viongozi wa vyama hivyo kuanzia ngazi ya mrajisi wa vyama vya msingi vya ushirika juu ya uadilifu na utendaji kazi wao. Wale ambao wataonekana kuwa kikwazo katika maendeleo ya wakulima wa alizeti, tutawashughulikia mara moja,” alisema RC Kone
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2011. Singida Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogz za Mikoa