Home » » MWENYEKITI WA KITONGOJI AFUNGWA KWA WIZI

MWENYEKITI WA KITONGOJI AFUNGWA KWA WIZI


na Jumbe Ismailly, Singida
MWENYEKITI wa Kitongoji cha Miyombwe, Kijiji cha Mkinya, wilaya mpya ya Ikungi amehukumiwa kifungo cha miaka miwili jela baada ya kupatikana na hatia ya wizi wa sh 100,000 iliyokuwa itumike kugharamia ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Kata ya Dungunyi, wilayani hapa.
Mwenyekiti huyo, Michael Khaliki (53) amehukumiwa kifungo hicho na Hakimu Terisophia Tesha wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida.
Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Tesha alisema ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka umethibitisha bila kuacha shaka kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo aliloshitakiwa nalo.
Alisema kutokana na kosa hilo, anampa adhabu ya kulipa faini ya sh 300,000 na akishindwa atumikie kifungo cha miaka miwili jela.
Hata hivyo, mshitakiwa huyo alishindwa kulipa faini hiyo, hivyo kulazimika kwenda kuanza kutumikia kifungo hicho.
Awali, Mwanasheria wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Singida, Antidius Rutayuga, aliiomba mahakama itoe adhabu kali kwa mshitakiwa, ili iwe fundisho kwake na watu wengine wenye tabia kama hiyo.
Kwa upande wake, mshitakiwa Michael aliiomba mahakama imhurumie kwa kuwa ni kosa lake la kwanza na pia ana familia kubwa inayomtegemea.
Katika kesi hiyo, ilidaiwa kuwa Septemba 16 mwaka 2008 katika Kijiji cha Mkinya, mshitakiwa alitumia sh 100,000 kwa matumizi yake binafsi iliyokuwa itumike katika ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Kata ya Dungunyi.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2011. Singida Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogz za Mikoa