Home » » MBUNGE ASIHI WAKAZI WA SINGIDA KUIPIGIA KURA CCM

MBUNGE ASIHI WAKAZI WA SINGIDA KUIPIGIA KURA CCM

MBUNGE wa Singida Mjini, Mohammed Dewji amewasihi wakazi wa Halmashauri ya Manispaa ya Singida kukipigia kura Chama Cha Mapinduzi wakati wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa nchini ili kukiwezesha kutekeleza Ilani yake kwa urahisi zaidi.
Mbunge huyo alitoa mwito huo juzi wakati wa uzinduzi wa kampeni za uchaguzi wa Serikali za Mitaa katika hafla iliyofanyika kwenye eneo la soko la zamani la Kibaoni mjini hapa.
Alisema chaguzi za Serikali za Mitaa ni jiwe la msingi la nyumba inayojengwa na serikali yoyote ile, hivyo ili kuiwezesha nyumba hiyo kuwa imara wakazi wote wa Jimbo la Singida Mjini hasa wana- CCM, hawana budi kuipigia CCM kura nyingi ili kuiimarisha kisiasa.
Alisema kuwa kwa vile tayari Mbunge wa jimbo hilo ni wa CCM, ingekuwa vizuri zaidi iwapo wananchi wataendelea kukiamini na kukipigia kura za ndio chama hicho ili kuweka mnyororo sahihi kwa ajili ya utekelezaji wa Ilani ya Chama na maendeleo katika jimbo hilo.
Katika uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika nchini kote baadaye mwezi huu, Chama Cha Mapinduzi Singida Mjini kimejihakikishia ushindi katika mitaa 14 kati ya 50 iliyopo, vijiji sita kati ya 20 na vitongoji 36 kati ya 83 baada ya vyama pinzani kuacha kuweka mgombea.
Wakati huo huo, MO amewataka wakazi wa Singida Mjini kukamilisha ujenzi wa maabara kwa shule za sekondari na kuanza kujenga madarasa kwa ajili ya Kidato cha Tano katika shule zao ili kuwa na uhakika wa kuwapatia nafasi za kuendelea na masomo ya juu wote watakaofaulu.
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Chanzo;Habari Leo

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2011. Singida Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogz za Mikoa