Home » » WANAFUNZI WASOMEA SEBULENI KWA MWALIMU

WANAFUNZI WASOMEA SEBULENI KWA MWALIMU

 WANAFUNZI 173 wanaosoma darasa la awali katika Shule ya Msingi Minga, iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Singida, wanasomea kwenye sebule ya nyumba ya mwalimu kutokana na upungufu wa vyumba vya madarasa unaoikabili shule hiyo.

Mwalimu Mkuu Msaidizi wa shule hiyo, Gregory Manimo, alibainisha hayo kwenye mahafali ya nne ya kuwaaga wanafunzi 162 wa shule ya msingi Minga.

Alisema kwa sasa shule hiyo ina vyumba 10 vya madarasa wakati mahitaji ya vyumba ni 38, huku kukiwa na vyumba viwili vya madarasa vilivyofikia hatua ya kupauliwa, nyumba mbili za walimu, ofisi moja ya mwalimu mkuu na ofisi mbili za walimu.

“Shule ina madawati 188, meza 12, viti 27, nyumba mbili za walimu huku kukiwa na nyumba moja iliyoanza kujengwa kwa nguvu za wananchi tangu mwaka 2006. Nyumba hii hadi bado haijakamilika na pia shule ina huduma za umeme na maji,” alisema mwalimu huyo.

Hata hivyo, alisema pamoja na mafanikio hayo, shule inakabiliwa na matatizo mbalimbali likiwamo la upungufu wa vyumba 28 vya madarasa, madawati 229, viti vitano, meza 20, nyumba za walimu 30 na chumba cha darasa la awali.

Kwa mujibu wa mwalimu mkuu huyo msaidizi, upungufu huo wa chumba cha darasa la awali umesababisha kwa sasa wanafunzi wake 173 kusomea kwenye sebule ya nyumba ya mwalimu wao.

Shule ya Minga, iliyoanza mwaka 2000 wakati huo ikijulikana kwa jina la Mughanga B, ilisajiliwa mwaka 2003 na kupewa jina hilo, ikiwa na wanafunzi 444 wa Darasa la Kwanza hadi la Nne.
 Chanzo;Tanzania Daima
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2011. Singida Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogz za Mikoa