NAIBU WAZIRI TAMISEMI AZIAGIZA HALMASHAURI KUTUMIA ‘MAFUNDI WAZAWA’ KATIKA MIRADI MIDOGO; AFURAHISHWA NA MIRADI YA WILAYANI MKALAMA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) Joseph Kakunda akipima kiasi cha saruji kilichowekwa kwenye mchanga katika ujenzi shule ya Sekondari Iguguni Wilayani Mkalama katika ziara yake ya Siku moja kufuatilia utoaji huduma mbalimbali kwa jamii.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) Joseph Kakunda akisisitiza jambo mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhandisi Jakson Masaka (kulia kwake) na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Mhandisi Godfrey Sanga (kushoto kwake).
Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) Joseph Kakunda akisalimiana na mwenyeji wake Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhandisi Jaksoni Masaka mara baada ya kuwasili wilayani humo kwa ajili ya Ziara ya ufuatiliaji wa miradi ya elimu na maji.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) Joseph Kakunda akisalimiana na Katibu Tawala wa Wilaya ya Mkalama Elizabeth Rwegasira mara baada ya kuwasili wilayani humo kwa ajili ya Ziara ya ufuatiliaji wa miradi ya elimu na maji.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) Joseph Kakunda ameziagiza halmashauri zote nchini kutumia mafundi wa kawaida wazawa waliopo katika maeneo yao katika miradi yote midogo kupitia utaratibu unaojulika kama ‘force account’. Naibu Waziri Kakunda ametoa agizo hilo jana mara baada ya kufanya ziara Wilayani Mkalama kufuatilia utoaji wa huduma mbalimbali kwa jamii huku akijikita zaidi katika sekta ya Maji na Elimu, ambapo ametembelea mradi wa maji Iguguno na Shule ya Sekondari Iguguno.

“Matumizi ya Wakandarasi yabaki katika miradi mikubwa tu lakini miradi yote midogo tuwatumie mafundi waliopo katika maeneo yetu, mafundi hawa wazawa wanatekeleza kazi kwa ubora kama huu ambao nimeuona leo na kwa gharama ambazo ni nzuri,” amesisitiza mara baada ya kutoa agizo hilo. Ameeleza kuwa gharama na ubora wa mradi wa Shule ya Sekondari ya Iguguno ambao unajumuisha ujenzi na ukarabati wa madarasa 8, mabweni mawili, vyoo vyenye matundu 11, bwalo la chakula na maabara ambapo vyote hivyo vimegharimu milioni 416, unatosha kudhirihisha kuwa mafundi wa kawaida wazawa wanaweza kufanya kazi nzuri.

“Huu mradi endapo tungetumia utaratibu wa wakandarasi na wazabuni hiyo gharama ya milioni 416 ingekuwa kama robo ya gharama, nasisitiza wakandarasi na wazabuni watumike katika miradi mikubwa tu”, Naibu Waziri Kakunda amesisitiza.

Ameongeza kwa kuipongeza halmashauri hiyo kwa kutekeleza mradi mkubwa wa maji ambao umewezesha usambazaji wa maji katika kata yote ya Iguguno na kuwasaidia wananchi wasihangaike kupata maji. Aidha Naibu Waziri Kakunda ameonekana kutofurahishwa na taarifa kuhusu wanafunzi 12 waliokatishwa masomo tangu mwezi Januari Mwaka huu kutokana na sababu ya kupewa ujauzito, ambapo ametoa rai kwa wazazi na walezi wote nchini kuwa mstari wa mbele kukomesha tatizo hilo.

Ameeleza kuwa wazazi wengi wamekuwa wakifanya makubaliano ambapo mwanafunzi aliyepewa ujauzito anamkana mhalifu aliyempa ujauzito ili kumuepusha na kifungo cha miaka 30 jela, jambo linalofanya kesi nyingi kukosa ushahidi huku tatizo la mimba kwa wanafunzi likiendelea kuwepo.

Naibu Waziri Kakunda amesema ili kukomesha hilo serikali kupitia Wizara yake ina dhamira ya kupeleka hati ya dharula bungeni ili itungwe sheria itakayofuta dhamana ya mtuhumiwa atakayempa ujauzito mwanafunzi huku uchunguzi wa Vinasaba (DNA) utatakiwa kufanyika ili kuthibisha kama mtuhumiwa ndiye baba wa mtoto ama la.

Awali, Mbunge wa jimbo la Mkalama Mhe. Alan Kiula amewasilisha changamoto mbalimbali za Wilaya hiyo kwa Naibu Waziri Kakunda kwa kumueleza changamoto kubwa ni kutokuwa na hospitali ya Wilaya.

Mhe. Kiula ameongeza kuwa upungufu wa watumishi katika Wilaya hiyo hasa wa Sekta ya Elimu na Afya umekuwa ukikwamisha baadhi ya shughuli kufanyika kwa kasi inayotakiwa.

Aidha amemshukuru Naibu Waziri Kakunda kwa ahadi yake ya kuitazama Wilaya hiyo kwa jicho la pekee katika mgao ujao wa watumishi kwa Mwezi Disemba na Januari huku akimuhakikishia kuwa Halmashauri itafanya kwa haraka taratibu za awali za upatikanaji wa eneo kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya Wilaya.

BWANA HARUSI AFARIKI, MKEWE AJERUHIWA AJALINI WAKITOKA KUFUNGA NDOA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Imeandikwa na Abby Nkungu, Singida.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Debora Magiligimba
WATU 12 wamekufa na wengine 22 kujeruhiwa katika ajali iliyotokea kijiji cha Ighuka wilayani Ikungi kwenye Barabara Kuu ya Singida – Manyoni baada ya Toyota Hiace walimokuwa wakisafiria kutoka kumchukua bibi harusi kugongana uso kwa uso na Toyota Noah iliyokuwa imepakia watu kutoka msibani.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Debora Magiligimba alisema kuwa ajali hiyo ilitokea juzi saa mbili usiku kwa kulihusisha gari lenye namba za usajili T 581 BBV iliyokuwa ikitokea Singida kwenda Manyoni na T 423 CFF iliyokuwa ikitokea Manyoni kwenda Singida.
Alisema kuwa ingawa uchunguzi wa kina juu ya chanzo cha ajali hiyo bado unaendelea, taarifa za awali zinaonesha kuwa sababu kuu ni mwendo kasi na uzembe wa madereva.
“Baadhi ya majeruhi walituambia dereva wa Toyota Hiace aliyekuwa anatoka Singida mjini alihama kutoka upande wake na kwenda upande wa pili wa barabara ambako aligongana uso kwa uso na Noah iliyokuwa imebeba watu waliokuwa wakitoka msibani na kusababisha vifo vya abiria 10 hapo hapo na majeruhi 24,” alisema.
Mganga Mfawidhi Hospitali ya Rufaa mkoa wa Singida, Dk Ng’hungu Kusenza alisema kuwa majeruhi wawili waliofikishwa Hospitali ya Misheni Puma kwa ajili ya matibabu pia walikufa hivyo kufanya idadi ya watu waliokufa kuwa 12.
Aliwataja waliokufa ambao miili yao imehifadhiwa Hospitali ya mkoa kuwa ni John Duma, Jasson Nsunza, Abubakar Omari, Mary Kinku, Mwanaidi Juma na Husna Juma, Wengine ambao miili yao imehifadhiwa Hospitali ya Misheni Puma wilayani Ikungi ni Ezekiel Joseph, Mussa Daniel, Namtaki Daniel, Hamis Omari, Jumanne Mganga na Wansola Shalua. Habari ambazo hazijathibitishwa zinadai kuwa Bwanaharusi na madereva wa magari yote mawili ni miongoni mwa watu waliopoteza maisha katika ajali hiyo.
CHANZO HABARI LEO 

MIZAHA KATIKA MIRADI YA MAJI HAITAVUMILIWA MKOANI SINGIDA.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 


Ofisi ya Mkuu wa Mkuu wa Mkoa wa Singida imedhamiria kusimamia uboreshaji wa huduma za maji mkoani hapa huku mizaha itakayofanywa na mtu yeyote katika miradi ya maji, kutovumiliwa.

Kaimu Katibu Tawala Sehemu ya Maji Mkoa wa Singida Mhandisi Lyidia Joseph amebainisha hayo leo wakati wa kikao maalumu na Timu ya usimamizi wa sekta ya maji ya halmashauri ya Wilaya  ya Manyoni, kwa ajili ya kufuatilia usimamizi na utekelezaji wa miradi ya maji.

Mhandisi Lydia amewaeleza wataalamu hao kuwa uongozi wa mkoa hautavumilia endapo kuna mtumishi yeyote atafanya mzaha katika kusimamia miradi ya maji kwakuwa mkoa umekuwa ukitoa ushirikiano wa kutosha hivyo hakuna sababu ya kushindwa kufanya vizuri.

“Sisi katika ngazi ya mkoa hatutavumilia mzaha katika masuala ya maji, tupo tayari kutoa ushirikiano popote mnapoona mnakwama ili tu tufikie malengo yetu ya kutoa huduma bora za maji kwa wananchi, hali ilivyo sasa hairidhishi kabisa, tufanye kazi kwa kasi zaidi”, ameongeza Mhandisi Lydia.

Amesema, halmashauri hiyo inapaswa kuhakikisha inatekeleza agizo la Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi la kuongeza asilimia ya upatikanaji wa maji katika halmashauri hiyo kutoka 45 hadi 72 ifikapo mwezi Juni, 2018 pamoja na kuandaa takwimu sahihi za upatikanaji wa maji ifikapo Disemba mwaka huu.

Mhandisi Lydia amefafanua kuwa halmashauri hiyo itaweza kuongeza asilimia ya upatikanaji maji na kufikia lengo la asilimia 72 endapo watendaji wote hasa wajumbe wa timu ya usimamizi wa sekkta ya maji, watashirikiana kusimamia ujenzi wa miradi mitano pamoja na ukarabati wa miradi minne iliyopo kwenye bajeti.

“Kila Mjumbe hapa ana kazi ya kufanya katika miradi hii ya Makanda, Nyaranga, Kikombo, Makutopola na Kicheho inayojengwa pamoja na ile ya Sanza, Mkwese, Londoni na Sorya inayokarabatiwa, Kitengo cha ugavi kisimamie taratibu za manunuzi zinafuatwa pamoja na kuhakiki ubora wa mkandarasi, mwanasheria aelekeze taratibu za kisheria, Maendeleo ya jamii ahakikishe wananchi wanaujua mradi vizuri, kila mmoja akitekeleza jukumu lake ipasavyo tutafikia lengo”, ameeleza na kuongeza kuwa,

“Idara ya maji msifanye siri miradi ya maji na kujifungia wenyewe hakikisheni timu hii ya usimamizi wa sekta yenu inafahamu vizuri miradi yote ya maji pamoja na kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo, mkifanya hivyo mtaenda kwa kasi na kazi itafanyika kwa ufanisi, sio kila kitu mfanye wenyewe tu”, ameongeza Mhandisi Lydia.

Aidha Mhandisi Lydia amempongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni Charles Fussi kwa kujitoa kwake katika kusimamia na kutoa fedha za kusaidia miradi ya maji akitoa mfano wa kiasi cha milioni 16 zilizotolewa na mkurugenzi huyo kutoka katika makusanyo ya ndani kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa maji.

Naye Mhandisi wa Maji kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Athanas Nziku ameieleza timu hiyo kuwa usimamizi wa jumuiya za watumia maji ni jambo muhimu kwakuwa takwimu zimeonyesha jumuiya hizo zimekuwa zikikusanya pesa nyingi sambamba na matumizi makubwa ya fedha wanazokusanya.

Mhandisi Nziku amewafafanulia kuwa jumuiya hizo za watumia maji zinapokusanya fedha nyingi sambamba na kutumia fedha nyingi ni moja ya kiashiria kuwa miradi hiyo ya maji inaweza kufa hivyo wazitembelee na kuona tatizo liko wapi endapo liko ndani ya uwezo wa halmashauri liweze kutatuliwa mapema.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Mkwese na Mwenyekiti wa huduma za Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni Robert Kenze amesema, halmashauri hiyo imedhamiria kuboresha huduma za maji ambapo ajenda ya maji imewekwa kipaumbele katika vikao vyote muhimu.

Kenze amesema wakuu wa Idara wa halmashauri hiyo watashirikiana na Idara ya maji wilayani humo huku wanasiasa wakiwa tayari kutoa elimu na kusimamia utekelezaji wa miradi ya maji.

ZOEZI LA USAJILI VITAMBULISHO VYA TAIFA LASHIKA KASI MKOANI SINGIDA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

Mkuu wa Kitengo cha Biashara Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa – NIDA Ndugu Thomas William pamoja na Ndugu Innecent Baraza Meneja Usimamizi wa Majengo (Kushoto) wakifuatilia kwa karibu Uingizwaji wa taarifa za waombaji wa Vitambulisho vya Taifa wakati wa Zoezi la Usajili na Utambuzi linaloendelea Mkoa wa Singida. 
Wanachi katika Halmashauri ya Manispaa ya Singida, wakifanyiwa usajili wa Maombi ya Vitambulisho vya Taifa katika zoezi la Usajili wa Mkupuo (Mass Registration) linaloendela hivi sasa Mkoani humo.
Baadhi ya Wananchi katika kata ya Kindai Halmashauri ya Manispaa Singida wakiwa kwenye foleni kuelekea kwenye chumba cha uchukuaji alama za kibaiolojia, picha na saini ya kielektroniki. 
Mkuu wa Kitengo cha Biashara Mamlaka ya Vitambulisho Ndugu Thomas William akisimamia zoezi la ugawaji wa fomu za Usajili wa Vitambulisho vya Taifa.

SERIKALI IMETOA BURE MBEGU NA VIUATILIFU KWA AJILI YA KILIMO CHA PAMBA KWA MKOA WA SINGIDA.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi (katikati) akimkabidhi mmoja kati ya wa wakulima wa Pamba wa kijiji cha Kinyangiri Wilayani Mkalama kilo kumi za mbegu za zao la pamba zilizotolewa bure na Serikali kwa wakulima hao. Kushoto kwa Mkuu wa Mkoa ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bodi ya Pamba nchini, Marco Mtunga.

Mkulima wa Pamba Bi Johari kutoka kijiji cha Kinyagiri Wilayani Mkalama akibeba mbegu za Pamba kilo kumi alizokabidhiwa na Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi, mbegu hizo zimetolewa bure kwa wakulima wa Pamba Mkoa wa Singida.
Mama Devid Mkulima wa Pamba wa Kijiji cha Kinyangiri Wilayani Mkalama akijifunza kwa vitendo namna ya kuandaa kamba inayotumika kuonyesha vipimo vya upana na urefu katika kupanda pamba badala ya kilimo cha mazoea cha kumwaga mbegu bila kufuata kipimo chochote.
Wakulima wa Pamba wa Kijiji cha Lyelembo Wilayani Mkalama wakiwasikiliza Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bodi ya Pamba nchini Marco Mtunga (hawapo pichani) kabla ya kupewa mbegu za pamba zilizotolewz bure.
Wakulima wa pamba wa kijiji cha Kinyangiri Wilayani Mkalama wakimfuatilia kwa makini mtaalam kutoka Bodi ya Pamba Nchini akiwaelekeza namna ya kupuliza dawa ya kuuwa wadudu waharibifu wa pamba, viuatilifu hivyo vitatolewa bure na serikali kwa wakulima wote wa pamba Mkoani Singida.

Serikali imeahidi kutoa bure pembejeo za kilimo kwa wakulima mbali mbali wa zao la pamba mkoani Singida kuanzia msimu huu wa kilimo ikiwa ni moja ya juhudi za kuhamasisha na kufufua kilimo hicho mkoani hapa.  
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bodi ya Pamba nchini, Marco Mtunga ameeleza hayo juzi katika vijiji vya Kinyangiri na Lyelembo wilayani Mkalama katika siku ya kwanza ya ziara yake ya siku mbili kuhimiza Kilimo cha pamba mkoani Singida. 
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, Kampuni ya Biosustain iliyopo mjini hapa imepewa jukumu la kuleta na kusambaza mbegu na madawa yote yahusuyo kilimo cha pamba bure na kwamba gharama ya pembejeo hizo italipwa na Serikali. 
Kutokana na hilo, Mkurugenzi huyo amewataka Wakulima kutumia vyema fursa hiyo kwa kulima mashamba makubwa zaidi lakini pia kwa kuzingatia tija na ubora wa pamba. 
Amesema kuwa Wakulima wataweza kufanya hivyo tu iwapo pia watawatumia kikamilifu wataalamu wao wa kilimo na kufuata Kanuni na Taratibu za kilimo bora. 
“Mmepewa upendeleo maalum, kazi yenu sasa ni kulima tu, malipo ya mbegu na viuatilifu vyote italipwa na Serikali. Hapa hakuna kisingizio cha kushindwa kulima”, amesema Mtunga na kuongeza;
“Pandeni vizuri ili wakati mnatumia dawa, kiwango kikubwa cha dawa kisipotee bure maana kama hukupanda kwa mstari lazima kutakuwa na ugumu wa kupulizia mimea yako. Jengeni utamaduni wa kuwatumia wataalamu wa kilimo kama ilivyo kwa wafugaji mifugo yao inapopatwa na maradhi”.  
Aidha, amewataka wakulima wa zao hilo kuhakikisha wanang'oa masalia yote ya misitu ya pamba na kuichoma moto kwa kuwa, kwa kuacha kufanya hivyo wanaruhusu wadudu waliomo kwenye masalia kuendelea kunenepeana na hivyo kuhatarisha mazao mapya yanayopandwa.  
Mkurugenzi huyo amewasihi wakulima kuacha kuchanganya kilimo cha pamba na mazao mengine akisema kuwa tafiti zinaonesha pamba iliyochanganywa na mazao mengine hutoa vitumba vitatu tu ikilinganishwa na vitumba 10 kwa kilimo cha pamba iliyolimwa peke yake. 
Wakulima wa zao hilo wamemueleza Mkurugenzi huyo kuwa, moja ya sababu za kushuka kwa uzalishaji pamba kwenye maeneo yao ni pamoja na bei kuwa ndogo kwa kisingizio cha Soko la Kimatafa kushuka na kuchezewa mizani wanazotumia kupima mazao yao, hali inayowapunja kimapato.  
Hata hivyo, wamejibiwa kuwa suluhisho la kuchezewa mizani lipo mikononi mwao ili mradi tu wajenge tabia ya kuhoji mara moja wanapoona mambo yanaenda isivyo badala ya kusubiri hadi siku ya vikao.
Wakati huohuo Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi amewataka watendaji wote wa serikali na Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoani Singida kulima ekari moja ya pamba kila mmoja ili kuamsha hamasa kwa wananchi wengine.
Dkt Nchimbi ameongeza kwa kuwataka watendaji hao kuliweka zao la pamba kama ajenga katika vikao vyao, huku akiwataka viongozi wa dini na vikundi vya kwaya kuonyesha mfano kwa kulima vizuri pamba.
Ameongeza kuwa vijana wanaocheza vijiweni ‘pooltable’ waache mara moja na kujikita katika kilimo cha pamba kwa kuwa ni chanzo kikubwa na cha uhakika cha kujipatia fedha na hivyo kuchangia kukuza uchumi.
Aidha amewataka wakulima wa pamba kuwasikiliza wataalamu na sio kupanda kwa mazoea huku akishauri kuwa mikutano yote inayohusu kilimo cha pamba ifanyike katika mashamba ya wakulima.
Dkt Nchimbi ameeleza kuwa kauli mbiu mpya ya kilimo cha pamba kwa Mkoa wa Singida ni, ‘Singida Mpya, kwa Pamba yenye Tija’.

SPIKA WA BUNGE ATANGAZA JIMBO LA SINGIDA KASKAZINI LIPO WAZI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2011. Singida Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogz za Mikoa