Home » » WENYE MAAMBUKIZI YA VVU WAJIUNGA KWENYE VITUO

WENYE MAAMBUKIZI YA VVU WAJIUNGA KWENYE VITUO

ZAIDI ya asilimia 69 ya watu waliobainika kuwa na maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) mkoani Singida wamejiunga kwenye vituo vya tiba na matunzo (CTC) na kuanza kupewa dawa za kupunguza makali ya VVU katika kipindi cha miaka tisa iliyopita.
Mratibu wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS) Mkoa wa Singida, Edson Mdala alisema hayo juzi wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani yaliyofanyika kimkoa katika kijiji cha Musimi kata ya Sepuka wilayani Ikungi.
Mdala alisema kuwa tangu 2005 hadi kufikia Juni mwaka huu, jumla ya watu waliopimwa VVU na kujiandikisha CTC ni 17,720, kati yao 12,286 wanapata dawa za kufubaza makali ya virusi vya Ukimwi (ARV).
Kadhalika, alisema kuwa vituo vya kutolea huduma ya dawa vimeongezeka kutoka vitatu mwaka 2005 hadi kufikia 30, mwaka huu.
Aidha, Mratibu huyo wa TACAIDS Mkoa alibainisha kuwa hali ya maambukizi mkoani Singida imepanda kutoka asilimia 2.7 mwaka 2008 hadi asilimia 3.3 mwaka 2012 ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 0.6 tu.
Akihutubia kwenye Maadhimisho hayo, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk Parseko Kone aliwataka wakazi wa Mkoa huu kupima mara kwa mara afya zao kwa hiari ili kujua kama wapo salama au la.
Katika hotuba hiyo iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa Wilaya ya Singida, Queen Mlozi, Dk Kone aliwataka wananchi wa Mkoa wa Singida kujiepusha na visababishi vinavyochochea kuongezeka kwa maambukizi ya ugonjwa huo.
Visababishi hivyo ni pamoja na kuwa na wapenzi wengi, matumizi ya pombe na dawa za kulevya na ngono zembe. Kaulimbiu ya Maadhimisho ya mwaka huu ni “Kuelekea sifuri tatu za maambukizi mapya, Unyanyapaa na vifo vitokanavyo na VVU/ Ukimwi”.
Chanzo;Habari Leo

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2011. Singida Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogz za Mikoa