MWENYEKITI WA KITONGOJI AFUNGWA KWA WIZI


na Jumbe Ismailly, Singida
MWENYEKITI wa Kitongoji cha Miyombwe, Kijiji cha Mkinya, wilaya mpya ya Ikungi amehukumiwa kifungo cha miaka miwili jela baada ya kupatikana na hatia ya wizi wa sh 100,000 iliyokuwa itumike kugharamia ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Kata ya Dungunyi, wilayani hapa.
Mwenyekiti huyo, Michael Khaliki (53) amehukumiwa kifungo hicho na Hakimu Terisophia Tesha wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida.
Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Tesha alisema ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka umethibitisha bila kuacha shaka kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo aliloshitakiwa nalo.
Alisema kutokana na kosa hilo, anampa adhabu ya kulipa faini ya sh 300,000 na akishindwa atumikie kifungo cha miaka miwili jela.
Hata hivyo, mshitakiwa huyo alishindwa kulipa faini hiyo, hivyo kulazimika kwenda kuanza kutumikia kifungo hicho.
Awali, Mwanasheria wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Singida, Antidius Rutayuga, aliiomba mahakama itoe adhabu kali kwa mshitakiwa, ili iwe fundisho kwake na watu wengine wenye tabia kama hiyo.
Kwa upande wake, mshitakiwa Michael aliiomba mahakama imhurumie kwa kuwa ni kosa lake la kwanza na pia ana familia kubwa inayomtegemea.
Katika kesi hiyo, ilidaiwa kuwa Septemba 16 mwaka 2008 katika Kijiji cha Mkinya, mshitakiwa alitumia sh 100,000 kwa matumizi yake binafsi iliyokuwa itumike katika ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Kata ya Dungunyi.
Chanzo: Tanzania Daima

MWENYEKITI WA KITONGOJI AFUNGWA KWA WIZI


na Jumbe Ismailly, Singida
MWENYEKITI wa Kitongoji cha Miyombwe, Kijiji cha Mkinya, wilaya mpya ya Ikungi amehukumiwa kifungo cha miaka miwili jela baada ya kupatikana na hatia ya wizi wa sh 100,000 iliyokuwa itumike kugharamia ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Kata ya Dungunyi, wilayani hapa.
Mwenyekiti huyo, Michael Khaliki (53) amehukumiwa kifungo hicho na Hakimu Terisophia Tesha wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida.
Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Tesha alisema ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka umethibitisha bila kuacha shaka kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo aliloshitakiwa nalo.
Alisema kutokana na kosa hilo, anampa adhabu ya kulipa faini ya sh 300,000 na akishindwa atumikie kifungo cha miaka miwili jela.
Hata hivyo, mshitakiwa huyo alishindwa kulipa faini hiyo, hivyo kulazimika kwenda kuanza kutumikia kifungo hicho.
Awali, Mwanasheria wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Singida, Antidius Rutayuga, aliiomba mahakama itoe adhabu kali kwa mshitakiwa, ili iwe fundisho kwake na watu wengine wenye tabia kama hiyo.
Kwa upande wake, mshitakiwa Michael aliiomba mahakama imhurumie kwa kuwa ni kosa lake la kwanza na pia ana familia kubwa inayomtegemea.
Katika kesi hiyo, ilidaiwa kuwa Septemba 16 mwaka 2008 katika Kijiji cha Mkinya, mshitakiwa alitumia sh 100,000 kwa matumizi yake binafsi iliyokuwa itumike katika ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Kata ya Dungunyi.
Chanzo: Tanzania Daima

CCM Singida yabariki agizo la RC Kone



Na Nathaniel Limu
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Singida, kimebariki amri halali iliyotolewa na mkuu wa mkoa wa Singida, Dk. Parseko Kone, ya kupiga marufuku wafanyabiashara binafsi kununua alizeti moja kwa moja kutoka kwa mkulima.

Baraka hizo zimetolewa na chama hicho katika kikao chake cha halmashauri kuu kilichofanyika Julai 5, mwaka huu mjini hapa.

Kwa mujibu wa tamko la chama hicho lililotolewa na CCM mkoa wa Singida, limeeleza kuwa pamoja na mambo mengine, limebaini kuwa amri hiyo ni halali, haikueleweka vizuri kwa wananchi.

Mbali na hatua hiyo CCM, imeagiza elimu ya kutosha kuhusu amri hiyo, itolewe ili lengo la amri hiyo liweze kutekelezwa kwa makini.

Taarifa hiyo ya CCM imeeleza kuwa, amri iliyotolewa na Mkuu wa mkoa wa Singida Dk. Parseko Kone, haikukataza mtu au kikundi chochote kununua zao la alizeti, isipokuwa imeelekeza kwamba ni vyama vya msingi vya ushirika ndivyo vitakavyonunua moja kwa moja zao hilo kutoka kwa wakulima na kisha kuwauzia wafanyabiashara binafsi.

Awali agizo hilo la Mkuu wa mkoa liliagiza kwamba mbali na vyama vya ushirika kuwepo, yaanzishwe magulio katika maeneo mbalimbali ambayo wakulima wa alizeti watauza kwa watu mbalimbali, kwa kufuata bei elekezi kama njia ya kuwanufaisha moja kwa moja kuliko ilivyokuwa awali.

“Wenye viwanda vya kukamua mafuta, wanaruhusiwa kuanzisha ushirika wao wa kununua alizeti, ili mradi wafuate bei elekezi,” ilieleza taarifa hiyo ya CCM katika tamko lao

Akifafanua zaidi, Dk. Kone, alisema hivi sasa ameteua kamati ambayo itajikita katika kuhakiki uwepo na uwajibikaji wa vyama vya msingi vya ushirika.

“Pia tutachunguza uwajibikaji wa viongozi wa vyama hivyo kuanzia ngazi ya mrajisi wa vyama vya msingi vya ushirika juu ya uadilifu na utendaji kazi wao. Wale ambao wataonekana kuwa kikwazo katika maendeleo ya wakulima wa alizeti, tutawashughulikia mara moja,” alisema RC Kone
Chanzo: Mtanzania

Tamko La CHADEMA Juu Yaliyojiri Singida



CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA)

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


Tamko Kuhusu Yaliyojiri Katika Mkutano wa Hadhara wa CHADEMA Uliofanyika Kata ya Ndago Siku ya Jumamosi Tarehe 14 Julai 2012

1. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kiliandaa mikutano ya hadhara katika Jimbo la Iramba Magharibi. Mikutano hiyo ilitolewa taarifa polisi na jeshi hilo lilitoa baraka zake kama utaratibu wa sheria unavyotaka kwa barua yake ya tarehe 12 Julai 2012 Kumb. Na. KIO/B1/1/VOL.V/268

2. Mkutano wa kwanza ulipangwa kufanyika katika Kata ya Ndago katika viwanja vilivyo karibu na kituo cha mabasi ambapo pia ni hatua chache karibu kabisa na Kituo cha Polisi Ndago. Mkutano huu ulipangwa kuanza saa nane mchana.

3. Msafara wa kitaifa unaofanya ziara ya ukaguzi wa chama, katika mkoa wa Singida chini ya uratibu wa Ofisa wa Sera na Utafiti Makao Makuu, Mwita Mwikwambe Waitara, (ikiwa ni maandalizi ya operesheni nyingine kubwa mkoani humo itakayofanyika baadae), uliwasili katika eneo la Mkutano majira ya saa tisa na nusu alasiri. Tulikuta wananchi wengi wakiwa wanatusubiri. Kabla ya Mkutano kuanza tulipewa taarifa kwamba kuna kikundi cha vijana kimeandaliwa kuvuruga mkutano wa CHADEMA kwa kufanya fujo, ikiwemo kurusha mawe ili mkutano huo usifanyike. Suala hilo lilielezwa mkutanoni mapema na Mheshimiwa Waitara, mbele ya askari polisi.

4. Wakati tukijiandaa kuanza hotuba, vijana wapatao wanane walianza chokochoko kwa kutoa matusi na punde mawe yakaanza kurushwa kutoka sehemu mbalimbali. Wakati fujo zinaanzishwa na kile kikundi, Mheshimiwa Waitara alikuwa bado anazungumza na wananchi kuwaandaa kusikiliza wazungumzaji wengine. Vurumai hiyo ilizimwa na wananchi wenyewe wa Ndago waliokuwa na hamu ya kusikiliza ujumbe wa viongozi wa kitaifa wa CHADEMA.

5. Kwa kweli tunawashukuru wananchi wengi wa Ndago walioonesha ujasiri mkubwa kuweza kuwaondoa vijana wale eneo la mkutano, kisha mkutano ukaendelea, huku wananchi wakionesha kila hamasa ya kufurahia hoja kutoka kwa wazungumzaji, akiwemo Mheshimiwa John Mnyika, ambaye aliombwa ahudhurie ziara hiyo kwa nafasi yake ya Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CHADEMA.

6. Mpaka tunamaliza mkutano huo ambao wananchi waliufurahia sana kwa namna ulivyohutubiwa kwa amani na utulivu huku wazungumzaji wakijenga hoja juu ya mstakabali wa jimbo na taifa lao kwa ujumla, mamia ya wananchi waliohudhuria walitaka tuendelea kuhutubia, lakini tulibanwa na ratiba ya kuwahi mkutano wa pili, eneo la Kinampanda

7. Lakini kutokana na vurugu hizo zilizokuwa zikisababishwa na kikundi cha vijana ambao tayari ilishatolewa taarifa yao kwenye mkutano huo, lakini askari waliokuwepo hawakuthubutu kuchukua hatua, tulilazimika kuomba msaada kutoka kwa OCD na R.P.C, ambapo baadae wakati mkutano unakaribia kuisha tuliona gari la polisi kutoka Mjini Singida likiwa na askari waliojipanga rasmi kwa ajili ya kuzuia vurugu likifika pale eneo la mkutano, lakini wakati huo hali ilishatulia na hotuba zimetolewa vizuri.

8. Kutokana na hali hiyo ya vurugu, zilitolewa taarifa Kituo cha Polisi cha Ndago, ambapo lilifunguliwa jalada NDG/RB/190/2012. Katika jalada hilo tulitaja baadhi ya majina ya watu waliokuwa vinara wa kundi lililokuwa likifanya fujo kwenye mkutano mbele ya askari polisi. Majina hayo ni; 1. Daniel Sima, 2. Tito Nitwa, 3. Bakili Ayubu, 4. Yohana Makala Mpande, 5. Ernest Kadege, 6. Abel John, 7. Athuman Ntimbu, 8. Martin Manase, 9. James Ernest, 10. Simion Makacha, 11. Anton John, 12. Frank Yesaya

9. Kwa hakika askari polisi wa Ndago waliokuwepo mkutanoni mbali ya kutochukua hatua yoyote dhidi ya fujo tulizofanyiwa ikiwemo kupondwa mawe na kikundi kidogo cha wahuni, fujo zilipozidi askari wote walikimbia eneo la mkutano, akabaki OCS pekee ambaye naye alionekana dhahiri kutotaka kuchukua hatua stahili. Hakuonekana kufanya juhudi zozote za kuhakikisha amani inalindwa na ulinzi unaimarishwa katika eneo la mkutano na hatua zinachukuliwa dhidi ya watu walioonekana kudhamiria kufanya fujo. Mtu yeyote makini angeweza kuona kuwa askari wale waliokuwepo pale mkutanoni ‘almuradi’ tu lakini kama vile walikuwa na maelekezo maalum ya kuhakikisha hawachukui hatua yoyote katika kuzuia mpango wowote wa kusababisha vurugu na kuvunja amani.

10. Baada ya kumaliza mkutano wa Ndago kwa amani, tulikwenda Kinampanda ambako tulifanya mkutano mwingine mzuri kwa amani kabisa, ambapo mbali ya wananchi kuwa wametusubiri kwa hamu kubwa na kutusikiliza kwa makini hoja zetu, polisi katika eneo hilo walitupatia ushirikiano mzuri tangu wakati tunafika mpaka tulipomaliza mkutano huo.

11. Jioni wakati tumerudi hotelini, tukasikia kuna taarifa zinasambazaa kuwa kuna mtu/watu wamekufa katika eneo la Ndago. Habari hizo zilikuwa zinakanganya kwa sababu zilikuwa zikitaja idadi tofauti tofauti. Lakini kwa vyovyote vile kama ni kweli kuna tukio la mtu kufariki, CHADEMA tunasikitika sana kwa tukio hilo la uhai wa mtu.

12. Tunalaani taarifa zinazozidi kusambazwa ambazo zinawataja polisi kuwa wanatuhusisha CHADEMA na tukio la mtu aliyefariki. Hii ni ajabu kubwa kwamba tumetoka kwenye mkutano ule kwa amani kabisa mpaka tumemaliza mkutano wa pili kwa amani na polisi wakiwepo sehemu zote mbili, kisha tunasingiziwa masuala ambayo wenyewe hatukuwa na habari nayo tangu mkutano wa kwanza ukiwa unaendelea mpaka mkutano wa mwisho ulipomalizika.

13. Kutokana na habari hiyo ya kifo cha mtu inavyoenezwa kwa kuihusisha CHADEMA, tumebaini kuwepo kwa mbinu na mikakati ya chama tawala pia vyombo vya dola vikihusika kutaka kuwatisha wananchi wa Singida, Watanzania wote wapenda mabadiliko na viongozi wa CHADEMA katika mkoa huu, wasifanye kazi ya kisiasa kwa kuwabambikizia tuhuma na kesi na pia kuwafanya waonekane ni watu wa vurugu.

14. Tunapenda kusema hapa kuwa njama hizo hazitafanikiwa. Zitashindwa kama zilivyoshindwa njama zingine zote ambazo zimekuwa zikifanywa na vyombo vya dola, viongozi wa serikali na chama tawala dhidi ya CHADEMA na vuguvugu la mabadiliko nchini.

15. Tunawataarifu wananchi kuwa ratiba ya kufanya Operesheni nyingine kubwa katika Mkoa wa Singida, ikiongozwa na Katibu Mkuu, Dkt. Willibrod Slaa, itafanyika baadae kama ilivyoazimiwa na kikao cha Kamati Kuu.


Imetolewa leo Singida, Julai 15, 2012 na;

Waitara Mwita Mwikwabe

Afisa wa Sera na Utafiti CHADEMA Makao Makuu

ZIARA YA VIONGOZI WA CHADEMA MKOANI SINGIDA.


Afisa wa sera na utafiti CHADEMA Makao makuu,Waitara Mwita Mwikwabe,akizungumza kwenye mkutano wa hadhara katika kijiji cha Ndago jimbo la Iramba Magharibi.
Mh. John Mnyika (katikati) na baadhi ya Viongozi wa CHADEMA.
Mshauri wa CHADEMA na mhadhiri wa chuo kikuu cha Dar-es-salaam Dk.Kitila Mkumbo akisalimia wakazi wa kijiji cha Ndago jimbo la Iramba Magharibi.
Mbunge wa jimbo la Ubungo jijini Dar-es-salaam John Mnyika akihutubia wakazi wa kijiji cha Ndago jimbo la Iramba Magharibi.
Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Ndago jimbo la Iramba Magharibi,wakiitikia salamu ya CHADEMA ya ‘nguvu ya umma’.
Baadhi ya askari wa FFU walioitwa kutuliza vurugu kwenye mkutano wa hadhara ulioitishwa katika kijiji cha Ndago kwa ajili ya viongozi wa CHADEMA kuzungumza nao.
Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Ndago waliohudhuria mkutano wa hadhara ulioitishwa kwa ajili ya viongozi wa CHADEMA kuzungumza nao.
(Picha zote na Nathaniel Limu).
Kwa Hisani ya Mo Blog

Singida wadhibiti kideri


na Hillary Shoo, Singida
SERIKALI imefanikiwa kudhibiti ugonjwa hatari wa mdondo, maarufu kama ‘kideri’ mkoani hapa, unaoua kwa wingi kuku wa kienyeji, katika halmashauri ya wilaya Singida.
Hayo yalibainishwa juzi na Mkurugenzi wa Maabara Kuu ya Taifa ya jijini Dar es Salaam, Dk. Sachindra Das, wakati akitoa taarifa ya ugonjwa huo, kwenye ukumbi wa chuo cha maendeleo mjini hapa.
Dk. Das alisema kuwa hali hiyo imeifanya halmashauri hiyo na Tanzania kwa ujumla kuongoza katika kudhibiti ugonjwa huo kati ya nchi nne za Afrika, zilizoshiriki kampeni hiyo ya chanjo.
Mkurugenzi huyo, alizitaja nchi zingine zilizoshiriki kampeni hiyo iliyodumu kwa miaka mitatu na kutarajiwa kumalizika Desemba mwaka huu, kuwa ni Zambia, Malawi na Msumbiji.
Alisema kampeni hiyo ilisimamiwa na kamati ya uratibu, mradi wa kitaifa udhibiti wa ugonjwa wa mdondo, kupitia Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, kwa kushirikiana na nchi ya Australia.
Aidha, mmoja wa wafugaji wa kuku wa kienyeji katika wilaya hiyo, Madai Njau, alisema kuwa kabla ya chanjo hiyo kuanza kutolewa, alikuwa akipoteza kuku wengi kutokana na kufa kwa ugonjwa huo.
Njau alifafanua kuwa baada ya kuzingatia sharti la chanjo, hivi sasa ananufaika kwa kiwango kikubwa na kuku wa kienyeji, ambao huuza mayai na kuku kwa wafanyabiashara wa jumla
Chanzo: Tanzania Daima

Kamati yaagiza waachimbaji, mwekezaji kutafuta suluhu


Gasper Andrew,
Singida 
KAMATI ya Ulinzi  na Usalama  ya Wilaya ya Iramba, mkoani Singida, imewataka wachimbaji wadogo wa dhahabu katika eneo la Sekenke wilaya humo,  kufikia mwafaka baina yao na mwekezaji mwenye leseni, vinginevyo sheria ichukue mkondo wake.

Kaimu Mwenyekiti wa  kamati hiyo,  Edward Ole Lenga, alisema agizo hilo linafuatia kushindikana kwa jitihada za kuzisuluhisisha pande hizo kwa njia ya mazungumzo.

 Ole Lenga alisema kushindikana kwa jitihada hizo kumetokana na kitendo cha wachimbaji wadogo, kugoma kusaini makubaliano  kati yao na mwekezaji  John Bina, ambaye amekubali kuingia ubia na  wachimbaji hao katika eneo la leseni yake.

 Ole Lenga ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Singida alisema hatua hiyo imeilazimisha kamati hiyo kuwataka wachimbaji hao, kufikia makubaliano nje ya mazungumzo rasmi.

Alisema vingine, Serikali itachukua hatua za kisheria  kwa mujibu wa taratibu, kanuni na sheria za madini nchini.


Kauli hiyo inakuja wakati Kamishina Msaidizi wa Madini  katika Kanda ya Kati,  Manase  Mbasha, akiwa amesema  wachimbaji hao wakiendesha  shughuli zao kinyume cha sheria na kwamba wanapaswa kushtakiwa.

Wachimbaji wadogo katika eneo la Sekenke, amegoma kuondoka katika eneo  hilo wala kuingia ubia na mwenye leseni,kwa madai kuwa leseni  yake inataja eneo la Mgongo na si Sekenke.
Chanzo: Mwananchi




KKKT Singida wapata askofu mpya


na Jumbe Ismailly, Singida
MKUTANO Mkuu wa Sinodi ya 12 ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kati Mkoa wa Singida, umemchagua Mchungaji Dk. Alex Mkumbo kuwa askofu mpya wa Dayosisi hiyo.
Dk. Mkumbo anakuwa ni askofu wa nne kuiongoza dayosisi hiyo tangu kuanzishwa kwake katikati ya miaka ya themanini.
Katika mkutano huo wa uchaguzi ambao ulifanyika mjini hapa, mchuano wake ulikuwa ni mkali hali iliyolazimisha upigaji kura kurudiwa mara tatu ili kumpata mshindi kati ya Dk. Mkumbo na aliyekuwa akitetea kiti hicho, Mchungaji Eliufoo Sima.
Uchaguzi huo ulisimamiwa na Askofu wa Dayosisi ya Meru, Paul Akyoo na Askofu wa Dayosisi ya Mashariki mwa Ziwa Victoria, Andrew Gulle ambapo wajumbe wa mkutano huo walikuwa 241.
Askofu mteule, Dk. Mkumbo mara kwanza alipata kuwa 135 kisha mara ya pili 137 na mara ya tatu alipata kura 136 dhidi ya kura 105 za mshindani wake, Sima, ambaye naye alipata kura 106 na 105 kwa mara ya pili.
Hata hivyo katika uchaguzi wa nafasi ya askofu msaidizi iligombewa na watu wawili, akiwamo Mchungaji Cyprian Hilinti na aliyekuwa akitetea nafasi hiyo, Mchungaji Yohana Mjungu.
Kwa mujibu wa matokea, Mchungaji Hilinti alinyakua nafasi hiyo baada ya kupata kura 164 dhidi ya kura 77 za mpinzani wake.
Aidha, aliyekuwa mwandishi wa kumbukumbu za vikao katika awamu iliyopita, Victor Bilahama, alishinda kwa kupata kura 165 dhidi ya kura 76 za Joramu Njiku.
Akizungumza baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo, Katibu Mkuu wa kanisa hilo nchini, Brigton Kilewa, aliwataka wajumbe wote wa mkutano huo, kuhakikisha wanaungana na kuwa kitu kimoja.
Chanzo: Tanzania Daima


 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2011. Singida Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogz za Mikoa