Singida kujenga machinjio ya kuku wa asili

WILAYA ya Iramba mkoani Singida inatarajia kuanzisha machinjio ya kuku wa asili ifikapo Julai mwakani.
Mkuu wa wilaya  hiyo bwana Yahaya Nawanda amebainisha hayo Mjini Kiomboi wakati akifungua   mafunzo ya siku mbili juu ya ufugaji kuku kisasa na kuanzisha SACCOS ya  wafugaji kuku
Amesema lengo la machinjio hayo ya kisasa yaliyopangwa kujengwa katika mji wa Misigiri ni kuhakikisha  kuwa kuku wanaozalishwa wanaongezwa thamani kwa kuchinjwa na kusindikwa ili kukidhi mahitaji ya soko badala ya kusafirishwa hai kwa adha kubwa na wengine kufa njiani.
Amesema uamuzi  wa kujenga machinjio  hayo  umefikiwa baada ya kubaini kuwa licha ya ufugaji wa kuku wa asili kuwa moja ya shughuli kuu za kiuchumi mkoani  Singida, kumekuwepo na changamoto mbalimbali.
Amesema miongoni mwa changamoto hizo ni  pamoja na ukosefu wa soko la uhakika na bei nzuri,  uhaba wa madawa na vifo  vinavyotokana na magonjwa na mazingira magumu ya usafirishaji.
Amesema kujengwa kwa machinjio hayo na kunzishwa kwa soko la kuku  pamoja na kituo cha kutoa elimu juu ya ufugaji wa kuku kisasa,  vitasaidia kuwaingiza wananchi kufuga kuku kibiashara ili kujikomboa kiuchumi.
 Inakadiriwa  kuwa zaidi ya kuku milioni  mbili wa  asali  wanafugwa  mkoani Singida.

Bilioni 6.4 zatumika ujenzi wa barabara Singida


ZAIDI  ya shilingi  bilioni 6.4 zimetumika kwa ajili ya shughuli  za  matengenezo ya barabara kuu, mkoa na madaraja  katika mkoa wa  Singida katika kipindi cha kuanzia  Januari hadi  Juni mwaka huu..

Kaimu meneja wa wakala wa baraara TANROADS mkoa wa Singida Mhandisi Yohannes Mbegalo, amebainisha hayo jana wakati akizungumza kwenye kikao cha 35 cha bodi ya barabara.

Mhanadisi  Mbegalo amesema  kuwa  fedha hizo zimetumika  kwa  ajili ya kugharamia  shughuli  za matengenezo ya kawaida kwa upande wa barabara za lami na changarawe zilizopo  mkoani Singida.

Amebainisha baadhi ya shughuli zilizofanyika kuwa ni pamoja na  matengenezo ya sehemu korofi, matengenezo ya vipindi maalum pamoja na matengenezo ya  kawaida na  kujenga makalvati.

Wakala wa barabara mkoa wa Singida,unahudumia jumla ya kilomita 1,689.5 za barabara kuu na zile za mkoa.

Kati ya hizo,kilomita 367.9 ni za lami sawa na aslimia 21.8 na sehemu iliyobaki yenye urefu wa kilomita 1,321.6 sawa na asilimia 78.3 ni za barabara za changarawe  na udongo.


Wanafunzi wabuni kifaa cha kumwagilia


Wanafunzi wawili Fideli Samwel na Jafari Ndagula kutoka shule ya sekondari Ilongero, iliyopo mkoani Singida, wameibuka washindi katika mashindano ya sayansi kwa vitendo iliyoshirikisha mikoa 18 nchini.

Mashindano hayo yalishirikisha wanafunzi 120 kutoka  shule za sekondari 60 pamoja na walimu wao wa sayansi, kwa ajili ya kuonyesha ubunifu na vipaji vya kisayansi ili kuzalisha wataalamu wengi nchini.

Ndagula alizungumza na NIPASHE jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki baada ya kutangazwa kuwa mshindi, alisema kubuni kifaa cha umwagiliaji, hawakuwa na uhakika wa kushinda kwenye maonyesho hayo na kwamba wanamshukuru Mungu kuwafanikisha.

Kifaa hicho kinatumika kama pampu ya kusukuma maji ambayo ina mipira maalumu inayoweza kumwagilia shamba au bustani.

“Unajua mashindano yalikuwa magumu, karibu washiriki wote wamejiandaa vizuri walibuni vifaa ambavyo vinahitajika ndani ya jamii, hivyo tusikate tamaa bali kila mmoja asonge mbele,” alisema. 

Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba alisema katika kuhakikisha vipaji hivyo vinaendelezwa Serikali imetenga Sh. bilioni 26 kwa ajili ya ukarabati wa maabara zake na kujenga zingine kwenye shule zote nchini.

Alisema mpango huo utasaidia kuongeza kasi kwa wanafunzi kujifunza masomo ya sayansi kwa kuwa na maabara za kutosha na za kisasa, pia serikali inajenga mtandao wa ufundishaji (ICT) utakaounganishwa kwenye Mkongo wa Taifa na mwalimu kufundisha kimtandao.

Naye Balozi wa Ireland nchini, Flonnual Gilsenan, alisema Serikali yake itaendelea kulidhamini Jukwaa la vijana wanasayansi Tanzania (YST) ili kuhakikisha linatimiza malengo ya kuzalisha wataalamu.

“Nitaendelea kushirikiana na Serikali yangu kuendeleza ubunifu wa vijana wa Kitanzania kupitia YST, pia naishukuru serikali ya Tanzania kwa ushirikiano wao,”alisema.

Naye Mkurugenzi wa YST, Gozbert Kamugisha, alisema maonyesha hayo yanadhihirisha ubunifu wa hali ya juu kwa Taifa kupata wataalamu wa kutosha, ikiwa fursa hiyo itatumika kuboresha kazi zao.

Alisema YST inasaidia kuwatangaza wasayansi miongoni mwa vijana na kuwapa moyo wa kutafuta ufumbuzi wa matatizo yanayowakabili katika maisha ya kila siku.

Katika mashindano hayo mshindi wa kwanza alipata Sh. milioni moja, medali, kikombe na tiketi ya kwenda kushiriki mashindano ya wanasanyansi vijana nchini Ireland.
 
CHANZO: NIPASHE




Hii Hatari :Vyandarua vyatumika kuezeka vyoo badala ya kukinga Mbu!

DC
Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mkoani Singida Edward Ole Lenga akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kinampundu mara baada ya kukabidhiwa Zahanati na nyumba mbili za mganga na shirika moja lisilo la kiserikali la HAPA,hafla hiyo ilifanyikajuzi kijijini hapo.
SIMAVI
 Ni Mwakilishi wa shirika la SIMAVI kutoka nchini Uholanzi Lieke Ongering akizungumza katika hafla ya kukabidhi mradi wake kwa ushirikiano na shirika la HAPA Singida kukamilisha mradi wa ujenzi wa Zahanati na nyumba mbili za mganga kijiji cha Kinampundu takribani umbali wa kilomita 70 kutoka mjini Singida.
NAPIMA
Ni mmoja wa kinamama wajawazito akipimwa uzito na mkuu wa Wilaya ya Mkalama Ole Lenga mara baada ya kukabidhiwa vifaa vya zahanati hiyo, anayeshuhudia kipimo hicho ni mhasibu mkuu wa shirika hilo Noel Makyao.
VIFAA
Mkurugenzi wa HAPA Davd Mkanje  (Kulia) kimkabidhi DC wa Mkalama Ole Lenga baadhi ya vifaa vya kutolea huduma kwenye Zahanati hiyo wakati wa hafla fupi ya makabidhiano ya mradi huo.
SELEBUKA
Ni baadhi ya wageni kutoka Mataifa mbalimbali nje ya nchi wakicheza muziki na wananchi wa kijiji cha Kinampundu mara baada ya kukabidhiwa mradi huo wa afya ya uzazi wa mama na mtoto.
UKAGUZI
Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Ole Lenga, kushoto mwenye suti, mwakilishi wa SIMAVI, Lieke, MMkurugenzi wa shirika la HAPA, Davd Mkanje na mhasibu mkuu wa shirika hilo Noel Makyao wakifurahia pamoja na wananchi mara baada ya kukabidhi mradi huo.
Na Hillary Shoo, MKALAMA.
Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mkoani Singida ameonya tabia ya baadhi wananchi kuezekea kwenye vyoo vyandarua vya kujikinga na mbu wa malaria.
Onyo hilo limetolewa mwishoni mwa wiki iliyopita na Mkuu huyo wa Wilaya, Edward ole Lenga wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kinampundu muda mfupi baada ya kukabidhiwa Zahanti ya kijiji na shirika la HAPA.
Alisema imezuka tabia ya wananchi kutumia vyandarua hivyo kwa matumizi yasiyo rasmi ikiwa na pamoja na wengine kuvifanya kama mabanda ya kuhifadhi vifaranga vya kuku.
“Hii ni aibu, wenzetu wanatupatia vyandarua  ili tusipate malaria, nyie mnatumia kuezeka vyoo kwa kweli hii ni aibu kubwa sana na mimi nimetembea vijijini na kujionea hili, na kwa kweli atakayekamatwa atakiona cha moto.” Alisema Dc Lenga kwa masikitiko.
Aidha alisema serikali inatumia fedha nyingi kwa ajili ya kuagizi vyandarua hivyo kwa ajili kujikinga na mbu wa malaria huku wananchi wakiziona kana kwamba hazina msaada na kuzitumia kama kinga kwenye vyoo.
“Hivi chandarua kukiezekwa kwenye choo si mtu unaonekana tu , acheni hii tabia chafu, nimeunda kikosi kila kijiji atakayebainika kufanya hivyo akamatwe na kuletwa kwangu mimi nitamshughulikia ipasavyo.” Alisisitza Ole Lenga.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Wilaya aliwataka wananchi wa Wilaya hiyo wanaoishi maeneo ya mijini kuja nyumbani na kujenga nyumba na vyoo bora.

Kwa hisani ya Mo Blog

WFP watoa msaada wa pampu za maji zenye thamani Tsh 94 millioni mkoani Singida


DSC02783
Mkuu wa Ofisi ndogo ya Mpango wa Chakula Duniani (WFP) Dodoma, Nima Sitta akihimiza utunzaji wa matenki ya kuvunia maji ya mvua yaliyojengwa katika shule za msingi wilaya ya Singida na Ikungi. Shirika la WFP limetoa shilingi 95,271,600 kugharamia ujenzi wa matenki hayo.(Picha  na Nathaniel Limu).
Na Nathaniel Limu
Shirika lisilo la kiserikali la Mpango wa chakula duniani (WFP) limetoa msaada wa pampu 210 za maji zenye thamani ya zaidi ya shilingi 94 milioni kwa shule za msingi na vikundi mbalimbali mkoani Singida.
Pampu hizo ni kwa ajili ya kilimo cha umwangiliaji bustani.
Hayo yamesemwa juzi na Mkuu wa Ofisi ndogo ya WFP Dodoma Nima Sitta,wakati akizungumza kwenye hafla ya makabidhiano ya matenki 12 ya kuvunia maji ya mvua yaliyojengwa kwenye shule sita za wilaya ya Singida na wilaya ya Ikungi.Hafla hiyo ilifanyika katika viwanja vya shule ya msingi Igaruri wilaya ya Singida.
Alisema lengo kuu la msaada huo wa pampu za maji,ni kila shule za msingi na vikundi vya vijana,kuanzisha kilimo cha umwangiliaji maji bustani.
Nima alisema kila shule ya msingi yenye chanzo cha maji,itapatiwa pampu si chini ya mbili,wakati vikundi vya vijana waliomaliza elimu ya msingi na wale waliomaliza kidato cha nne,watapatiwa si chini ya pampu tatu.
“Kwa upande wa vijana,kila kikundi kinatakiwa kumiliki ekari sisizopungua tatu na wawe wamejipanga vizuri,shule za msingi zimepewa sharti la kuwa na shariti la kumiliki ekari mbili.Hivi sasa tunaendelea kuzizungukia shule ili zile zenye sifa,ziweze kukabidhiwa pampu mapema iwezekanavyo”alifafanua Nima.
Katika hatua nyingine,Nima alitumia fursa hiyo kulipongeza shirika lisilo la kiserikali la SEMA la mjini Singida, kwa kazi nzuri ya ujenzi wa matenki ya kuvunia maji na inayofanana na thamani ya fedha zilizotumika .
“Kwa kweli SEMA kazi yao ni nzuri mno,wametekeleza kwa kiwango cha juu yale yote ambayo yapo kwenye mkataba na kufanya mazuri zaidi baadhi ya shughuli ambazo hazipo kwenye mkataba.Nisema tu kwamba kazi ya SEMA,inapaswa kuigwa na wajenzi wengine kwa maendeleo ya wananchi”,alisema.

Mkandarasi atishia kujitoa ujenzi wa barabara

KAMPUNI ya China ya Sinohydro imetishia kusimamisha ujenzi wa barabara ya lami ya Manyoni- Itigi mkoani Singida hadi Chaya mpakani mwa Tabora kutokana na kuidai Serikali zaidi ya Sh bilioni 14.7. Madai hayo ni sehemu ya gharama za ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 89.3 kwa kazi ambayo imekwishafanyika.

Hali hiyo inatajwa kuwa moja ya sababu za utekelezaji wa mradi huo kuwa nyuma kwa zaidi ya miezi sita sasa kutokana na mkandarasi kukabiliwa na uhaba wa fedha.

Mkandarasi mshauri wa mradi huo Nicholas Geyer kutoka Ireland, alisema kutokana na madai ya fedha kwa muda mrefu bila mafanikio, shughuli hiyo inaweza kusimamishwa wakati wowote.

Alisema hatua hiyo itakachelewesha zaidi ujenzi na kuigharimu Serikali kwa kulazimika kulipa fidia kwa mujibu wa sheria za mikataba.

Hata hivyo, Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Singida, Yustaki Kangole alisema anaamini Serikali italipa fedha hizo kumuwezesha mkandarasi kuendelea na ujenzi.

Alisema huo ni sehemu tu ya miradi mingi nchini inayodaiwa zaidi ya Sh bilioni 300.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk. Parseko Kone, aliyetembelea ujenzi wa barabara hiyo alisema na kuchelewa suala kubwa ni kuzingatia ubora.

Ujenzi wa barabara ya lami ya Manyoni-Itigi-Mkoani Singida hadi Chaya mpakani mwa Tabora unaogharimu zaidi ya Sh bilioni 100 ulitarajiwa kukamilika Desemba mwaka huu kwa mujibu wa mkataba.
Chanzo: Mtanzania

Halmashauri ya Singida yakusanya mapato ya zaidi ya shilingi bilioni 22 kutoka vyanzo yake mbalimbali.

 Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Singida Jumanne Mnyampanda (katikati) akiongoza kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa chuo cha maendeleo ya wanancvhi mjini Singida. Wa kwanza kushoto ni makamu mwenyekiti halmashauri ya wilaya ya Singida Hamisi Mumbee na kulia ni Mkurugenzi wa halmashauri ya Singida Illuminata Mwenda.
 Baadhi ya madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Singida wakifuatilia kwa makini hoja zilizokuwa zikijadiliwa kwenye kikao cha baraza la madiwani. Kikao hicho kilifanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa chuo cha maendeleo ya wananchi mjini Singida.
Mwenyekiti wa huduma za jamii katika halmashauri ya wilaya ya Singida na diwani (CCM) wa kata ya Msange Elia Digha, akichangia hoja kwenye kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri ya Singida.
Halmashauri ya wilaya ya Singida imekusanya mapato kutoka vyanzo vyake mbalimbali zaidi ya shilingi bilioni 22.9 kati ya Julai mwaka jana na Juni mwaka huu.
Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Illuminata Mwenda amesema hayo wakati  akitoa taarifa yake ya mapato na matumizi kwenye kikao cha baraza la madiwani, kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa chuo cha maendeleo ya wananchi mjini Singida.
 Amesema makusanyo hayo ya mapato ni sawa na asilimia 78 ya lengo la kukusanya shilingi 29,583,444,380 kwa mwaka huo wa fedha.

 Mwenda amesema kuwa vyanzo vya ndani vya mapato, walikusanya zaidi ya shilingi..........
419,000,000 sawa na aslimia 42 ya lengo la kukusanya shilingi 1,004,817,000.
Mkurugenzi huyo amesema serikali  kuu imewapa ruzuku ya kulipia mishahara zaidi ya shilingi 13.8 bilioni na ruzuku nyingine ya zaidi ya shilingi 1.5 bilioni kwa ajili ya matumizi yasiyo ya mishahara.
 Katika hatua nyingine, kikao hicho kimeagiza mkaguzi wa mahesabu wa ndani afanye ukaguzi wa vitabu vya kukusanyia mapato ya ndani kwa watendaji wote wa kata.

 Vile vile mkaguzi huyo, amkague kwa makini Afisa mapato wa halmashauri hiyo anayehusika na kutoa vitabu vya kukusanyia mapato.


 Aidha, kikao hicho kimemwagiza mkaguzi huyo kufanya ukaguzi zaidi kwa watendaji wa kata ya Merya, Itaja, Mudida na Ikhanoda ili kubaini tuhuma zinazowakabili.
Chanzo. Blog ya Singida
 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2011. Singida Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogz za Mikoa