Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
  
 
 
MSICHANA Jackline Lasway maarufu kwa jina la Pendo, mkazi wa eneo la
 Minga Manispaa ya Singida, amenusurika kifo baada ya kumwagiwa uji wa 
moto na mke wa tajiri wake wa dukani kutokana na kile kinachosadikiwa ni
 wivu wa kimapenzi.
Pendo amelazwa wodi namba mbili hospitali ya Mkoa wa Singida, huku 
akiwa na majeraha ya kuungua sehemu ya sikio la upande wa kulia na 
mgongoni.
Akizungumza kwa taabu katika wodi hiyo, Pendo alisema tukio hilo 
limetokea jana mchana wakati akiwa dukani kwa bosi wake aliyemtaja kwa 
jina la Charles Kamnde ‘Frarucha’.
Alisema akiwa anaendelea na kazi yake ya kuuza bidhaa mbalimbali 
dukani hapo, ghafla alitokea mke wa bosi wake akiwa na chupa yenye uji 
wa moto na kutaka kumwagia usoni.
Alisema aligeuka ili uji ule usimwagigikie usoni na ndipo ulimuunguza
 sikio la kulia na mgongoni, ambako baada ya mke wa bosi wake kumkosa 
uso, alitoa kisu kutaka kumchoma kifuani.
“Mimi sikuwa na ugomvi naye wala sijui chanzo cha yeye kufika dukani 
na kufanya hili tukio, maana kama ni kazi mi nafanya kulingana na 
maelekezo kutoka kwa bosi wangu Chale,” alisema.
Alisema katika purukushani za kujiokoa asichomwe kisu, alifanikiwa 
kumkamata mkono mwanamke huyo na kupiga kelele na watu walifika 
kumwokoa.
Hata hivyo, alisema alichukuliwa na bosi wake hadi kituo cha polisi 
mjini Singida na kupewa PF 3 kwa ajili ya matibabu na kuletwa katika 
hospitali hiyo, ambako amelazwa huku akiwa na majeraha makubwa mgongoni.
Muuguzi wa zamu katika wodi namba mbili ya wanawake, Anna Cyprian, 
alisema hali ya mgonjwa huyo inaendelea vizuri na anaendea kupatiwa 
matibabu ya majeraha ya moto aliyopata.
Kwa upande wake mmiliki wa duka hilo, Frarucha, alikiri kutokea kwa 
tukio hilo na kwamba hayuko tayari kulizungumzia, kwani maelezo aliyotoa
 binti huyo yanajitosheleza.
Baadhi ya kina mama waliohojiwa kuhusiana na tukio hilo, wameonesha 
masikitiko yao kutokana na hatua ya mwananmke huyo kumwagia uji msichana
 huyo.
Amina Ramadhani, alisema hicho ni kitendo cha kinyama kwa binti mdogo
 kama huyo na kwamba kama aliona kuna mahusiano ya kimapenzi na mumewe, 
angetumia busara na kumwondoa dukani na siyo kumuunguza kwa uji wa moto.
Veronica Masawe, alisema amesikitishwa na tukio hilo na kuwa 
hakiendani na haki za binadamu, kwa kuwa ni kumdhalilisha msichana huyo 
ambaye alikuwa akifanya kazi kwa ajili ya kujipatia kipato.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Geofrey Kamwela, alithibitisha kutokea
 kwa tukio hilo na kwamba, wanamshikilia mtuhumiwa kwa mahojiano na 
baada ya upelelezi kukamilika atafikishwa mahakamani
Chanzo:Tanzania Daima