Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mfanyabiashara
maarufu nchini na Mbunge wa Singida Mjini (CCM), Mohammed Dewji
(pichani) kwa mara ya kwanza ameingia kwenye orodha ya mabilionea 29,
akiwa tajiri kijana kuliko wote barani Afrika.
Jarida la Forbes la
Marekani limemtaja Dewji (39), katika nafasi ya 24 ya matajiri wa
Afrika akiwa na utajiri wa Dola 1.3 bilioni za Marekani (Sh2.34
trilioni) unaotokana na biashara mbalimbali anazozifanya kupitia kampuni
yake ya Mohammed Enterprises (Metl Group).“Dewji alibadilisha biashara
aliyoanzisha baba yake kutoka uuzaji bidhaa na kuwa na viwanda vya
Metl,” inasema sehemu ya habari inayomuhusu bilionea huyo Mtanzania .
“Alinunua
viwanda vya nguo na mafuta vilivyokuwa vinamilikiwa na Serikali kwa bei
ndogo na kuvifanya viwe na faida zaidi kwa kutumia mtindo wa kisasa wa
menejimenti,” inaongeza ripoti hiyo.
Metl ina viwanda vya
kutengeneza nguo na bidhaa nyingine za matumizi ya binadamu vikiwamo
vyakula, sabuni na vinywaji. Pia ina mapato yanayozidi Dola 1.4 milioni
za Marekani (Sh2.5 trilioni) kwa mwaka.
Katika kampuni hiyo,
ambayo imekuwa na ushindani dhidi ya kampuni kubwa nyingine kama Said
Salim Bakhresa, Dewji anamiliki asilimia 75 ya hisa zote.
Kwa
mujibu wa tovuti yake, Metl inaendesha shughuli za uagizaji na
usafirishaji bidhaa kutoka na kwenda nje, uzalishaji unaohusisha nguo,
vinywaji na vyakula, usagaji nafaka, nishati na petroli na utengenezaji
baiskeli.
Pia inahusika na huduma za simu, fedha, kilimo na pia ina kitengo cha kontena kwenye Bandari ya Dar es Salaam.
Dewji
anashika nafasi mbili juu zaidi ya kada maarufu wa CCM na aliyekuwa
mbunge wa Jimbo la Igunga, Aziz Rostam (50) aliyewekwa nafasi ya mwisho.
Rostam
amefungana nafasi ya 26 na mabilionea wa Nigeria, Abdulsamad Rabiu na
Femi Otedola wenye utajiri wa Sh1.8 trilioni kila mmoja.
Orodha
hiyo ya 29 bora inaoongozwa na bilionea wa Nigeria, Aliko Dangote akiwa
na utajiri wa Dola 15.7 bilioni za Marekani (Sh28.2 trilioni), kiwango
ambacho ni mara moja na nusu ya bajeti ya Serikali ya Tanzania ya mwaka
2014/15.
Forbes linamtaja Rostam kuwa na utajiri wenye thamani ya
Dola 1 bilioni za Marekani (Sh1.8 trilioni), kiwango ambacho kimebaki
pasi na mabadiliko kutoka orodha ya mwaka jana. Rostam anamiliki
asilimia 35 ya hisa katika kampuni ya huduma za simu za mkononi ya
Vodacom.
BBC
BBC
0 comments:
Post a Comment