Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
ZAIDI ya wanawake 9,000 mkoani Singida wamegundulika kuwa wamekeketwa katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.
Daktari Bingwa wa Ushauri wa magonjwa ya Wanawake na Uzazi mkoani
hapa, Suleiman Mutani aliyasema hayo kwenye Jukwaa la Kitaifa la
kuadhimisha Siku ya kupinga ukeketaji lililofanyika mjini hapa.
Dk Mutani alisema, idadi hiyo ya waliokeketwa ni sawa na asilimia
20.8 ya wanawake wote waliokwenda kujifungua kwenye vituo mbalimbali vya
kutolea tiba mkoani humu, kati ya Januari 2013 na Desemba mwaka jana.
“Wanawake 9,386 walibainika kufanyiwa ukeketaji, jambo ambalo ni
kinyume cha sheria na ni ukiukwaji wa misingi ya haki za binadamu, licha
ya kuwa na madhara makubwa ya kiafya” alisema Dk Mutani.
Alitaja madhara yatokanayo na ukeketaji kuwa ni pamoja na kuwa na
uzazi pingamizi wakati wa kujifungua, wanawake kupata shida wakati wa
hedhi, uwezekano wa kupata fistula, kuugua maradhi ya kujamiiana na
kuhisi maumivu makali wakati wa tendo la ndoa.
Dk Mutani alisema pia kuwa madhara hayo ni matokeo hasi yasababishwayo na jamii husika kuendelea kukumbatia mila hiyo potofu .
Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake
(Tamwa), Edda Sanga alisema, madhumuni ya jukwaa hilo ni kutoa fursa kwa
wadau kujadili kwa kina utekelezaji wa maazimio ya miaka iliyopita na
kupanga mikakati na njia bora zaidi za kukabiliana na mbinu mpya za
ukeketaji.
Alitaja mikoa ambayo ni vinara wa ukeketaji na asilimia kwenye mabano
kuwa ni Manyara (71), Dodoma (64), Arusha (59), Singida (51) na Mara
(40).
Mikoa mingine ambayo pia inahusishwa na ukeketaji kutokana na watu wa
makabila yanayoendesha vitendo hivyo kuhamia, ni Dar es Salaam, Pwani
na Morogoro.
Hata hivyo, wadau waliohudhuria kikao hicho walisema kuwa, pamoja na
mikakati mbalimbali, mbinu bora zaidi ni kuwawezesha ngariba kuwa na
miradi ya kipato mbadala ili waache biashara ya kukeketa.
Aidha, walishauri wazee wa kimila katika maeneo husika wahusishwe
kikamilifu katika vita dhidi ya ukeketaji kwa sababu wanaheshimika zaidi
na wana ushawishi mkubwa kwa jamii.
Jukwaa hilo la siku mbili lililoandaliwa na Tamwa, limefadhiliwa na
Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya Watu (UNFPA).
Lilihudhuriwa na wadau kutoka mikoa minane ambayo baadhi ya makabila
yake yanaendesha ukeketaji.
CHANZO: HABARI LEO.