Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
SERIKALI wilayani Mkalama mkoani Singida imeridhishwa na kasi 
inayofanyika kuibadili jamii ya Wahadzabe kutoka kutegemea maisha ya 
ujima na kuanza kuishi maisha ya kawaida yanayoambatana na mabadiliko ya
 mazingira yaliyopo sasa.
Akizungumza na gazeti hili, Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Christopher 
Ngubiagai kuhusu jamii hiyo ambayo chakula chao kikuu ni nyama, mizizi, 
matunda na asali ikiendelea kuishi kwenye viota katikati ya pori, 
alisema Halmashauri ya wilaya hiyo inafanya mapinduzi makubwa hasa kwa 
kufikisha elimu kwa watoto wao.
Wahadzabe ni miongoni mwa makabila madogo zaidi nchini linalopatikana
 kaskazini mwa Tanzania kando ya Ziwa Eyasi kwenye Bonde la Ufa na 
kupakana na uwanda wa Serengeti pia wapo katika wilaya ya Mkalama.
Jamii hiyo inayoaminika kuwa ni ya mwisho kabisa barani Afrika 
inayotegemea uwindaji kwa ajili ya kuishi, inatakiwa kubadilika taratibu
 kutokana na muingiliano wa kasi unaojitokeza na jamii ya wakulima na 
wafugaji wanaowazunguka.
Katika kuwezesha elimu kwa vijana, Halmashauri ya wilaya ya Mkalama 
inatoa chakula, nguo na kuendesha programu maalumu kwa ajili ya 
kuhudumia wanafunzi wa jamii hiyo waliopo katika shule ya msingi 
Munguli, kata ya Mwangeza iliyotengenezwa mahsusi kwa ajili ya watu wa 
jamii hiyo.
Hata hivyo, Mkuu huyo wa Wilaya alisema pamoja na kuwapo kwa 
wanafunzi wa jamii hiyo, shule hiyo pia hutumiwa na watu wengine ambao 
wapo hapo wa jamii ya Kisukuma, Wamang’ati na Wabarbaig.
Pamoja na halmashauri hiyo kutoa mambo hayo muhimu, taasisi za 
kijamii ikiwamo Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (Haydom - 
Mbulu) na asasi ya kiraia ya FFCC hutoa mchango wa chakula kuongeza 
nguvu kwa jamii hiyo kushiriki kikamilifu katika kupata elimu ya 
kawaida.
Ngubiagai alisema watoto wa jamii hiyo wana akili sana kutokana na 
jinsi wanavyoweza kushika kwa haraka kusoma, kuandika na kuhesabu na 
kwamba katika mtihani wa darasa la tatu, watoto wa jamii hiyo walishika 
namba moja hadi 10 huku Wahadzabe wengine wakifanya vyema katika stadi 
mbalimbali.
CHANZO ; HABARI LEO.
0 comments:
Post a Comment