Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
SERIKALI ya Burundi na chama tawala cha nchi hiyo CNDD-FDD imewataka
Watanzania kumuunga mkono Rais John Magufuli katika azma yake ya
kusimamia nidhamu ya viongozi na kuleta maendeleo kwa taifa.
Mkuu wa Wilaya ya Kibago mkoani Makamba nchini Burundi, Juma Albert
alitoa kauli hiyo akiongoza ujumbe wa watu watano wa kiserikali na chama
tawala cha nchini humo, waliohudhuria maadhimisho ya miaka 39 ya
kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), yaliyofanyika kimkoa kwenye
kijiji cha Munzenze, wilayani Buhigwe mkoani hapa.
Albert alisema, Serikali ya Burundi na chama tawala cha CNDD- FDD
imekuwa ikifuatilia mambo yanayofanywa na Rais Magufuli na kwamba,
wanamuunga mkono kwa yale anayofanya ambayo yamekuwa na tija kwa uchumi
wa Tanzania.
Alisema, Magufuli pia amekuwa akilenga kuimarisha uchumi wa nchi yake
sambamba na ustawi wa jirani zake ikiwemo Burundi. Pamoja na hayo
viongozi hao walitoa shukrani zao kwa wananchi wa Kigoma kuendelea
kuwahifadhi ndugu zao katika kambi mbalimbali za wakimbizi, kufuatia
mapigano ya wenyewe kwa wenyewe nchini mwao.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa
Kigoma, Dk Walid Kabouorou aliwataka viongozi wa upinzani kukubali
kwamba uchaguzi umekwisha na CCM ndio mshindi.
Alisema, kutokana na hilo, hawana budi kuungana na kutekeleza Ilani
ya CCM kwa kuhakikisha miradi ya maendeleo iliyopangwa kutekelezwa
inafanikiwa. Awali, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Issa Machibya aliwataka
wananchi kupeleka watoto wao shule ili kuunga mkono mpango wa Serikali
wa kuondoa ujinga kwa Watanzania kutojua kusoma na kuandika.
Alisema, kumekuwa na tabia ya kuwaficha watoto walemavu na kuwanyima
haki yao ya kupata elimu, hivyo aliitaka jamii kuwafichua wote wenye
kuendekeza ukatili huo dhidi ya wenye ulemavu.
CHANZO: HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment